Asakwa kwa kumiliki kadi 21 za kupigia kura

0
974
amanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa, akiwaonyesha waandishi wa habari kadi bandia za kupigia kura zilizokutwa katika nyumba anayoishi mtuhumiwa Yusuph Makarani wakati wa msako uliofanyika juzi huko Kerege Bagamoyo.

Na GUSTAPHU HAULE -PWANI

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamsaka Yusuph Makarani (50) mkazi wa maeneo ya Kitonga, Kerege wilayani Bagamoyo kutokana na tuhuma za kukutwa na kadi feki za kupigia kura ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake  jana kuwa tukio la kukamata nyara za Serikali lilitokea Mei 7, mwaka huu huko Kerege.

Nyigesa alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, kuna mtu tapeli ambaye amekuwa akitapeli wananchi mashamba eneo la Mapinga kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali.

Alisema baada ya taarifa hizo, askari wake walikwenda haraka katika nyumba ambayo mtuhumiwa alikuwa anaishi na kufanya upekuzi  ambao ulisaidia kukamata kadi feki za kupigia kura 21.

Nyigesa alisema kadi hizo zilikuwa hazijajazwa taarifa yoyote, lakini zimewekwa nembo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku nyaraka nyingine zikiwa ni mihuri 10 ya viongozi wa vitongoji mbalimbali, fomu za mauziano ya ardhi na vitabu saba vya stakabadhi ya malipo.

“Tulipofanya upekuzi wetu katika nyumba ya mtuhumiwa, tumekamata kadi feki 21 za kupigia kura zikiwa mpya hazijajazwa kitu pamoja na nyaraka mbalimbali za Serikali,” alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema mtuhumiwa alifanikiwa kukimbia kabla ya kukamatwa na polisi wanaendelea kumtafuta ili achukuliwe hatua za kisheria.

Kamanda Nyigesa aliwatahadharisha wananchi kuwa wawe makini wanapotaka kununua ardhi kwa kuwashirikisha viongozi wa Serikali wa eneo husika, wakiwemo wenyeviti wa vijiji na maofisa kata, kwa  kufanya hivyo kutasaidia kupunguza utapeli.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo linamshikilia Hassan Malubara (30) mkazi wa Dunda kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya (mirungi) kilo 17.

Kamanda Nyigesa alisema tukio hilo lilitokea Mei 9, mwaka huu, saa 11 jioni  huko Zinga wilayani Bagamoyo.

Alisema wakati polisi wakiwa katika msako wa kudhibiti biashara haramu, walimkamata mtuhumiwa akiwa amepakia mirungi kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 216 BBP aina  ya Boxer rangi nyeusi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here