31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia 70 wanaotibiwa JKCI wakabiliwa na tishio shinikizo la damu

Na WARDA LUPENZA (TUDARCo) -DAR ES SALAAM

ASILIMIA 70 ya Watanzania wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wanakabiliwa na tatizo la shinikizo la damu ambalo linasababisha ugonjwa wa moyo.

Akizungumza na MTANZANIA, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Samwel Rweyemamu, alisema kwenye taasisi hiyo wameona wagonjwa karibu 300 kwa siku kwa kipindi hiki toka taasisi imeanzishwa.

Pia alisema wameona wagonjwa 350,000 na ambao wamefanya upasuaji ni 6,000, hivyo Tanzania bado iko kwenye changamoto ya magonjwa ya moyo kama dunia nzima inavyokwenda.  

“Ugonjwa wa moyo unaenda kwa hatua moja baada ya nyingine, ukiwa na presha kubwa sana misuli ya moyo itatuna, moyo utatanuka, kinachofuatia baadaye kama hutatibu presha au ukashindwa kuidhibiti ikawa ya kawaida, itasababisha moyo kushindwa kufanya kazi.

“Kwa hiyo shida ya ugonjwa wa moyo unaweza ukasema ni kubwa sana hususani ule unaotokana na shinikizo la damu,” alisema Dk. Rweyemamu.

Alisema wagonjwa wengi wana viashiria vinavyoonyesha wamekaa na shinikizo la damu kwa muda mrefu bila ya wao kujijua, hivyo kuna wengine walikuwa hawajui kama wana magonjwa kama hayo.

“Mtu anapata ugonjwa wa kiharusi kwa kuwa alikuwa ana ugonjwa wa moyo ambao unasababisha athari kubwa sana.

“Nimemuona mgonjwa mmoja ambaye mishipa ya moyo ina kiashiria cha kuanza kutuna, mwengine vyumba vya moyo vimeanza kutanuka na mmoja ana dalili ya muda mrefu anapata kizunguzungu, dalili ya kutaka kuanguka.

“Huyu angeweza kuanguka muda wowote kwa sababu tumeona mishipa ya damu inashindwa kufanya kazi vizuri, ambao ni ugonjwa wa valvu kubwa ambayo hupitisha damu na wengine wana uzito mkubwa na kisukari,” alisema Dk. Rweyemamu.

Alisema kaulimbiu yao ni mtu mwenyewe kuwa na uamuzi sahihi kuhusu afya yake ya moyo, hivyo anaweza akaamua kutunza moyo wake usiathirike.

Pia Dk. Rweyemamu aliwashauri watu kuacha sigara, kunywa pombe wastani, kufanya mazoezi, kupunguza uzito na kuendelea kunywa dawa zao kwasababu ni vitu ambavyo wanaweza kuvifanya bila gharama yoyote.

Alisema taasisi inatoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe, jinsi gani inaweza kuwakomboa watu na kuwakinga dhidi ya magonjwa makubwa yasiyo ya kuambukizwa kama haya ya moyo.

Dk. Rweyemamu alisema watu wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu lishe, hawajajua wapangilie vipi lishe zao.

Alisema walio wengi wanatumia vyakula vinavyopikwa njiani vyenye mafuta mengi ambavyo vinasababisha ugonjwa wa moyo, hivyo elimu bado inahitajika kuhusu suala la lishe bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles