30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ASILIMIA 34 YA WATOTO HAWANYWI MAZIWA

Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


ASILIMIA 34 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana tatizo la udumavu kutokana na kutokunywa maziwa na kukosa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.

Akizungumza na wadau wa sekta ya maziwa Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Olenasha, alisema hali hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika kwa kiwango kikubwa cha watoto wenye udumavu, ikitanguliwa na Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

 Alisema uchumi wa taifa hauwezi kuimarika wakati watoto wake wakiwa hawana afya bora inayoweza kuwafanya wakafikiri vizuri na kuwa wabunifu katika shughuli wanazozifanya.

“Kutokana na Watanzania wengi kutokuwa na tabia ya kunywa maziwa, Tanzania kila mwaka inatumia Sh milioni 650 kugharamia matatizo yanayotoka na ukosefu wa lishe bora.

“Udumavu hausababishwi na kukosa chakula tu bali ni kukosekana kwa mlo kamili. Ukinywa maziwa hata glasi  moja unakuwa umepata viinilishe vyote kwa wakati mmoja,” alisema Olenasha.

Alisema wastani wa unywaji maziwa kwa kila Mtanzania kwa mwaka ni lita 47, sawa na mililita 131 kwa siku tofauti na kiwango kilichowekwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) cha lita 200 kwa mwaka.

“Haya yote yanatokea wakati Tanzania ni nchi ya pili Afrika kuwa na mifugo mingi, baada ya Ethiopia. Tuna jiografia nzuri ya malisho, kama tukiweza kuitumia vuziri tutalisaidia taifa kuondokana na udumavu,” alisema Olenasha.

Alisema Serikali inatarajia kuzindua kampeni ya kuhamasisha watu kunywa maziwa yenye kaulimbiu ya ‘Okoa jahazi, jenga afya na uchumi kupitia maziwa’.

Olenasha alisema kampeni hiyo ambayo itakuwa ya nchi nzima, itazinduliwa Mei mwaka huu mkoani Kagera na inatarajiwa kugharimu Sh milioni 380.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles