IOWA, MAREKANI
MWIMBAJI wa Injili kutoka Marekani, Fidel Murua, amewashukuru wapenzi wa muziki huo kwa mapokezi makubwa ya wimbo wake, Asante aliomshirikisha Rose Muhando.
Fidel ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiitangaza Injili kupitia muziki, ameweka wazi furaha yake ya kushirikiana na mwimbaji mkongwe barani Afrika, Rose Muhando kwenye wimbo huo unaofanya vizuri kwa sasa.
Aidha wakati wa kufanyika kwa wimbo Asante, wakiwa studio mwimbaji Rose Muhando alimpa baraka nyingi Fidel kwa kutumia vizuri kipawa chake cha kuimba na kuchagua kumtumikia Mungu.
“Mapokezi yamekuwa makubwa sana, namshukuru Mungu kwa hatua hii ya kuweza kufanikisha kufanya wimbo wa pamoja na Rose Muhando, video tayari ipo kwenye chaneli yangu ya YouTube kila mmoja anaweza kwenda kuitazama,” amesema Fidel.