27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Askofu Dk. Shoo atishwa

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) linapita katika wakati mwingine mgumu, baada ya kuibuka mvutano wa jinsi ya kushughulikia sintofahamu ya Sh bilioni 3 za mkopo uliochukuliwa benki kwa mgongo wa kanisa hilo.


Katikati ya mvutano huo, yumo mkuu wa kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo ambaye anaonekana kuwekwa katika kitisho cha kuondolewa katika nafasi yake na kundi linalompinga.


Askofu Dk. Shoo ambaye anajulikana kwa misimamo, ameonekana kutofautiana namna ya kutekeleza uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo kuhusu kuwaondoa baadhi ya watendaji wake kutokana na suala hilo.

Kwa sababu hiyo, baadhi ya viongozi wa kanisa hilo wanaopingana na Askofu Dk. Shoo, wanamwona kama anakingia kifua uzembe na ufisadi ndani ya kanisa.

Jambo hili limeibuka sasa ikiwa ni takribani miezi sita tangu kanisa hilo lifanye Uchaguzi Mkuu Agosti mwaka jana, ambao licha ya kuonekana kuwa wa moto, ulishuhudia Askofu Dk. Shoo akishinda kipindi cha pili.
Askofu Dk. Shoo anatofautiana na Halmashauri Kuu jinsi ya kutekeleza uamuzi wa kuwaondoa naibu makatibu wakuu wa kanisa hilo.


Wakati baadhi ya maaskofu wakitaka watumishi hao waondolewe kama
ilivyoamriwa na Halmashauri Kuu, na kwamba tofauti na hapo ni kuisigina katiba ya kanisa hilo, na hivyo kutishia nafasi yake, Askofu Dk. Shoo kupitia waraka wake aliouandika Januari 31, mwaka huu kwenda katika chombo hicho ambao gazeti hili limeupata, anaona uamuzi huo utasababishia kanisa kesi na gharama kubwa.


“Ikumbukwe kuwa chanzo cha haya yote hadi hapa tulipofika ni mkopo
uliochukuliwa benki kinyemela na watu wanaojifanya wadhamini wa kanisa.


Manaibu makatibu wakuu tunaotaka kuwaondoa kazini katika suala hili
hawajahusishwa na kutuhumiwa popote. Kuna taratibu za kisheria ambazo zimekiukwa katika zoezi hili.


“Watumishi wa walengwa wameonyesha kuumia na kuona kuwa hawatendewi haki. Baadhi yao wamedai kuwa wanaandamwa kwa sababu ya visasi kwa kuwa walitekeleza wajibu wao kwa uadilifu na kukataa kutimiza matakwa ya baadhi ya viongozi waliokuwa na masilahi binafsi (Mfano mmoja ni shauri lililomhusisha mmoja wa viongozi aliyechukuliwa hatua na Halmashauri Kuu mwaka 2014).


“Kamachombochakanisa,HalmashauriKuu inapaswa kujiridhisha kwa dhamira safi kuwa maamuzi yake yanazingatia haki, ukweli na usawa kwa wote.


“Kuwaondoa watumishi hawa kwa njia hii kutasababisha kesi na gharama kubwa zisizo za lazima,” unasomeka waraka huo wa Askofu Dk. Shoo.

Katika waraka huo, Askofu Dk. Shoo anamtaja mmoja wa watumishi wake
anayehusika na masuala ya fedha, ambaye anasema ndiye mlengwa katika
sakata hilo, na kwamba ndiye waliyemtuma kupeleka kesi mahakamani na ni shahidi muhimu kati ya kanisa na benki.


Anasema wamempa ridhaa mwanasheria aendelee na kesi mahakamani kwa kuwa deni linalodaiwa na benki si la kanisa hilo.
“Ushauri wa mwanasheria ni kuwa kuwaondoa kwa sasa kutaathiri vibaya kesi hiyo na kuliweka kanisa katika hatari ya kulipa deni ambalo kwa sasa linafikia Sh bilioni 3. Tunapaswa kupima vizuri na kwa hekima sana faida/hasara kwa kanisa,” unasomeka waraka huo wa Askofu Dk. Shoo.


Zaidi katika waraka wake huo, anasema jambo hilo wameshauriwa sana na wengi wenye taaluma na uzoefu mkubwa, kuwa kitendo cha kuwaondoa viongozi wote wa ngazi ya juu wa taasisi yoyote kwa wakati mmoja kina madhara kwa taasisi kama hiyo.


Katika hilo, Askofu Dk. Shoo ameonekana kushangazwa ama kufunikwa au
kusahaulika kwa ushauri wa kupatikana Katibu Mkuu mpya ambaye atashiriki zoezi la kuwapata wale watakaomsaidia.


Alishangaa mapendekezo ya kutaka waanze kuondolewa naibu makatibu wakuu na hasa akilengwa yule anayehusika na masuala ya fedha.


Pamoja na hayo, Askofu Dk. Shoo ameeleza kuhuzunishwa na agenda ya
kumtaka ama ajiuzulu mwenyewe au aondolewe kutokana na kutofautina
kuhusu kushughulikia suala hilo.


Askofu Dk. Shoo ameitahadharisha Halmashauri Kuu kuchunguza kwa kina kabla ya kutoa uamuzi kuhusu jambo hilo.


Wakati Askofu Dk. Shoo akisema hayo, gazeti hili limedokezwa kuwa
Halmashauri Kuu katika vikao vitano iliamua kuwaondoa Katibu Mkuu na
manaibu wake katika kile kilichotajwa ni sintofahamu ya ziliko fedha za mkopo huo.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, kanisa linakabiliwa na madeni mengi, likiwamo la mkopo huo toka benki moja inayohudumu Afrika Mashariki.


Hali kadhalika namna ya uendeshaji na taratibu za masuala ya kifedha na zile za malipo, ikiwamo kuingizwa viongozi ambao hawastahili, nayo inadaiwa kuliweka kanisa katika hali ya sintofahamu.


Kutokana hayo, inadaiwa baadhi ya dayosisi zimeamua kutotuma michango yake.


Jana gazeti hili lilifika katika ofisi za Makao Makuu ya kanisa hilo, Arusha lakini hakuna kiongozi yeyote aliyekuwa tayari kuzungumza kuhusu jambo hilo.


Askofu Dk. Shoo na Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Briton Kilewa nao hawakuweza kupatikana.

Juhudi za kuwasiliana nao bado zinaendelea.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,554FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles