26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Bagonza azungumzia tetesi kuchomwa kanisa

 FARAJA MASINDE– DAR ES SALAAM

UONGOZI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, umesema umekuwa ukipokea simu nyingi zinazoulizia kuhusu kuchomwa moto kwa kanisa moja katika dayosisi hiyo taarifa ambazo zimeleta taharuki.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, ilisema kuwa hakuna kanisa lolote lililochomwa moto.

“Taarifa hizi zimeleta taharuki miongoni mwa waumini wetu na wananchi kwa ujumla. Napenda kutoa taarifa hii, ili kwa njia hii kupunguza usumbufu wa kuulizwa ulizwa kwa simu ya jambo hili. 

“Hakuna kanisa lolote la dayosisi hii lililochomwa moto. Pia hatuna taarifa zozote toka polisi wala mamlaka yoyote zinazoeleza uwepo wa nia au mazingira ya kuchoma moto kanisa letu. 

“Tumesikia kupitia vyombo vya habari, mamlaka moja ya kiserikali ikisema kuna watu walitaka kuchoma moto kanisa lakini ina mamlaka ikaingilia na kuzuia, taarifa hiyo haikusema ni kanisa gani na wahusika hao ni kina nani. Tunaamini kanisa hilo si letu, kama lingekuwa letu, tungejulishwa kuwa tunalindwa na tungeambiwa wenye nia ya kuchoma kanisa letu ni kina nani na kwanini,” alisema Askofu Bagonza.

Alisema wanazo taarifa za kimaungano, zilizowafikia kuwaeleza kuwa kuna mtu mmoja amekuwa anatumia nafasi yake kuwashawishi vijana wafanye fujo au kuchoma moto kanisa kwa sababu ambazo hawajajulishwa.

“Vijana hawa walikataa mpango huo, kwa kuwa mtuhumiwa ni mtu mwenye nafasi ya muhimu katika jamii, tumeamua kuijulisha mamlaka yake ya kinidhamu aonywe kusudi asivuruge uhusiano mwema wa kihistoria kati ya kanisa na mamlaka anayotumikia, tunaamini akumulikaye mchana, usiku anaweza akakuchoma.

“Kwa kuwa mtuhumiwa huyo mchochezi ni muumini wa kilutherani, tunapenda kumuonya aache. Kama hataki kuacha uchochezi, basi yeye mwenyewe achome kanisa kuliko kusingizia watu wengine wasiokuwepo. 

“Ama atachukuliwa hatua za kisakramenti zenye uwezo wa kumuathiri akiwa hapa au popote atakapokuwa. Mchungaji wake atafahamishwa hatua za kumsaidia hata kumrudisha darasa la kipaimara, sakramenti si haki ya binadamu, ni haki ya muumini mtiifu kwa kanisa na viongozi wake,” alisema Askofu Bagonza.

KUSITISHWA KWA IBADA

Aidha katika hatua nyingine, Askofu Bagonza alisema kuwa Dayosisi ya Karagwe kupitia vikao vyake vya kikatiba, ilisitisha ibada kwa muda wa wiki nne ili kuweka mazingira salama ya kuabudu bila kuhatarisha afya za waumini, na kwamba kazi hiyo imekamilika na miundombinu kuwekwa. 

“Ibada zitarejea Jumapili ya Pentekoste Mei 31, mwaka huu. Katika kufanya maamuzi hayo, katiba ya Dayosisi ilizingatiwa, Dayosisi ya Karagwe kama zilivyo dayosisi nyingine za KKKT, haina mamlaka nyingine juu yake zaidi ya Sinode yake. 

“Waumini wa KKKT-Dayosisi ya Karagwe wanajua na wamefundishwa hivyo katika kipaimara. Hakuna mamlaka nyingine ya kikanisa iliyotakiwa kujulishwa. Tunawaomba ndugu zetu wasio Walutheri muwe na amani katika mambo yenu kama tulivyo na amani na mambo yetu. 

“Aprili 1, 2020 tulianza vita hii kwa maombi ya kidayosisi yaliyowashirikisha watu wote, hatujaacha na hatutaacha, corona bado iko na inaua, hatujui kama inaongezeka au inapungua ila tunajua ipo na inaua,” alisema Askofu Bagonza.

Alisema; “Tutaendelea kutumia silaha zote tulizonazo kupigana vita hii, ikiwamo kutumia imani, akili, kufunga na kufungua makanisa, kutoa elimu na kusisitiza masharti yote.

“Hatuombi watu wafe ili tuonekane tuko sahihi katika maamuzi yetu, ni bora tuonekane tumekosea kuliko kusababisha watu waabudu kwa mashaka. Kuchukua tahadhari siyo woga.

“Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; (Wafilipi 1:18).” 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles