Na JANETH MUSHI, ARUSHA
ASKOFU Dk. Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), amewataka wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu nchini, kuifanya elimu wanayopata darasani iendane na maisha halisi ya mitaani.
Askofu Dk. Hotay, alitoa wito huo mjini hapa juzi baada ya kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) juu ya elimu ya dini kutoka Taasisi ya Biblia Japan (JBI).
Akizungumza katika mahafali yaliyohusisha pia viongozi wa dini na watu mashuhuri katika jamii, Askofu Dk. Hotay aliishukuru JBI kwa mkazo wake wa kuzingatia misingi iliyowekwa na Mungu, kwani hakuna jamii iliyofanikiwa kujua mambo yote.
“Jamii yetu inahitaji sana taaluma, lakini tujiulize ni taaluma ya namna gani, kwa sababu elimu duniani kote kwa sasa imetikisika na si Tanzania peke yake.
“Taifa lolote ili liwe salama ni lazima liiweke salama misingi aliyoiacha Mungu. Elimu pekee ya kichwani kama haijaweza kutafsiriwa, basi unaweza kuwa na shahada mbili za kilimo na ukaendelea kulima kama babu asiye na elimu.
“Kwa sasa, Afrika inakabiliwa na hatari ya wanafunzi wa shahada kushindwa kufaulu mtihani unaopima uwezo wa kufikiri kwa asilimia 50, huku nchini Marekani, wahitimu wa shahada wakidaiwa kufikia asilimia 40 ya wanaoshindwa kufaulu mahojiano,” alisema Askofu Dk. Hotay.
Kwa upande wake, Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, Dk. Philemon Mollel, ambaye pia alitunukiwa shahada ya uzamili ya heshima, aliiomba jamii nchini kuthamini mchango unaotolewa na Watanzania wenzao.
Awali, mgeni rasmi katika mahafali hayo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro, alihimiza wahitimu kutumia kalamu vizuri ili kulisaidia taifa.