Askari mbaroni akituhumiwa kupokea rushwa Sh mil 1.5

0
636

Janeth Mushi – Arusha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imewakamata watu wawili akiwamo askari Polisi, Sgt. Michael Njau kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 1.5, akitaka kumsaidia ndugu wa mtuhumiwa apate dhamana na kesi iliyokuwa ikimkabili isifikishwe mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni mpigapicha wa kujitegemea Mohamed Hamis.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Januari 10 mwaka huu katika eneo la Kwa Father Babu, ambako wanadaiwa kubadilisha mazingira ya kupokea rushwa hiyo.

Alidai kuwa askari huyo mwenye namba E2548 ambaye ni mpelelezi wa makosa ya jinai Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya upelelezi wa kesi za jinai, alishawishi na kupokea rushwa kutoka kwa mmoja wa ndugu wa mtuhumiwa ambaye  yupo rumande.

“Askari huyo alimshawishi ndugu wa  mtuhumiwa kumpatia rushwa ya Sh milioni 1.5, ili aweze kumpa ndugu yake huyo dhamana na pia kumsaidia katika shauri lake hilo lisifikishwe mahakamani.

“Njau alikuwa akiwasiliana na mtoa taarifa wetu kupitia kwa Hamis na Takukuru ilifanikiwa kuwakamata wote wawili baada ya kupokea sehemu ya fedha hiyo aliyokuwa amehitaji kupewa,” alisema Wikesi.

Alisema wanatarajia kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani Januari 20, baada ya uchunguzi kukamilika.

“Watuhumiwa bado wako mahabusu na tunatarajia kuwafikisha mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. Askari polisi wako wanaozingatia weledi ila wasiozingatia tutawakamata mpaka waache kupokea rushwa.

“Tunatoa wito kwa wasimamizi wote wa sheria kutenda haki bila ya kuonea watu, kwani wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuonewa na wasimamizi mbalimbali wa sheria ikiwemo askari polisi, rushwa inanyima haki kwa wanaostahili hivyo usikubali kutoa wala kupokea rushwa,” alisema Wikesi.

Akizungumzia utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana, alisema waliwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 22 kwa tuhuma mbalimbali za vitendo vya rushwa na walipokea taarifa 127 zilizosababisha kufunguliwa majalada 36.

Wikesi alisema katika kipindi hicho, mapambano dhidi ya rushwa walifanikiwa kuokoa fedha zaidi ya Sh milioni 29 na shamba la Kijiji cha Ayalabe ambalo liliporwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Masai, lenye ukubwa wa hekari 17 ambalo limerejeshwa kwa wanakijiji hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here