Na HAMISA MAGANGA,
UTAFITI unaonesha kuwa asilimia 90 ya kinamama wanaowakata kucha watoto wao kila baada ya siku kadhaa, hukosea na kuwakata pamoja na nyama za kucha.
Wakati mwingine watoto wenye uelewa, hulalamikia suala hilo kwa baba zao; kwamba mama amemkata kucha vibaya na hivyo kumsababishia maumivu makali.
Jambo hilo husababisha hasira kwa baba ambaye wakati mwingine huzua ugomvi akidhani kuwa mama anafanya hivyo bila kuwa makini, jambo linaweza kuwa kweli au ni kwa bahati mbaya.
Hata hivyo, mzazi hasa mama inapotokea amemkata mwanawe kucha vibaya, hujikuta akiwa na huzuni asijue la kufanya zaidi ya kumpa tu pole mtoto.
Hali hii inadhirisha kuwa wakati mwingine matatizo madogo yanaweza kusababisha migogoro ndani ya familia.
 Kwanini watoto wanapaswa kukatwa kucha mara kwa mara?
Kwa kawaida mtoto hata akiwa na umri mdogo, kucha zake huwa ni ngumu.
Sasa basi, kutokana na umri mdogo alionao, hushindwa kudhibiti harakati zao, hivyo anaweza kujikwaruza ama kumkwaruza mama yake usoni wakati wowote.
Pia, watoto wadogo huwa na tabia ya kuingiza vidole mdomoni, wakiilamba bila kujali wameshika nini au vidole ni vichafu kiasi gani.
Hivyo, anapoingiza vidole mdomoni wakati ambapo kucha zake ni ndefu kuna uwezekano wa kula uchafu uliopo katika kucha na hivyo kujikuta akiugua maradhi ya tumbo na kuathiri afya yake.
Kwa sababu hii, ni muhimu kuosha kucha za watoto au kuzikata kabisa kila zinapokua.
Unapunguza kucha za mtoto kwa muda gani?
Kiwango cha ukuaji wa kucha za miguu na mikono kwa mtoto huwa si sawa. Hata hivyo, ukimwangalia tu kwa macho unaweza kuona ni kwa kiwango gani kucha zake zimekua hivyo zinahitajika kukatwa.
Kucha za mikono kwa mtoto hupaswa kukatwa mara moja hadi mbili ndani ya wiki moja. Wakati kucha cha miguuni zinatakiwa kukatwa mara moja hadi mbili ndani ya mwezi mmoja.
Mama anapaswa kuwa makini na ukuaji wa kucha za mtoto ili kufahamu ni wakati gani sahihi wa kuzipunguza.
Wakati wa kupunguza kucha za mwanao unapaswa kufahamu njia sahihi ili kuepuka kukata na nyama.
Kwanza; hakikisha mwanao amelala kitandani au umeshikilia mikono yake vema, hii huenda ikawa ni njia sahihi.
Pia mama na mtoto mnapaswa kuangaliana ili iwe rahisi kwako kujua kama unamuumiza au la.
Pili, wakati wa kumkata kucha mtoto ni vema ukashika kidole kimoja baada ya kingine ili kuepuka kuvidhuru vidole vingine pindi itakapotokea mtoto amejitingisha kwa bahati mbaya.
Tatu; baada ya kukata kucha za mtoto, unapaswa kuhakikisha nguo ulizovaa au alizovaa mtoto hazina kucha, kwani zinaweza kumwingia machoni au sehemu yoyote ya mwili hatimaye kumdhulu.
Kumbuka kuwa kucha zinapokuwa kubwa sana hadi kufikia hatua ya kuingia ndani ya nyama za vidole pembeni, zinaweza kumsababishia uvimbe na maumivu na hivyo ukajikuta ukitumia muda mrefu kumuuguza.
Inashauriwa kuwa kwa watoto walio na umri wa mwaka mmoja kushuka chini, akatwe kucha wakati akiwa amelala.
Mtoto kuanzia mwaka mmoja hadi miwili, anapaswa kukatwa kucha wakati akiwa amelala huku ananyonya/kunywa maziwa.
Mtoto wa miaka miwili hadi mitatu kwa kawaida huwa anakuwa ameshaanza kujielewa hivyo unaweza kujaribu kumkata akiwa macho huku ukimshauri atulie ili usimuumize.
Wazazi wengi wanadhani kukata kucha za mtoto ni rahisi na hivyo kuifanya kazi hii wakati wowote ule. Ukweli ni kwamba kumkata mtoto kucha kunahitaji umakini wa hali ya juu kwani usipoangalia unaweza kumfanya mtoto alichukie zoezi hilo pindi inapotokea kuwa kila anapokatwa kucha anaumia.