28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Asimulia anavyomudu kuvua samaki huku akiwa haoni

Magesa Moshi mlemavu asiyeona akiwasili mwalo wa Ndolage kuongea na mwandishi wa makala hiiNA VICTOR BARIETY, GEITA

TUMEKUWA tukiamini kuwa Watanzania tuko salama na hakuna mauaji yoyote yanayotokea dhidi ya raia.

Hiyo inaweza kuwa kweli, lakini  kuna matukio mengi ya kusikitisha, mfano mauaji ya wanawake vikongwe, walemavu wa ngozi (albino), watu kuliwa na mamba katika harakati za kujikimu kimaisha kama uvuvi, kuchota maji kando ya ziwa kwa matumizi ya nyumbani na kuwinda. Hata hivyo, Serikali imeshindwa kuonyesha jitihada zozote kuokoa maisha ya watu hao.

Katika makala hii, tutazungumzia juu ya matukio ya wavuvi kuliwa na mamba katika visiwa vilivyoko ndani ya  Ziwa Victoria kwenye mikoa ya Geita, Mwanza na  Kagera.

Katika  Kijiji cha Isaba, kisiwa cha Maisome, Sengerema mkoani Mwanza kuna changamoto nyingi zinazowakabili wavuvi.

Mpaka sasa watu takribani 40 wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati wakivua samaki kutokana na vifaa duni vya uvuvi, lakini pia mazingira hatarishi yaliyopo kando ya ziwa.

Pia kuzamishwa na askari wa hifadhi ya Rubondo baada ya kukamatwa wakivua katika maeneo ya hifadhi hasa Rubondo ambapo zaidi ya wavuvi 30 wanadaiwa kuuliwa na askari hao.

Mbali na hayo, zaidi ya watu 10 wameachwa bila ya viungo vyao kutokana na mikasa hiyo.

Magesa Moshi, ni mlemavu wa macho (haoni), anaelezea changamoto anazozipata katika kazi yake ya uvuvi wa kutumia mtumbwi wa kasia ndani ya Ziwa Victoria eneo la Mwalo wa Ndolage, uliopo katika kijiji cha Kasang’hwa kata ya Butundwe wilayani Geita.

“Sina msaada kutoka kwa mtu yeyote yule, ndia maana nimeamua kuwa mvuvi japo sioni kabisa,” anasema Moshi.

Anasema alizaliwa miaka 35 iliyopita katika Kijiji cha Kabugozo kata ya Nyachiluluma wilayani Geita.

Akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya Mzee Moshi Igaile na kwamba ameanza kazi hiyo akiwa na miaka 28 baada ya baba yake kufariki na hivyo kukosa mwelekeo wa maisha.

“Nilizaliwa nikiwa mzima… nimejikuta sioni nikiwa na miaka 13 baada ya kuugua ugonjwa wa surua,” anasema na kuongeza:

“Wakati naanza kuugua huu ugonjwa wa surua, wazazi wangu walikuwapo na badala ya kunipeleka hospitalini wao walitumia dawa za mitishamba nikajikuta ninalemaa na ninaamini iwapo wangeniwahisha hospitali ningepona.” Anasema.

Anasema kuwa wadogo zake wane pia wanamtegemea yeye hivyo wakati mwingine hufikia hatua hata ya kutamani kufa.

“Nilitamani sana nitangulie kufa, maana wakati baba anafariki mdogo wangu mmoja wa kiume ndio alikuwa ameo.

“Sikuwahi kufikiria kama siku moja nitakuwa na maisha magumu kama niliyonayo sasa kwa kuwa tulikuwa tuinamtegemea baba kwa kila kitu,” anasema.

Anasema baba yake alikuwa mvuvi na mkulima hodari, kifo chake kilikuwa ni pigo kubwa kwani alifia ziwani.

Akizungumzia matukio ya mamba kula watu na namna anavyojikinga, Moshi anasema hutegemea kuongozwa na na watu anaoongozana nao kwa kuwa hali ni mbaya, kila kukicha mamba wanakula watu.

Anasema amekuwa akikumbana na matukio mbalimbali ya kutisha, lakini bado hajakata tamaa ya kuendelea kutafuta fedha.

Moshi anataja matukio aliyowahi kukumbana nayo kuwa ni Aprili 2013 siku ya Jumapili, akiwa yeye na mdogo wake na mtoto wa mjomba wake, walinusurika kugongwa na feri Kastamu ya Nungwe.

“Tulikuwa na mtumbwi tunatega, ilikuwa majira ya alfajiri na tulikuwa watatu, kama si feri kutuona na kusimama ningekufa siku hiyo na wenzangu maana ingetukanyaga na kutuzamisha majini,” anasema.

Anataja tukio la pili  kwamba lilitokea wakati wakivua milago miwili kwenye lutende.

“Nilikuwa na Hindia Isemwile (sasa ni marehemu), pamoja na mdogo wangu Magesa Moshi. “Ilikuwa siku ya Ijumaa saa 8 usiku mwaka 2003, tukiendelea kutega, mara mamba akatokea na kulenga kukamata mkono wangu bahati mbaya au nzuri ikakamata kasia… ikabidi mwenzangu amshambulie kwa kutumia msiki handa ambao hutumika kuchoma majini ili kuwapeleka samaki ulipo mtego na kunasa,” anasema Moshi.

Anasema katika umri wake huo hajawahi kuwaona mamba wanavyofanana kabla na baada ya kupofuka na anafahamu tabia za wanyama hao kupitia simulizi za wavuvi wenzake, hivyo anaomba Mungu isitokee hata siku moja akajikuta yupo kinywani mwa mamba.

Anasema yapo matukio ya mara kwa mara ya kunyeshewa mvua wanapokuwa ziwani wakivua samaki hivyo humtanguliza Mungu hasa pale mvua inapokuwa imeambatana na upepo mkali.

Kutokana na mateso anayoyapata kupitia shughuli zake za uvuvi, anasema iwapo atapata fursa ya kuonana na Rais Dk. John Magufuli, atamuomba amjengee

nyumba na kununuliwa mtumbwi wa injini, ili aajili wafanyakazi ili naye aweze kupata kipato cha kumsaidia na familia yake.

Kuhusu kumudu utambuzi wa masuala mbalimbali ya kimaisha, anasema elimu yake ipo kwenye miguu yake.

“Kisomo changu chote kipo miguuni na ndiyo maana sivai viatu. Nikijua sijaifikia alama fulani ambayo huwa naikanyaga wakati natembea hapo najua nimepotea inabidi nigeuze kurudi nyuma na nikishaifikia ndiyo itanipa welekeo,” anasema na kuongeza kuwa anaweza kuutambua usiku na mchana kwa kuhisi ubaridi.

Anasema anatembea umbali mrefu bila ya tatizo lolote huku akipishana na wenye baiskeli, pikipiki na magari.

“Suala la fedha ndio bado linanichanganya, siwezi kutambua hii ni shilingi ngapi hadi nitakapokwenda kununua kitu na mwenye duka ndiye atakayeniambia.Ikitokea mtu amenidhulumu ugomvi wake huwa si mdogo.

Naye Simba Antoni ambaye ni Mwenyekiti wa Mwalo wa Ndolage anakofanyia kazi Moshi, akizungumzia tatizo la mamba kula watu, anasema Januari 2015 alikula mvuvi ambaye alikuwa mgeni wa eneo hilo.

Mbali na huyo, tukio la pili lilikuwa la mtoto wa miaka saba aliyeliwa na mamba Desemba 2015.

Kuhusu shughuli za uvuvi anazofanya Moshi licha ya ulemavu alionao, anasema alianza kumfahamu alipohamia Ndolage akiwa mlemavu wa macho.

“Niliwahi kumkuta akivua samaki na kwa mara ya kwanza nilishangaa kumuona akivua wakati haoni…sijawahi kumuona akilima bali hutega kwa kutumia nyavu na ndoano.

Naye Baraka John (25), mvuvi na mkazi wa Ndolage, anasema  kaka yake Moshi ambaye ni mtoto wa mjomba wake, wakati akianza shughuli za kuvua samaki miaka 15 iliyopita, alikuta tayari Moshi ni mvuvi.

“Nilimkuta kaka akivua samaki Mwalo wa Ndolage, wakati huo Magesa alikuwa na miaka 25,” anasema.

Naye Mariamu Paulo (21) ambaye ni mke wa Moshi anasema alikubali kuolewa na Moshi kwa kuwa aliona ni binadamu kama wengine.

Anasema kuna siku mumewe alipotea akamtafuta na kumkuta senta ya Kasang’hwa.

“Mume wangu akiwa kazini huwa sina amani moyoni mpaka atakaporudi ndipo nafsi yangu hutulia,” anasema.

Anasema kutokana na tatizo la mamba kuwa wengi katika Ziwa Victoria, amewahi kushuhudia watu watano waliouawa.

“Maisha ni magumu hivyo unaposikia kuwa mwenzako kaliwa mamba unajua ni siku zake zimefika tu,’’ anasema Geresi ambaye ni mdogo wake Moshi.

“Ninaomba Serikali imsaidie kaka yangu, maana akiugua nabeba mzigo wangu na wake… apewe hata usafiri wa injini akinunuliwa hata injini itamsaidia maana wakati mwingine samaki tunaopata wanaishia kuwa kitoweo kwa vile uvuvi wetu ni ule wa ndoano,” anasema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles