RIPOTI za kimataifa zinasema watu milioni 10 au zaidi duniani hawana utaifa wowote ule, idadi ambayo ni sawa na ile ya watu wa mataifa ya Norway na Denmark kwa pamoja.
Hali kadhalika, sehemu kubwa ya watu hao milioni 10 wamejikuta katika hali hiyo ya kukosa utaifa kwa makosa au uzembe usio wao.
Hali ya kutokuwa na utaifa hutokea kwa sababu ya ubaguzi dhidi ya makundi fulani katika jamii, kuchorwa upya kwa mipaka ya nchi na kuwapo mianya katika sheria za uraia.
Mbaya zaidi mtu asiye na utaifa hawezi kuishi maisha ya kawaida kama ya mtu mwenye utaifa.
Pamoja na kwamba watu wasio na utaifa wana mazingira yanayofanana, lakini wengi wao hawana kabisa haki za kisheria.
Wengi wao hawatambuliki uwepo wao, hawana vitambulisho, hawana nyaraka yoyote, hawawezi kupata elimu, huduma ya afya, hawawezi kupata ajira halali.
Hali kadhalika wengine hawana hata cheti cha kuzaliwa, hawawezi kupanda ndege bila hati ya kusafiria, hawawezi kufungua akaunti benki, mahali pa kuishi ni shida tupu, hakika hiyo ni hali isiyokubalika kibinadamu.
Watu wanaweza kunyimwa uraia kutokana na sababu mbali mbali, zikiwamo za ubaguzi wa kikabila, wa kimadhehebu na hata wa kijinsia. Hali hiyo pia inaweza kutokea pale mataifa yanaposambaratishwa na vita au mizozo.
Hali hiyo inazidi kuwa mbaya kwani watoto wasio na utaifa wanazaliwa na wazazi wasio na utaifa.
Tatizo hilo limeenea zaidi kusini mashariki mwa Asia, Asia ya Kati, Mashariki mwa Ulaya, Mashariki ya Kati na barani Afrika.
Kutokana na hali hizo, ndiyo maana katika miaka ya karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeanzisha kampeni inayolenga kumaliza tatizo hilo ifikapo mwaka 2024.
UNHCR limesema kupitia kampeni hiyo linataka kuzimulika changamoto wanazokabiliana nazo watu wasio na uraia, na kuyahimiza mataifa kurekebisha sheria zao ili asiwepo mtu anayejikuta katika hali ya kutokuwa raia wa nchi yoyote.
Mkurugenzi wa UNHCR, Antonia Guterres aliwawahi kuwaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba kila baada ya dakika 10 anazaliwa mtu asiye na uraia wa taifa lolote duniani, na kwamba kutokuwa na uraia huwafanya watu hao kuhisi kama kuwapo kwao ni makosa.
Tatizo hilo limeenea zaidi kusini mashariki mwa Asia, Asia ya Kati, Mashariki mwa Ulaya, Mashariki ya Kati na barani Afrika.
Hauwezi kuwa na takwimu sahihi za wasio na utaifa bila kugusia Afrika Magharibi, ambako ni tatizo linaloitafuna mithili ya saratani.
Kwa sababu za kimazingira na kimaumbile ikiwamo mfumo dume, sehemu kubwa ya watu hao wasio na utaifa duniani ni wanawake.
Uwiano huo uko maeneo mengi ikiwamo katika ukanda huo wa Afrika magharibi.
Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (NHRC) nchini Nigeria, inasema kwamba kati ya watu karibu milioni moja wasio na utaifa Afrika magharibi, wanawake wanachukua asilimia 60.
Taifa la Ivory Coast linasemekana kuongoza zaidi kwa kuwa na watu 700,000 wasio na utaifa ambao imechagizwa na sheria zake tangu uhuru.
Sheria hizo ziliwaathiri wale ambao mababu au mababa zao walitokea mataifa mengine jirani hasa Burkina Faso pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha, sheria nyingi katika ukanda huo huzuia wanawake kurithisha utaifa kwa watoto wao na uwapo wa upungufu wa usajiri wa uzazi.
Usugu wa tatizo hili unatokana na ugumu pia wa kubainisha baina ya mtu ambaye hana utaifa na yule ambaye hana nyaraka zinazotambulisha utaifa wake.
Utakuta wanawake ambao waume zao wamekimbia kwa sababu za kijamii au vita, wamejikuta ukimbizini iwe ndani au nje ya taifa lao, kutokana na sheria zilivyo wanajikuta wakikosa utaifa kwa kukosa nyaraka halali za kuwatambua.
Kwa mfano; wanawake wengi wa Burkina Faso hufanya kazi katika migodi ya dhahabu nchini Ivory Coast, lakini hawana uthibitisho wa utaifa wao na hivyo kuongeza hatari ya kukosa utaifa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Oti Ovrawah alifichua hilo mapema wiki hii mjini Abuja wakati wa kusherehekea Siku ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).
Tukio hilo liliandaliwa na Tume kwa kushirikiana na Mtandao wa Taifa wa Taasisi za Haki za Binadamu Afrika Magharibi (NNHRI-WA) na ECOWAS, chini ya kauli mbiu: “Haki za Wanawake na Vijana wadogo.”
“Hali za wanawake walio wakimbizi wa ndani (IDPs) hasa katika makambi inatisha. Idadi kubwa ya wanawake wasio na utaifa Afrika Magharibi pia ni suala lenye kutia wasiwasi,” anasema Ovrawah.
Anataja lengo la kusherehekea siku hiyo ya kwanza ya haki za binadamu ECOWAS ni kuwa na siku maalumu, ambayo raia wa Afrika Magharibi wanaweza kuwasilisha masuala yao ya haki za binadamu yanayowaathiri katika jamii zao mbalimbali.
“Ukiukaji wa haki za binadamu ukanda huu hususani dhidi ya wanawake na watoto ni mkubwa; unaanzia uwapo wa hali mbaya magerezani, mfumo duni wa jinai, upatikanaji wa nafasi za elimu na taarifa na machafuko dhidi ya wanawake hadi upatikanaji wa huduma za afya.”