Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan amepongeza juhudi za kampuni ya ASAS kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kulinda tamaduni za Kitanzania kupitia udhamini wa Tamasha la Kizimkazi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa tamaduni, mila na desturi za Kitanzania kuwa msingi wa maendeleo ya taifa, akieleza kuwa kupenda kisichokuwa cha Kitanzania ni sawa na utumwa.
Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati akifunga kilele cha Tamasha la Kizimkazi, lililofanyika Unguja, Zanzibar, likiwa na kaulimbiu “Kizimkazi Imeitika.” Tamasha hilo, ambalo lilifanikishwa kwa sehemu kubwa na kampuni ya ASAS, liliwaleta pamoja wananchi kwa burudani za aina mbalimbali, kuanzia taarabu asili na ya kisasa, Bongo Fleva, Singeri, hadi ngoma za asili. Hili lilikuwa na lengo la kuimarisha mshikamano kati ya ndugu wa pande mbili za Muungano.
“Kama taifa, tunapaswa kuhakikisha kuwa maendeleo yanayoletwa na sekta binafsi kama ASAS yanaendana na tamaduni, mila, na desturi zetu. Kupenda kisichochetu ni utumwa, na kupenda chetu ndiyo uungwana,” alisema Rais Samia, akitoa shukrani kwa ASAS kwa mchango wao katika kuendeleza utamaduni wa Kitanzania.
Rais Samia alikumbushia pia miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisema kuwa taifa limeweza kujenga umoja na uzalendo miongoni mwa wananchi wake. Alisisitiza kuwa tamasha kama Kizimkazi lina nafasi kubwa katika kudumisha Muungano na kuendeleza urithi wa tamaduni za Kitanzania, ambao ni msingi muhimu wa Muungano wetu.
ASAS pia imetumia tamasha hilo linaloendelea kujizolea umaarufu kutambulisha bidhaa yake mpya ya maziwa ya unga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ASAS, Ahmed Asas, amesema bidhaa hiyo mpya ni mwendelezo wa kuendelea kuwajali wateja wao kote nchini.
Juhudi za ASAS katika kudhamini matamasha kama Kizimkazi zinaonyesha jinsi gani sekta binafsi inaweza kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa taifa, huku ikisaidia pia kukuza uchumi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.