23 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Arteta awataka mashabiki viwanjani

LONDON, ENGLAND 

BAADA ya timu ya Arsenal kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester United, kocha wa timu hiyo Mikel Arteta, amewataka mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi viwanjani kushuhudia makubwa.

Juzi Arteta alipata ushindi wake wa kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Manchester City ambapo alikuwa kocha msaidizi, lakini kwenye mchezo huo dhidi ya United timu ya Arsenal ilionekana kuwa kwenye kiwango cha hali ya juu tofauti na michezo iliyopita chini yake.

Arteta anaamini uwepo wa mashabiki wengi uwanjani unasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nguvu wachezaji kutokana na timu hiyo kuwa kwenye wakati mgumu msimu huu.

Mashabiki walianza kukata tamaa na timu yao chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Unai Emery, lakini kwa sasa chini ya Arteta timu inaonekana kuwa na mabadiko jambo ambalo limeanza kuwapa nguvu mashabiki.

“Ushindi dhidi ya Manchester United ni furaha kubwa sana kwetu, najivunia kuona wachezaji wangu wakipambana kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kuipigania timu, tangu mwanzo wa mchezo hadi mwisho nimeona timu ikiwa kwenye mabadiliko ya hali juu.

“Lakini nashukuru sana kwa sapoti ya mashabiki ambayo wameionesha, ukweli ni kwamba wameonesha wanaipenda timu yao, hivyo wanatakiwa kujitoa kwa wingi ili kuzidi kuwapa nguvu wachezaji na wachezaji wenyewe wapo tayari kuwapa furaha mashabiki wake,” alisema Arteta.

Kutokana na ushindi huo wa juzi, Arsenal wanashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi baada ya kucheza michezo 21 na kupata pointi 27, hivyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 38, amedai atapambana kuhakikisha timu hiyo inarudi kwenye ubora wake na ikiwezekana kwenye nafasi nne za juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles