25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Asasi za kiraia yaiomba serikali kuziondolea kodi

Cladio Matimo- Mwanza

ASASI za kiraia nchini zimeiomba Serikali kuziondolea kodi ya mapato na ongezeko la thamani kwa sababu zinatekeleza majukumu yake bila kutengeneza faida bali zinatoa huduma kwa jamii.

Ombi hilo lilitolewa jijini hapa juzi na Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),   Onesmo ole Ngurumwa, wakati akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wa asasi hizo kwenye mkutano wa tano wa mwaka wa wakurugenzi wa asasi za kiraia uliobeba dhima ya kodi zinazohusiana na azaki na mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Alisema asasi za kiraia zinakabiliwa na changamoto za utekelezaji wa sheria za kodi ikiwemo ya mwaka 2015, inayozitaka kulipa kodi ya mapato na ongezeko la thamani wakati zinapata fedha kutoka kwa wafadhili ambazo ni za walipakodi katika mataifa yao na miradi wanayoitekeleza inalinufaisha taifa na Watanzania kwa jumla.

“Kodi zingine tunalipa hatukatai kabisa ikiwemo ya mishahara, lakini inayotokana na faida sisi hatutengenezi faida ukizingatia wanaotufadhili wanatupa fedha za walipakodi katika nchi zao kwa hiyo, huwezi tena kuzipiga kodi mara mbili.

“Mchango wa asasi za kiraia katika taifa hili ni mkubwa, lakini hatutambuliwi hata kwenye taarifa za maendeleo wakati tunatoa ajira, tunaleta fedha za kigeni, tunalipa kodi, tunajenga shule na hospitali, mfano hospitali ya rufaa ya Bugando imejengwa na asasi za kiraia za kidini hizi zilimsaidia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kupata uhuru,” alisema.

Akijibu hoja ya ombi hilo kwa niaba ya mgeni rasmi Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phlip Mpango, Kamishna wa Sera za Bajeti, Shogholo Msangi, alisema hakuna nchi yoyote duniani inayotoa msamaha wa kodi bila kuwa na vigezo hivyo, alizitaka asasi hizo kufanya shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji zikifuata sheria za nchi na kuwasilisha mapendekezo na maoni juu ya sheria za kodi katika wizara hiyo ili yafanyiwe kazi.

Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Andrew Komba, alizitaka asasi za kiraia kurasimisha shughuli zao zote ili ziweze kutambulika kwenye ripoti za Serikali na kuzisaidia mamlaka kujua mambo yanayopaswa kupewa msamaha wa kodi.

Mkutano huo uliofanyika jijini Mwanza kwa siku mbili Oktoba 13 na 14, pia ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na miaka 30 ya uwepo wa asasi za kiraia nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles