25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Askofu ataka ibada ya Pasaka iadhimishwe kwa kusameheana, kutobambikiziana kesi

Na Dotto Mwaibale-Singida

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Singida, Edward Mapunda, amewataka waumini wa dhehebu hilo kuwa na huruma na msamaha kama kumbukizi na tafakuri halisi ya Ijumaa Kuu katika muktadha chanya wa kumuishi Yesu kwa matendo.

Alisema kuendelea kutendeana vitendo vya kikatili, kutosameheana, kupakaziana, kubambikiana kesi, na kuchafuana kwa namna yoyote ile ni kuendelea kumsulubisha Yesu msalabani.

Askofu Mapunda aliyasema hayo wakati akiongoza mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki walioshiriki ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani hapa juzi.

“Tusitendeane vitendo vya kikatili, na daima tuwe vyombo vya upendo, huruma na msamaha.

“Kifo hiki cha Kristu kinatufundisha upendo wa kweli, huruma ya Mungu kwa namna alivyofuta dhambi zetu na kutuweka huru, lakini pia kuonja msamaha wa kweli,” alisema Askofu Mapunda.

 Alisema kwa mujibu wa Injili ya Yohana kama inavyosimulia mateso hayo, Yesu Kristu alishtakiwa kwa makosa matatu ambayo hakuna hata moja lililokuwa na ukweli.

Shtaka la kwanza ni la kidini, ambapo Yesu alishtakiwa na Wayahudi kwa kujifanya Mwana wa Mungu na shtaka la pili ni la kutamka kuwa atalivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, huku la tatu likiwa ni la kisiasa ambalo ni kesi ya uhaini kwa kujifanya mfalme wa Wayahudi.

“Mashtaka yote haya ni ya uongo, yalilenga kupakaziana, kubambikiana kesi na kuchafuana,” alisema Askofu Mapunda.

Alisema nyakati hizi mambo ya kuchafuana kwenye mitandao na kubambikiana kesi kwa uongo bado yapo kiasi cha baadhi ya watu kuendelea kuozea gerezani kwa kuoneana.

Askofu Mapunda alisisitiza kilichomuua Yesu Kristu kwa mujibu wa Nabii Isaya ni dhambi na uovu wa binadamu.

Alisema kifo cha Yesu msalabani ni mapenzi ya Mungu kwa wanadamu kama chimbuko la kosa lenye heri lililofanywa na Adamu na Eva.

Hata hivyo alisisitiza kifo cha Yesu msalabani ni njia iliyompendeza Mungu kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kumtuma mwanaye ili aje atusafishe dhambi zetu.

“Kwa tukio la leo na daima msalaba ni fahari yetu, ni mti wa uzima, mti wa wokovu na kwamba Wakristu tunapaswa kujivunia msalaba,” alisema Askofu Mapunda.

Hata hivyo, katika jitihada za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, waumini wa kanisa hilo juzi waliabudu na kusujudu msalaba huo mtakatifu kwa tendo la kuinama kwa unyenyekevu tofauti na kuubusu kwa mdomo kama ilivyozoeleka huko nyuma.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles