29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

ASKARI 23 WA MWISHO STARS AFCON HAWA HAPA

Na MOHAMED KASSARA

-DAR ES SALAAM

WAKATI  timu ya  Taifa ‘Taifa Stars’ ikitarajia kushuka dimbani leo kuumana na Misri, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki,kocha wa kikosi hicho, Emmanuel Amunike ametangaza wachezaji 23 wa mwisho wataoiwakilisha Tanzania katika fainali za mataifa ya Afrika(Afcon).

Wachezaji waliofanikiwa kusalia katika kikosi  hicho, baada ya tisa kutemwa ni  makipa; Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons).
Mabeki,  Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Ally Mtoni (Lipuli FC) na Aggrey Morris (Azam FC).
Viungo ni Feisal Salum (Yanga SC), Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadida Morocco) na Farid Mussa (Tenerife, Hispania).
Washambuliaji yumo Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Rashid Mandawa (aliyekuwa BDF, Botswana), Abdillah Abdallah Mussa, ‘Adi Yussuf’ (Blackpool, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, Algeria) na nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji). 

Walioengua katika kikosi hicho ni beki Abdi Banda anayeichezea Baroka ya Afrika Kusini, kiungo Shiza Ramadhani aliye kwa mkopo ENNPI ya Misri, mshambuliaji Shaaban Chilunda, kipa Suleiman Salula (Malindi ya Zanzibar), Claryo Boniface kutoka timu Taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, beki David Mwantika kutoka (Azam), Freddy Tangalu (Lipuli FC) Miraj Athumani (Lipuli) na kinda wa Serengeti Boys (U-17), Kelvin John 

Fainali za Afcon zitaanza kutimua vumbi Juni 23 na kufikia tamati Julai 19 nchini Misri.

Kikosi cha Stars kitautumia mchezo wa leo  dhidi ya mafarao hao, kama maandalizi ya fainali hizo.

Stars imepangwa kundi C, pamoja na Algeria, Senegal na majirani zao, Kenya (Harambee Stars).

Itazindua kampeni zake kwa kuumana na Senegal Juni 23, kabla ya kuivaa Kenya, katika  mchezo wa pili, utakaochezwa Juni 27. 

Misri itakayojipima na Stars leo, ipo kundi A, ikiwa na Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) na Uganda.

Mafarao hao watazindua kampeni zao kwa kuumana na Zimbabwe Juni 21, kabla ya kuivaa Uganda ‘The Cranes, Juni 26.

Mara ya mwisho Stars kukutana na Misri ilikuwa Juni 4, 2016 katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon.

Katika mchezo huo, Stars ilikubali kichapo cha mabao 2-0, Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana,  Amunike alisema mchezo huo ni muhimu kwao kwake katika kukijenga kikosi chake kabla ya fainali za Afcon.

“Mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Misri utatupa dira juu ya mwelekeo wetu katika michuano ya Afcon, kitakuwa kipimo kizuri kwetu, wachezaji nimewaandaa vizuri na matarajio ni makubwa ya kufanya vizuri,” alisema Amunike ambaye ni nyota wa zamani wa Barcelona ya Hispania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles