TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
ASILIMIA nne tu ya wanaume wamekuwa wakihudhuria katika vituo mbalimbali vya kliniki ya baba, mama na mtoto jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali kuhakikisha uzazi unakuwa salama.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, baada ya kupokea ujumbe wa wabunge kutoka Bara la Asia, Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanaojishughulisha na Idadi ya Watu na Maendeleo, Jamal Kassimu Ali, alisema sera inamtaka manaume kushiriki kikamilifu katika suala la uzazi.
Alisema baada ya kutembelea hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo walibaini uwepo wa wanaume wachache waliofika kupata huduma hiyo.
“Bado ushiriki wa wanaume katika suala la uzazi ni changamoto kutokana na wachache kuhudhuria katika vituo hivyo niwaombe tujitokeze kupata elimu,” alisema Ali.
Kutokana na hali hiyo aliishauri serikali kutenga nafasi ya kutosha kuwawezesha wanaume kujisikia huru wanapokwenda katika vituo hivyo.
Naye Katibu wa chana hicho ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi (CCM), alisema pamoja na serikali kuweka mipango mizuri kupitia sera na sheria, lakini bado mila na desturi pamoja na elimu imekuwa changamoto katika kutekeleza sera ya afya ya uzazi.
“Kwa vijana wa sasa wamekuwa wakipata elimu nyingi kupitia mitandao hivyo kuna muda wanapata zisizo na ukweli,” alisema Kapufi.
Kwa upande wake Mbunge wa viti Maalumu, Suzani Lyimo alisema wamebaini pia kuwapo kwa upungufu mkubwa wa watumishi wa afya katika vituo jambo linalosababisha kukosekana kwa huduma stahiki.