33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ANTHOY KOMU: MBUNGE ANAYEKERWA NA ELIMU BURE

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


BAADA ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilifanikiwa kushinda katika baadhi ya majimbo nchini.

Chadema kama vilivyo vyama vingine vya siasa nchini, kwa sasa kinaendelea kuwatumikia wananchi kupitia maeneo waliyoshinda likiwamo Jimbo la Moshi Vijijini linaloongozwa Anthony Komu.

Katika mahojiano na MTANZANIA yaliyofanyika jana mjini Dodoma, mbunge huyo anaeleza shughuli zake jimboni pamoja na siasa kwa ujumla.

“Jimbo langu lina kata 16 na katika kata hizo, tunaongoza kata 15 na kata moja inaongozwa na CCM.

“Unaweza ukajiuliza CCM walipenyaje katika kata hiyo, lakini ukweli ni kwamba, kuna ujanja fulani ulifanyika ambapo mgombea wetu alijitoa dakika za mwisho na kumwacha mgombea wa CCM apite bila kupingwa.

“Pamoja na ujanja huo, nakuhakikishia CCM siioni ikinyanyuka Moshi Vijijini kwa sababu wananchi wanahitaji mabadiliko ya kweli yanayoweza kuwafikisha wanakotaka kufika.

“Najua Chadema hatuna hatimiliki ya kuongoza Moshi Vijijini, lakini tutazidi kuongoza jimbo hilo kwa sababu tunatekeleza wanayotaka wananchi na ninashirikiana nao vizuri.

“Kwa mfano, nimekuwa nikishiriki kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa makanisa na shule za makanisa na miradi mbalimbali na ushahidi wa hilo, Oktoba 7 mwaka huu, nitakuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa hosteli ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Natiro, ambako zinatakiwa shilingi milioni 42,” anasema Komu.

Akizungumzia jimbo hilo kwa ujumla wake, anasema wakati anaingia madarakani, alilikuta likiwa na hali mbaya kwa kuwa baadhi ya mambo yalikuwa hayaendi vizuri.

SEKTA YA ELIMU

Akizungumzia sekta hiyo, Komu anasema anakerwa na sera ya elimu bure kwa kile anachosema imerudisha nyuma sekta ya elimu jimboni kwake.

“Kati ya mambo yanayonikera ni hii sera ya elimu bure. Nasema hivyo kwa sababu pamoja na Serikali kuamua kufanya hivyo, fedha inazotoa kwa ajili ya kuendesha shule ni ndogo na hazitoshi kwa namna yoyote.

“Kabla ya elimu bure, sisi tulikuwa na utaratibu wetu wa kutoa fedha za kuwalisha watoto wetu shuleni na tulikuwa tukitoa fedha za walinzi na mitihani ya majaribio ya kila mwezi.

“Baada ya sera hiyo, sasa mambo yamesimama na naamini elimu inaangamia kwani CCM wameshindwa kuitekeleza ingawa sera hiyo inatekelezeka kama watajipanga vizuri.

“Kwa upande wa shule za msingi, wakati naingia madarakani hali ilikuwa mbaya kwani kuna baadhi ya shule hazikuwa na vyoo kabisa ingawa ni za muda mrefu,” anasema Komu.

Katika mazungumzo yake, mbunge huyo anaizungumzia Shue ya Msingi Kimanganuni yenye wanafunzi 270 na walimu 14 ambayo anasema haikuwa na choo enzi za uongozi wa mbunge wa CCM .

Kwa mujibu wa Komu hivi sasa shule hiyo ina choo kilichojengwa kwa Sh milioni 37 kwa nguvu za wananchi wakiwamo wakazi wa jimbo hilo waliosoma shuleni hapo.

“Tunajenga pia katika Shule za Kifuni, Shule ya Msingi Mkomongo, Shule ya Msingi Ngilishi, Shule ya Msingi Ngumeni na Katika Shule ya Sekondari Mnini,”anafafanua.

SEKTA YA AFYA

Akizungumzia sekta hiyo, anasema mbunge aliyemtangulia alishindwa kuimarisha sekta hiyo kwa kuwa miradi mingi ya afya ilikuwa haitekelezwi.

“Katika sekta hiyo, jitihada za kuiimarisha zilikuwapo lakini zilikuwa hafifu. Kwa mfano, Kituo cha Afya Shimbwe chenye gharama ya Sh milioni 100 kilikuwa na tatizo la uwepo wa umeme katika baadhi ya majengo.

“Kwa hiyo, nilichokifanya ni kutafuta fedha kupitia Mfuko wa Jimbo na sasa umeme uko katika maeneo yote na mambo yanakwenda vizuri.

“Hata Zahanati ya Kirereni ilikuwa ikifanya kazi katika kiwango kisichoridhisha hasa katika kitengo cha mama na mtoto baada ya kukosekana kwa Sh 500,000.

“Kituo hicho hakikuwa pia na shimo la uchafu na miradi hiyo, ilikwama kwa sababu inasemekana wananchi walichanga fedha zao kisha zikaliwa na wajanja, hivyo wakakata tamaa ya kuendelea kuchangia,” anasema.

SEKTA YA MAJI

Katika sekta hiyo, anasema kulikuwa na tatizo la miradi kukwama, lakini baada ya kuingia madarakani, amefanikisha kujenga chanzo cha maji cha Kishingoshayo kwa fedha za wananchi waliochangia Sh milioni 14 huku mwekezaji akitoa Sh milioni 42.

Pamoja na hayo, anasema mifereji ya umwagiliaji iliyokuwa haitumiki ukiwamo mfereji wa Makeresho, umeanza kufanya kazi ingawa si kwa kiwango kinachoridhisha.

SEKTA YA BARABARA

Kwa upande wa sekta hiyo, anasema amefanikiwa kuwahamasisha wananchi ambapo kila Jumatatu wanashiriki shughuli za maendeleo ya pamoja kupitia kauli ya msalagambo. Kutokana na hali hiyo, anasema idadi kubwa ya barabara zinapitika ingawa bado jitihada zinaendelea.

BUNGENI

Akizungumzia chombo hicho cha kutunga sheria, Komu anasema kimetekwa na wabunge wa CCM kwa kuwa ni wengi kuliko wabunge wa upinzani.

“Bunge ni kama la chama kimoja kwa sababu tunashindwa kutoa uamuzi sahihi hata kwa mambo ya kitaifa.

“Kinachofanyika katika chombo hicho, ni wabunge wa CCM kuangalia masilahi ya chama chao na jambo hilo ni tatizo kubwa linalotuumiza sisi na Watanzania kwa ujumla.

“Kwa hiyo, nawaomba wananchi wawachague wagombea wa upinzani mwaka 2020 ili tuweze kufika tunakotakiwa kufika,” anasema.

UCHAGUZI MKUU 2020

Kuhusu uchaguzi huo, anasema nafasi ya CCM kushinda ni ndogo kwa sababu wamezidisha ugumu wa maisha kwa Watanzania.

“Sioni CCM wakishinda 2020 kwani hata mbinu walizotumia kushinda mwaka 2015, hazitafanikiwa kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi.

“Katika nchi hii kwa sasa wakulima wanalia, wafugaji wanalia, wavuvi wanalia, wafanyakazi wanalalamika, wasomi wamekata tamaa, wanafunzi wamekata tamaa pia na kila mmoja amechoshwa na kupanda kwa gharama za maisha.

“Kwa hiyo, naamini CCM hawatashinda tena kwani hawatakuwa na cha kuwaambia wananchi wakati wa kampeni,” anasema.

POMBE ZA VIROBA

Kuhusu uamuzi wa Serikali wa kupiga marufuku biashara hiyo, mbunge huyo anayeunga mkono katazo hilo, anasema halikufanyika kwa ustaarabu kwa sababu wafanyabiashara wengi wameingia hasara kwa kuwa wengi wao walikuwa na mikopo benki.

NGUVU YA LOWASSA

Kuhusu mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chadema, anasema alikuwa bora na mwenye nguvu kisiasa kuliko wagombea wote wa urais walioshiriki uchaguzi huo.

“Lowassa alikuwa bora na hadi sasa ni bora kwa sababu ana rekodi za kipekee zikiwamo za kupeleka maji Shinyanga kutoka Ziwa Viktoria, ujenzi wa shule za kata na kufanikisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Udom,”anafafanua Komu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles