30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Apandikizwa mbegu za mwanamke, ajifungua mjukuu

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 61 mkazi wa Jimbo la Nebraska, Cecile Eledge, amewashangaza wengi baada ya kujifungua mjukuu wake.

Mtoto huyo ni mjukuu wake kwa sababu alipandikiziwa mbegu za mwanawe wa kiume aitwaye Matthew.

Tukio hilo linafanana na lile la Sherri Dickson (51), mama wa Kimarekani aliyeamua kumzalia mwanawe wa kike aliyeshindwa kushika ujauzito, na hivyo kujitolea kuwa ‘surrogate mother.’

Tukirejea kwa Cecile, huo haukuwa uamuzi wa kukurupuka kwani alifanya hivyo baada ya mazungumzo na kisha kukubaliana na mumewe, Elliot Dougherty.

Mpango ulikuwa ni kupata mtoto atakayetokana na familia yao tu, na si atokee mtu mwingine wa nje. Ndipo Cecile alipomwambia mwanawe, Matthew, waende hospitali kwa ajili ya zoezi hilo la kupandikiziwa mbegu.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kiasi hicho mbele ya madaktari kwani vilikuwapo vigezo walivyovitaka, ikiwamo umri wa mwanama huyo, kabla ya kuifanya kazi hiyo.

Wakati Matthew akichangia mbegu, dada yake aliongeza yai, hivyo kwa pamoja vilipachikwa kwa mama yao huyo.

Baada ya madaktari kumaliza kazi yao, Cecile alibeba ujauzito kwa miezi tisa, kabla ya kujifungua katika Kituo cha Afya cha Nebraska.

Akizungumza baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, mwanamama huyo alisema: “Hakukuwa na kusita hapo. Ilikuwa ni kawaida tu.”

Kwa mujibu wa taarifa ya madaktari, alijifungua mtoto wa kike mwenye afya njema, uzito wake ukiwa ni kilogramu tano na gramu zaidi ya 360.

“Tumefurahishwa na kila kitu kilivyokwenda,” alisema Matthew, baba mwenye mtoto huyo waliyempa jina la Uma.

“Tumefurahi kuona Uma na bibi yake wote wako hapa wakiwa na furaha na afya tele. Kwa sasa, tunakwenda kutulia na kusherehekea,” aliongeza Matthew.

Alisisitiza kuwa timu yote, kuanzia madaktari hadi wasaidizi wao, walionesha weledi na moyo wa kujitoa kwa kiwango kikubwa.

Licha ya kufanya hivyo, bado Cecile hamfikii Maria del Carmen Bousada de Lara, ambaye ndiye mwanamke anayeshikilia rekodi ya kujifungua akiwa na umri mkubwa zaidi.

Akitumia mfumo huo wa kisasa wa kupandikiziwa mbegu na kuchangiwa yai, Mhispania huyo aliandika historia hiyo mwaka 2006, alipojifungua mapacha akiwa na umri wa miaka 66 na siku 358.

Bahati mbaya ni kwamba alifariki mwaka 2009, chanzo kikiwa ni saratani ya kizazi. Hiyo ililazimu watoto wake hao wa kiume wahamie kwa mpwa wake anayeendelea kuwalea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles