27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ASKARI WANAOFUATILIA WAUZA UNGA HUTUMBUKIA KATIKA BIASHARA HIYO

Mwandishi Wetu


 

WIKI iliyopita, niliandika kuhusu muuza unga kuwa na uwezo wa kutengeneza mpaka Sh 2.23 bilioni ndani ya miezi miwili, akitokea kwenye sifuri.

Leo pia msome Rick Ross ‘Freeway Rick’ (siyo yule wa Hip Hop), ambaye alikuwa bilionea wa unga na kila mtu alijua.

Askari kanzu (undercover cops) walimfuatilia na kufanikiwa kumkamata na ushahidi. Alihukumiwa kifungo cha maisha jela, ila alipokata rufaa alishinda kwa sababu ushahidi uliokuwapo haukutosha kumtia hatiani.

Hata hivyo, alifanya makubaliano na polisi kwa kukiri kosa, hivyo alifungwa miaka 10 na mwaka 2009 aliachiwa huru.

Katika documentary ya How to Make Money Selling Drugs, iliyoandikwa na kusimuliwa na Mathew Cooke kisha kutengenezwa na Adrian Grenier, Freeway anasema enzi zake alikuwa anatengeneza mpaka Dola za Marekani milioni tatu milioni, Sh 6.7 bilioni kwa siku.

Freeway anasema ubosi wa unga ulimfanya awe tajiri wa polisi na jamii. Alitoa misaada kwa watu na polisi waliokuwa naye, walikuwa na uhakika wa kupata mpaka dola 40,000 Sh 89.4 milioni kwa siku.

 

POLISI WALIMFUATILIAJE?

Kwa kuelezea hilo, kumfuatilia muuza unga si jambo jepesi. Inataka maarifa na usichoke, maana hukatisha tamaa kwa jinsi ambavyo walivyo wepesi kuepuka mitego.

Askari kanzu ambao walimfuatilia Rick Ross, walifanya kazi kwa muda mrefu. Walijichomeka kwenye magenge ya wauza unga na kujifanya na wao ni wauzaji.

Kwa kawaida, wauza unga huwa wana vipimo vyao kubaini kama mtu amejichomeka kuwatega au kweli anauza. Kanuni za uchunguzi ni mbili, ama wakuamrishe uue mtu au wakulazimishe uvute unga.

Katika hilo, askari wengi wameshajikuta wamekuwa mateja, baada ya kulazimishwa kutumia unga kwa nguvu, wapo pia ambao hujikuta wakiwa wamezamia kwenye uuzaji.

Wakili wa Mahakama Kuu Marekani, Erick Sterling ambaye ni mtafiti wa kesi za dawa za kulevya duniani, anasema biashara ya dawa za kulevya ni kesi ngumu kuliko kesi nyingine zote.

Sterling anasema: “Ugumu wa kwanza wa vita dhidi ya dawa za kulevya ni kuwa hakuna mlalamikaji. Kesi nyingine zote huwa kuna walalamikaji. Hata mauaji, ndugu watalalamika ndugu yao kuuawa kisha uchunguzi utaanzia hapo.

“Dawa za kulevya hakuna chanzo cha kuziwezesha mamlaka za serikali kuanza uchunguzi. Inatakiwa mamlaka zenyewe zianze uchunguzi bila uhakika, kwa kuanza kubahatisha kisha zimhisi mtu na kufuatilia nyendo zake mpaka mwisho.” 

 

HATUA YA KWANZA

Mashirika ya kimataifa kwa hatua ya kwanza husambaa maeneo mbalimbali. Mashushushu huzunguka kufuatilia aina ya maisha ambayo watu wanaishi.

Je, watu wanatumiaje fedha zao? Wanapobaini mtu anaishi katika mazingira ambayo si ya kawaida, hususan kifedha, huyo huanza kumfuatilia shughuli zake. Inapoonekana kuna walakini kwenye kazi zake, humwekea mitego.

Mataifa mengi yaliyoendelea yanatumia mfumo unaoitwa snitch (usaliti) kwa lugha za wauza unga, polisi huita Wanyetishaji Wahalifu (Criminal Informants), kwamba anakamatwa mhalifu mdogo na ushahidi.

Kutokana na ule ushahidi, anaahidiwa akubali kuwa snitch kwa kwenda kushirikiana na wenzake halafu awe anatoa taarifa polisi za kusaidia kukamata wale vigogo wa unga, kisha yeye anaahidiwa hatofungwa au anafutiwa kabisa mashitaka.

Njia nyingine ndiyo hiyo ya kutumia askari kanzu ambao huingia kwenye biashara ya unga kama wahusika kweli, mwisho wanasaidia taarifa za kuwakamata wahalifu. Hii ni njia ambayo huhatarisha maisha ya askari wengi lakini imesaidia wauza unga wengi kukamatwa.

Askari wa Uingereza, Donnie Brasco, Novemba mwaka jana, alitangazwa shujaa wa taifa, baada ya kujigeuza mhalifu wa unga kwa miaka mitatu, akilichunguza genge hatari la biashara ya dawa za kulevya na silaha.

Kazi yake hiyo ilifanikisha kukusanya ushahidi na hivi sasa watu 24 walioonekana hawagusiki (the untouchables) wapo jela. Na ukiona mpaka askari amefanikiwa hayo, ujue ameshakumbana na mengi.

USHUHUDA NEW YORK 

Mkuu wa Mamlaka ya Mapambano ya Dawa za Kulevya Marekani (DEA) tawi la New York, Joe Gilbride alipohojiwa kwenye documentary inayoitwa How to Make Money Selling Drugs, alisema kuwa mitandao ya dawa za kulevya inashirikisha watu wasomi wakubwa wa sayansi.

Gilbride anasema kuwa eneo lake wameshakamata pipi nyingi ambazo ukiziona ni zenyewe kabisa. Juu zimefungwa na unaweza kulamba kuthibitisha ni pipi, hata hivyo ndani ya pipi hizo kunakuwa na dawa za kulevya.

“Huwezi kupata pipi nzuri kabisa lakini ndani yake kuna unga kama kazi kubwa haifanywi na wataalamu viwandani,” anasema Gilbride.

Marekani wanahangaika mno. Maofisa wa DEA hutumia pia mbinu ya kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuwashikilia kwa muda kwa mahojiano.

Hayo mahojiano ni kumzungusha mtuhumiwa, kwani kipindi wakimhoji, wakati huohuo DEA kwa kutumia wataalamu wao wa magari, huingiza kifaa maalumu kwenye gari la mtuhumiwa.

Kifaa hicho hufanya kazi mbili, kwanza ni simu, ambayo makao makuu ya DEA husikia kila anachozungumza akiwa kwenye gari, vilevile ni kitambusho cha eneo (GPS Locater), hivyo popote anapokwenda hufahamika kwa mashushushu wa DEA.

Mtuhumiwa anapongia kwenye gari lake huwa hajui kama amewekewa kitu, maana hukuta kila kitu kipo kama alivyoacha. Wakati mwingine DEA huwa hawakamati wahalifu, isipokuwa huyavizia magari ya wahalifu.

Maofisa wa DEA, hufanya kazi kimafia kama ambavyo wauza unga nao hutekeleza majukumu yao. DEA huyafuatilia magari ya wauza unga kwenye maeneo mazuri kisha kuingia ndani na kufunga simu zao pamoja na GPS Locater, hivyo kuwa rahisi kuwafuatilia na kuwakamata wakiwa na ushahidi.

 

ATHARI ZA MSALITI

Wasaliti wengi huwa ni wauzaji wadogo, kwa hiyo hufahamu kuwa wauzaji wakubwa wana fedha na uwezo mkubwa. Hivyo, huamua kujisalimisha na kutoa siri ili kuwa na uhakika na maisha yao.

Inapokuwa hivyo, husababisha polisi kuwa wanapewa taarifa za uongo na wakati mwingine hupotezwa na kwenda kuvamia wasiohusika.

Upande wa pili muuza mkubwa unga hapendi kufuatiliwa. Muuzaji mdogo anapokamatwa hata akiachiwa, wale wauzaji wakubwa humtafsiri kuwa ni msaliti. Kwamba tayari alishakubaliana na polisi ili kuwachoma, kwa hiyo kufupisha mzunguko huwa wanamuua.

Rachel Hoffman alikuwa binti anayesoma Chuo Kikuu cha Florida, Marekani. Alikamatwa na polisi kwa kujihusisha na biashara ya unga mwaka 1980. Alipoachiwa tu, mabosi wake walimhisi tayari ni msaliti, kwa hiyo alipigwa risasi. Wauza unga huwa hawana mchezo.

Vita ya dawa za kulevya huhitaji zaidi ulinzi wa askari waaminifu. Askari wanaweza kufanya kazi nzuri lakini kwa sababu uaminifu ni mdogo, vibaraka huvujisha siri za jeshi kisha wale waaminifu huingia kwenye matatizo ikiwamo kuuawa.

Askari mstaafu wa kikosi cha dawa za kulevya Marekani, Neill Franklin anasema kuwa ukitaka uione dunia chungu basi wauza unga wakugundue wewe ni polisi na ulikuwa unawachunguza.

“Wakipata picha yako na familia yako ujue umekwisha, watakupigia simu uchague mawili, ama ujisalimishe kwao ili wakutumie kuwapa siri za polisi na uwasafirishie dawa au ukatae kisha waje wakuue na familia yako,” anasema Franklin na kukumbuka kifo cha bosi wake, Edward Toatley, aliyeuawa kwa kupigwa risasi baada ya wauza unga kumgundua.

Itaendelea Alhamisi ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles