Asas yatoa mashine za kisasa kupambana na corona stendi

0
657
Ofisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas, Cosmas Charles

Na Mwandishi Wetu -Iringa

STENDI Kuu ya mabasi ya Igumbilo na stendi ya zamani mkoani Iringa,  zimekabidhiwa msaada wa mashine ya kunawia mikono ya kisasa kutoka Kampuni ya Asas ili kupambana na ugonjwa wa corona.

Mashine hizo za kisasa zinazotumiwa na miguu kutoa maji na vitakasa mikono ni kubwa zinazoweza kuhudumia watu sita kwa wakati mmoja.

Zimekabidhiwa na mwakilishi wa kampuni hiyo, Ofisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas, Cosmas Charles  kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri kwa wenyeviti wa stendi hizo.

Alisema Kampuni ya Asas Group imeimarisha huduma ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa abiria wanaotumia stendi kuu za mjini Iringa kwa kuongeza mashine za kisasa za kunawia mikono kwa lengo la kuhudumia wananchi wengi zaidi.

Charles alisema mashine hizo zenye uwezo wa kuhudumia watu sita kwa mara moja kwa kila moja zimetolewa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Igumbilo, mjini Iringa na stendi kuu ya daladala zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mjini humo.

“Kama kampuni tumelenga maeneo yenye mikusanyiko mikubwa, tukianzia na stendi kuu za mjini Iringa, baadae tutaenda kwenye maeneo mengine ambayo pia yana mikusanyiko mikubwa ya watu ndani na nje ya mkoa kwa lengo la kusaidia jamii kupambana na maambukizi ya corona,” alisema Charles.

Alisema kampuni pia imetoa msaada wa ndoo maalumu za kunawia mikono, barakoa na vitakasa mikono kwa makundi mbalimbali ya jamii mjini hapa, wakiwemo madereva wa daladala, bajaji na bodaboda.

Mwenyikiti wa Stendi ya Igumbilo, Mwinyi Mwaugali alisema wanakumbana na changamoto kubwa ya uhaba wa vifaa vya kunawia mikono kwenye stendi  kutokana na kuwa kubwa.

Askari wa usalama barabarani wa kituo kikuu cha daladala, Koplo Rashid aliwataka abiria na watu wengine wanaotumia kituo hicho kuitumia mashine hiyo ili kujinusuru na janga hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here