Asha Baraka ataja sababu za kung’oka Twanga

0
1192

Jessca Nangawe

GWIJI wa muziki wa dansi nchini, Asha Baraka ambaye alikua Mkurugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta, ametaja sababu zilizomfanya kukaa pembeni.

Asha Baraka ambaye ameiongoza bendi hiyo kwa zaidi ya miaka 20, alisema ameamua kumuachia majukumu yake Luiza Mbutu kutokana kuwa na mambo mengi.

Akizungumza na MTANZANIA jana alipotembelea ofisi za New Habari Ltd, zilizopo Sinza Kijiweni alisema wameamua kubadili muundo mzima wa bendi hiyo kwa kuhakikisha inafanya kazi kisomi zaidi huku akiamini Luiza atatosha kuvaa viatu vyake akisaidiana na Msafiri Diof pamoja na Chaz Baba.

Alisema kwa sasa anakabiliwa na majukumu ndani ya klabu ya Simba, kujiandaa na kampeni za uchaguzi mkuu kumsapoti rais wa awamu ya tano, kukuza vipaji vya wasanii chipukizi pamoja na kuwa mshauri ndani ya bendi hiyo.

“Nimeachia madaraka ndani ya Twanga lakini haimaanishi ninaondoka, nitabaki kuwa mshauri, hii inatokana na kubanwa na majukumu mengine ya kazi na naamini Luiza Mbutu atatosha sana kuva viatu vyangu,”Alisema.

Aliongeza kwa kuwataka mashabiki wa bendi hiyo kumwamini Luiza kwani amekaa na bendi hiyo kwa miaka 20 na ana uzoefu mkubwa wa kuiongoza na kuifikisha mbali hata zaidi ya yeye alipoifikisha.

Kwa upande mwingine Asha ameiomba Serikali kuhakikisha inawatengea wasanii nafasi za kumbi za burudani ili kuwapa motisha na kurudisha uhai wa bendi nyingi ambazo zimeonekana kupotea kutokana na kukosa sapoti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here