22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

ASHA BALOZI: MWANAMKE SHUPAVU ANAYEMSAIDIA MUME WAKE KUWA JASIRI

Na Sarah Mossi, Zanzibar


KUNA Msemo wa Kiswahili ”Ukimwelimisha mwanamke, umeielimisha jamii” Lakini Wahenga wanao msemo wao unaosema ”Palipo na mafanikio yoyote ya mwanamme, nyuma yake yuko mwanamke jasiri na muelewa”

Mama Asha Balozi ni mfano wa methali hizo za wahenga kwani ni mmoja wa kinamama shupavu wa Tanzania ambao wameolewa na viongozi, Huyu ni Mke wa Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi. Mama Asha ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wake wa Viongozi Zanzibar na wanawake viongozi. Pamoja na kuwa mke wa kiongozi lakini Mwanamke huyu ni mstaafu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na amefanya kazi kwa karibu sana takribani na marais waliopita wa Zanzibar akiwamo, Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi, Marehemu Idrissa Abdulwakil na Dk. Salmin Amour ” Komandoo”

 

Mwanamama huyu pia aliwahi pia kuwa Katibu Muhtasi wa aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha kwa muda wa miaka kumi na baadaye alistaafu kazi baada ya mume wake Balozi Seif Ali Iddi kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Wiki iliyopita Mwandishi wetu SARAH MOSSI alifanya mahojiano na mwanamke huyu nyumbani kwake  nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na yafuatayo ni mahojiano hayo… Endelea…

MTANZANIA: Wewe ukiwa ni mke wa kiongozi hapa Zanzibar, unafikiri wanawake wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto zipi?

ASHA BALOZI: Kwanza mimi licha ya kuwa ni mke wa kiongozi lakini mimi ni mfanyakazi mstaafu wa Serikali nimefanya kazi kwa karibu sana na marais waliopita kwahiyo changamoto za kinamama wa Zanzibar nilikuwa nikiziona na nikizikabili moja kwa moja na kusaidia kuzitafutia ufumbuzi.

Lakini niliweza kusogea kwa karibu zaidi ni pale alipochaguliwa Dk. Ali Mohammed Shen hakupenda mke wake Mama Mwanamwema Shein aanzishe Ngo’s Ikulu. Kwa sababu Ngo’s zina matatizo yake zinadumu pale unapokuwa kwenye madaraka, unapoondoka kwenye madaraka zinakufa na ni moja moja zinaweza kuendelea kuwapo. Na kwa sababu mumeo akiwa madarakani una uwezo wa kumwita yeyote aje kukusaidia, Ngo’s zinakumbwa na mtihani mmoja kwamba wakati wote wewe utafute kitu cha kuwapa watu.

Mama Shein akaniita na baadaye akaniuliza watatuelewaje wanawake pale tutakapokwenda kuwaomba kura, nikamwambia hicho kidogo tutakachopewa na waume zetu tukitumie. Tuwaite wake wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Wake wa wabunge, wawakilishi wanawake na wabunge wanawake na tutoe chetu mfukoni.

Kwa bahati nzuri tukawaita kwa Mama Shein ambaye ni Mlezi wa huu umoja wetu na mimi ni Mwenyekiti wao. Tukakubaliana nao kila baada ya miezi mitatu kila mmoja wetu atoe Shilingi laki moja na kisha tutembee kila jimbo. Lakini kila jimbo tutakalokwenda tuongozwe na yule mke wa mwakilishi au mbunge wa jimbo husika.

Lakini tukasema kwa majimbo ya Pemba ambayo hatukuwa na mbunge wala mwakilishi jukumu hilo tutalibeba mimi na Mama Shein kwa ajili ya kusaidia kinanama na nyie waume zenu wa majimbo mtakuwa mkiendelea kusaidia majimbo kama kawaida.

Tukaenda hivyo kwa kipindi chote na hata kwa vijana. Na katika kusaidia kinamama sisi hatukubagua kwa wanaCCM tu na tunawaambia tunapokuja hatutaki kupelekwa kwenye siasa kwa sababu sisi ni wake za viongozi, CCM, Chadema, CUF na hata wale wasio na vyama wote wetu.

Tunapenda sana kwenda kusaidia hata kwa vile vikundi ambavyo havina mrengo wa kisiasa, sisi tupo kwa ajili ya wanawake wote.

Mara ya kwanza kama mtakumbuka tukio la mabomu ya Gongolamboto tukachanga haraka haraka na kupata kiasi cha Sh. milioni 10  na kuwapelekea waathirika. Baadaye tukaanza kwenda jimbo moja moja na wilayani.

Lkini tatizo tuliloligundua hasa katika kipindi hiki cha pili ni ubunifu, kwa maana ya kwamba unaweza kumsapoti mtu lakini ukirudi baada ya muda akupe mrejesho utamkuta bado yupo pale pale hajasogea mbele na kwa maana hiyo mtakuta hata ule mfuko hauwezi kukua na kwa msingi huo hata ukiendelea kumsapoti mara kwa mara utajikuta unachoka. Lakini pia tatizo lingine ni soko pamoja na namna ya ufungashaji wa bidhaa zinazozalishwa.

Mimi hapa sasa sasa hivi nimetengeneza Green House na nimeshanunua vifaa vyote nasubiri mvua zimalizike. Kwa sababu nimetembelea baadhi ya Green House na wameniambia unapojiunga kwenye umoja wao wala hutafuti soko, yupo meneja masoko kutoka Dar es Salaam ambaye atasambaza kwenye hoteli na utapata order. Anakuja na kununua kama kilo za nyanya, utajikuta katika miezi mitatu unao uwezo wa kukamata Sh. Milioni 20 mpaka 30 na hapo sasa unabadilisha na kufanya kitu kingine.

 

Nimesema nikianzisha hiyo kitu nitajaribu kuwakusanya kinamama na kusema ile kazi ya kwenda kila siku kuwasaidia, tutawaambia kinamama na vijana fanyeni kitu kama hiki na mimi iwe kama ni shamba darasa , waje niwaelimishe. Lakin kwenda kuwapa fedha peke yake hawatofanya kitu.

Katika awamu ya kwanza ya utawala wa Dk. Shein tayari umoja wetu tumeshatoa michango na misaada kwa vikundi 72 vya Unguja na Pemba na katika awamu hii tunayokwenda nayo tumeshatoa michango yetu kwa vikundi kumi.

Tatizo la elimu ya biashara ni kubwa, wataalamu wanasema unapokuwa na mfuko wako wa shilingi laki moja, usitumie laki moja ile ukasema ni matumizi yako lakini fanya ni mtaji. Na hili ni tatizo kubwa la kinamama wetu wa Zanzibar ni kula mitaji.

 

MTANZANIA: Hebu waeleze kinamama ili wafanikiwe na kufika malengo yao wafanye nini?

ASHA BALOZI:  Kitu chochote ni lazima uwe na malengo, mimi tangu nilipokuwa msaidizi wa viongozi waliopita tulikuwa tunasafiri na nilianza kazi wakati ule mshahara ukiwa ni Sh. 300 kwanza nilianza na National Services kwa kiwango cha Sh. 175 hadi mwaka 1970 mshahara wangu ukapanda hadhi Sh. 300.

Nilikuwa na tabia moja ili kufikia malengo yangu ya kile nilichokipanga. Amini Mungu niko tayari kuwalisha watoto wangu wali na sukari na sitotumia fedha ovyo hadi nifikie lengo nililokusudia.

Nilikuwa nasafiri na viongozi  nikajiwekea malengo kwa kila posho ninayopewa basi nikifika Dubai ninunue kitu chochote cha dhahabu hata kama ni pete ya dhahabu. Hakuna kitu chenye thamani kama dhahabu kwa sababu kila mwaka thamani yake inapanda. Na kwa nchi yetu ukiwa na malengo hutoshindwa.

Kilikuwapo kipindi fulani nilikuwa nikialikwa hata sherehe za arusi basi nilikuwa natafuta visingizio vya hapa na pale nisishiriki ile sherehe kwa sababu nilikuwa na lengo la kujenga nyumba yangu kule Mombasa Zanzibar.

Kwa sababu unapoalikwa sherehe unaweza kutumia muda mwingi na fedha kununua nguo mpya na mimi sikuwa na fedha hizo. Lakini sasa wewe mwanamke ukitaka kushiriki kila tukio la sherehe kuanzia Jumatatu hadi Jumapili utajikuta hufikii malengo uliyojiwekea kwani utatumia muda na fedha zako kununua kivazi ili upendeze.

Tatizo kubwa la wanawake wengi hususani wa sasa hivi wanapenda mambo makubwa lakini hawaangalii mbele na ndio maana hao hao utawakuta makazini wengine wanaiibia Serikali.

Mimi nilifika hadi nastaafu kazi sikuwahi kununua gari lakini leo kijana ana mwaka mmoja kazini tayari anamiliki gari na nyumba za fahari. Amepata wapi fedha za kufanya hivyo?

MTANZANIA: Hili tatizo ni kubwa, sasa mmejipanga vipi kuliondoa?

ASHA BALOZI: Sasa wewe utamchukua punda mtoni na kumlazimisha kunywa maji? Kama hataki hatayanywa? Lakini akiwa na kiu kama hujafika kwenye mto atakimbilia ayanywe. Kwa sababu ili ubaini tatizo lako ni lazima kwanza wewe mwenyewe ufkiri kichwani mwako kwamba hili ni tatizo kwangu.

Je, wanawake wenyewe wanafahamu kwamba hili ni tatizo? Mimi na Mama Shein tulikwenda kusaidia kinamama fulani hapo Mangapwani wakasema wanahitaji boti ya uvuvi, tukawapa boti  na mashine, wakatueleza mashine ni ndogo, nikatafuta mashine kubwa. Lakini haikufika miezi mitatu boti ile wakaiuza na fedha wakagawana. Utamsaidiaje mtu kama huyo?

MTANZANIA: Moja ya tatizo kubwa hivi sasa ni vijana kujiingiza kwenye kazi ya kula dawa za kulevya, hili mmefanyaje mkiwa kama wazazi?

ASHA BALOZI: Mimi ninao vijana nimewapeleka Sober House waliacha hata kula dawa za kulevya. Baada ya kutoka Sober House, nikawanunulia boti ya uvuvi na mashine na baadhi nimewaozesha. Nimetumia takribani Sh. milioni nane. Tayari nimenunua boti mbili za uvuvi.

Hao vijana wako kama 21 na tayari wametoka Sober House, lakini cha kushangaza juzi nilipokwenda kuwafuatilia wote wamerudia kula dawa za kulevya. Vijana Zanzibar wanaokula dawa za kulevya wengi wao si watoto wa masikini, unajiuliza tatizo ni nini? Pia na sisi wenyewe hatutaki kubadilika, sasa huyu utamfanya nini?

Wapo vijana wanaotoka kwenye familia za kimasikini lakini ndio wanajitahidi kusoma lakini wale wanaotoka kwenye familia zenye uwezo hawataki kusoma. Siku zote Maisha ya mwanadamu yapo mikononi mwake, akiharibu ni yeye mwenyewe ameyaharibu na akiyatengeneza ni yeye mwenyewe ameyatengeneza. Hakuna mujiza, miujiza yetu sisi ni pale unapoomba msada tutakusaidia baada ya hapo ukajinyanyue mwenyewe. Tunawapa elimu.

Kule Pemba kulikuwa na vijana 20 walitoka CUF wakajiunga na CCM walianzisha NGO’s  ya usafi pamoja na kuelezwa kuwa si wanachama wa CCM mimi hilo halikunisumbua kwani niliona vijana hawa wakijiunga na kujisaidia wao na watoto wao basi mimi nitapata fungu langu kwa Mwenyezi Mungu.

Nliwanunulia vifaa vya usafi vya gharama ya Sh. mlioni 25 na nikawaomba Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wakawapa mkataba ambao kila siku za wikiendi na siku za sikukuu wanakwenda kufanya usafi kwenye Uwanja wa Michezo wa Gombani kisiwani Pemba.

Wamepata pia mkataba wa kufanya usafi katika ofisi za Serikali na nikawaahidi iwapo wakiendelea kufanya vizuri nitawanunulia gari la kukusanya taka taka. Pale sikuangalia mrengo wa chama lakini niliangalia wale vijana ni wadogo na watakachovuna basi mimi kwa Mungu ninalo fungu langu.

 

Rais Magufuli amesema unapokuwa kiongozi usiingize siasa na amesema wazi yeye sasa si mwanasiasa na kwa sababu kila anachofanya hafanyi kwa ajili ya wanaCCM pekee. Ukijenga skuli hasomi CCM bali watasoma watoto wa Watanzania na hata treni hawatopanda CCM pekee. Kwahiyo Magufuli si mwanasiasa. Siasa ni pale wakati wa uchaguzi tu, tukimaliza uchaguzi hakuna siasa. Wote ni watoto wako ni wananchi wako.

Maendeleo wape wote usiwabague, Wazanzibar na Watanzania sote ni ndugu, tukibaguana haileti picha nzuri na hata kwa Mungu hayuko radhi.

MTANZANIA: Zanzibar sasa inapita katika kipindi kigmu cha ubaguzi wa mrengo wa vyama CCM na CUF, ukiwa mama kiongozi changamoto hii unaikabili vipi kuiondoa?

ASHA BALOZI:  Kusema ukweli si wengi wanaofanya hivyo lakini CUF wanafanya hivyo na kama mliwahi kusikia CUF walizuia mpaka watu wa CCM wasichote maji, hawa wanaweza kufanya hivyo. Na sasa hivi umeingia ule Hizbu na ASP.

Na ndio maana nimesema hata hii michango yetu tulipokuwa tukichangia Unguja lakini Pemba tunachangia mara mbili zaidi kwa sababu hali zao ni nzito na Pemba ni kugumu na wanaosababisha ugumu huo ni wenyewe. 

MTANZANIA: Sasa hali hii mtaiondoa vipi?

ASHA BALOZI:  Waliondoe wenyewe waliolizoea, wewe mtu wa nje huwezi kuliondoa.

MTANZANIA: Wewe ni mke wa kiongozi mkubwa wa Serikali, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, unamsaidiaje mume wako kufanya kazi zake kwa ufanisi katika ujenzi wa Taifa?

ASHA BALOZI: Mbona hizo kazi zake mimi ndio nazifanya kabla hata hajawa Makamu wa Rais. Kwa sababu alipotaka kugombea ubunge wa Jimbo la Kitope ni mimi ndiye nilimpa hilo wazo na alikwenda kugombea.

Yeye alikaa nje zaidi ya miaka 30 hata watu walikuwa hawamjui na hata wakati wa kampeni baadhi ya watu walimchafua eti si Mzanzibar lakini nilisimama mimi nikamuombea kura na baada ya kupata akateuliwa Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na hapo sasa akawa si mtu wa kutulia jimboni lakini mimi ndio nilikuwa nikijulikana jimboni kwake.

Yakitokea mazishi nipo, ameumwa mtu nashughulika hospitali lakini nilikuwa nikimpa taarifa za kila siku na ilionekana ingawa hayupo Zanzibar lakini yupo. Na Wazo kubwa mimi nilipata kutoka kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alipokuwa kiongozi hapa Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar wakati huo mimi nilipelekwa pale kwa kazi maalumu kwa muda. Kikwete alisema unapokuwa na jimbo au kazi yoyote pendelea kutumia vyombo vya habari.

Jimbo letu la Kitope sisi lilikuwa ni kama mikia ya Pweza, limeanzia Kiwengwa hadi Fujoni. Sasa ukiwa Kiwengwa yule wa Fujoni hajui kama upo lakini unapotoka kwenye vyombo vya habari ukisaidia yule wa Kiwengwa anajua kumbe upo jimboni.

Tulitumia sana vyombo vya habari na sisi tulikuwa na shule 12 na mpaka hili jimbo linakatwa hakuna mwanafunzi anayekaa chini. Tulihakikisha watoto wetu wa Jimbo la Kitope wote Wanakaa na kusoma kwenye madawati.

Sasa hivi baada ya jimbo kukatwa tumebakiwa na skuli nane na bado hakuna mwanafunzi anayekaa chini. Tunazo Shule za Sekondari tatu na tumehakikisha tumejemga maabara na kuweka vifaa vyote vya maabara na tunayo shule yetu moja hapa imetoa wanafunzi wa Kidato cha Tano ambayo ipo kijijini Skuli ya Fujoni ambayo imeanza mwaka juzi. Siku za nyuma ilikuwa wanafunzi wakifaulu kwenda Kidato cha Tni lazima waende mjini.

MTANZANIA: Unawaeleza nini kinamama wenzako walioolewa na viongozi??

ASHA BALOZI: Mimi ninawaambia jimbo ni lako wewe Mama kwa sababu kura nyingi ni za wanawake na wanawake ndio walezi wa kinababa. Mbunge yuko bungeni miezi mitatu na mpiga kura wako akifikwa na shida aje kwako wewe mama usimkasirikie, mpokee vizuri na kile ulichopewa na mume wako kula mgaiye kidogo na ataondoka na matumaini.

Usikose sehemu ya pili ya mahojiano haya maalumu  Jumatano ijayo……….

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles