29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Anthony Mtaka: Buriani Mkapa, pumzika rafiki yangu

 ANTHONY MTAKA

NIMEBAHATIKA kupata fursa kadhaa kukaa na kuzunguma na Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa katika uhai wake.

Fursa ambayo sitaisahau ni ile ya mazungumzo kati yetu iliyodumu kwa takriban saa 10 wakati alipokuja shambani kwake Turiani Morogoro Novemba, 2014 wakati huo nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero.

Kupata wasaa wa saa 10 ya mazungumzo na Rais Mkapa ni jambo adhimu na la nadra sana. Mazungumzo yale yalinijenga na kunikomaza kiuongozi.

Nilipata fursa ya kujifunza mambo ya msingi kutoka kwake na kupata ufafanuzi juu ya maoni mengi tofauti juu yake ambayo ama nilipata kuyasoma magazetini au kuyasikia.

Tulizungumza mambo mengi yahusuyo uongozi na hatma ya nchi yetu.

Nilitumia wasaa huo kumuuliza na kujadili naye baadhi ya mambo aliyopata kuyazungumza katika hotuba zake kabambe wakati alipokuwa Rais na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, ikiwemo ile aliyoitoa kwenye Halmashauri Kuu ya CCM ya Agosti 2004 maarufu kama “Ushupavu wa Uongozi” (The Courage of Leadership); na nyingine aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa 2005 wa kuchagua Mgombea Urais wa CCM. Maswali yangu wakati huo yalilenga kupata maoni yake iwapo hoja nyingi alizoibua wakati ule zingeweza kukidhi matakwa ya siasa za kuelekea mwaka 2015 ambao ulikuwa ni wa Uchaguzi Mkuu uliokuwa unafuata.

Nilitaka pia kujua maoni yake kuhusu mtazamo wake na hisia juu ya uamuzi wa kuwaondoa wazee (wenyeviti wastaafu, makamu wenyeviti wastaafu na makatibu wakuu wastaafu) kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM.

Katika hili, jibu lake lilikuwa uamuzi ule ulitokana na mapendekezo ya wazee hao wenyewe kuomba wapumzishwe kwenye vikao hivyo vya juu vya chama.

Alinieleza, sababu zao kubwa zilikuwa mbili. Kwanza, waliona busara kumpatia Rais na Mwenyekiti wa chama aliyeko madarakani uhuru zaidi wa kuongoza.

Pili, kuondoa dhana iliyokuwa ikijitokeza kila walipopata udhuru na kutohudhuria kuhisiwa na vyombo vya habari kwamba wamesusia vikao vya Mwenyekiti.

Ushauri wao ulikuwa ni kuundwa kwa Baraza la Wazee ili kukidhi dhima yao ya kutoa ushauri.

Aidha, alinieleza kuwa uamuzi ule uliwaondoa tu kuwa wajumbe wa kudumu wa vikao vya chama lakini haukuondoa uwezekano wa wao kualikwa kwenye vikao hivyo kwa mwaliko maalum.

Udadisi wangu haukuishia hapo. Nilimuuliza pia mtazamo wake juu ya maoni ya wengi juu ya mafanikio ya sera yake ya ubinafsishaji. Alinifurahisha kujua kuwa amekuwa akisoma na kuona namna jambo hilo lilivyopokewa na wachambuzi mbalimbali.

Kilichomshangaza yeye ni namna ambavyo wapinzani wa sera hiyo ama kwa makusudi au kwa kupitiwa walijikita tu kwenye mifano ya maeneo ambayo ubinafsishaji haukwenda vizuri.

Alishangaa kwa nini watu hao hawakutoa pia mifano mizuri ya ubinafsishaji kama ile ya Benki ya NBC iliyozaa Benki ya NMB, Kiwanda cha Sigara (TCC), baadhi ya viwanda vya sukari vinavyofanya vizuri na maeneo mengine.

Tukiwa bado kwenye eneo hilo, nilimuuliza kwa nini aliamua kubadili noti na sarafu alipoingia madarakani. Jibu lake lilikuwa, uamuzi ule ulilenga kuwashawishi wale waliokuwa wamehodhi fedha majumbani mwao kuzirudisha benki.

Kwa maelezo yake uamuzi ule ulikuwa wa mafanikio, kwani fedha iliyorudi benki ambayo ilikuwa nje ya mzunguko ilikuwa ni zaidi ya ile iliyokuwapo katika benki zetu.

Jambo lingine nililotaka kupata mtazamo wake ni ule utamaduni wa kukabidhi kofia ya uenyekiti wa chama kwa Rais mpya (kuunganisha kofia mbili) kabla ya miezi 24 ya kwanza kuisha, yaani kabla ya Mkutano Mkuu wa Chama kikatiba.

Maelezo yake yalikuwa kwamba kipindi hicho ndio muafaka zaidi wakati Rais mpya akiwa bado kwenye fungate la kisiasa (political honeymoon). Baada ya muda huo, Rais huwa ameelemewa na mambo mengi.

Sikuishia hapo, nilitaka pia kujua kwa nini alikuwa hapendi kuzungumza chochote kama mzee mstaafu wakati CCM na serikali yake vilipokuwa vinapitia katika changamoto nyingi katika kipindi cha kati ya mwaka 2008-2014.

Jibu lake lilikuwa kwamba, silaha nzuri kwa kiongozi mstaafu duniani ni kukaa kimya maana upo mstari mwembamba sana kati ya kushauri na kutoa maoni kwa upande mmoja, na kukosoa na kuingilia uamuzi kwa upande mwingine.

Mazungumzo yetu yaliendelea pasipo kukoma na kwa kweli sikumpatia wasaa wa kupumzika.

Nikataka kujua iweje hakuwahi kumteua komredi Abdulrahman Kinana katika nafasi yoyote ya kiongozi ilihali alikuwa meneja wa kampeni zake za urais mara mbili.

Jibu lake lilikuwa alitamani kumteua, lakini kila mara Kinana alimkatalia.

Alifanya hivyo tena ilipofufuliwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kumuomba ampendekeze kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki jambo ambalo hatimaye alilikubali.

Tukaendelea, nikamuuliza, katika siku ya kwanza ya urais wake baada ya kuapishwa na kurejea Ikulu ni jambo gani la kwanza alilolifanya? Akaniambia, alimwandikia mtangulizi wake Rais Ali Hassan Mwinyi barua kwa mwandiko wa mkono wake bila kuichapa, akimshukuru sana kwa mchakato mzima wa kumpata Rais na kuahidi kuendelea kuomba ushauri wake katika kuendesha nchi.

Nilimdadisi juu ya mtazamo wake kwenye kinyang’anyiro cha urais 2015 kilichokuwa mbele yetu wakati huo. Katika hili, hakuwa tayari kufunguka. Pengine ni katika kuishi ile dhana ya kuwa ukistaafu unapaswa kujifunza kukaa kimya.

Hata hivyo, nilimchokoza kwa kumtajia majina ya wagombea mbalimbali waliokuwa wakitajwa tajwa wakati huo.

Nakumbuka vyema kwamba, nilimtajia majina 13. Wakati nikimtajia jina alikuwa anaitikia tu kwa kutikisa kichwa.

Yapo majina ya wagombea ambayo hakuwa akiamini kama kweli watagombea na wapo wale alioishia kutabasamu na wapo walioonekana kumsisimua.

Utulivu wa mzee Mkapa ulikuwa unafanya kutojua hisia zake, lakini unapogusa mahala anakopapenda uliweza ona hata mishipa ya utosi wake ikifurahi.

Nililiona hilo nilipolitaja jina la Dk. John Joseph Pombe Magufuli. Ni dhahiri Rais Mkapa alimpenda sana Dk. Magufuli. Haikuhitajika tochi kuona mapenzi yake kwake.

Alichozungumza siku hiyo kilibaki funzo na darasa kubwa kwangu.

Tulizungumza zaidi ya masuala ya siasa. Nilipenda pia kufahamu maisha yake nje ya siasa na uongozi.

Moja ya wasaidizi wa Mzee Mkapa wakati huo, marehemu Mkude ambaye alikuwepo usiku ule hakusita kueleza hisia zake kwangu.

Aliniambia kuwa mimi ni mwenye bahati kupata wasaa mrefu vile wa kuteta na Mzee.

Katika kuonyesha furaha yangu, nikamwambia kaka Mkude fursa ile itabaki kwenye kumbukumbu za maisha yangu kama Novemba Kuu (The Great November).

Nakumbuka pia kwamba, marehemu Mkude ndiye alinipiga picha na Mzee Mkapa usiku ule mtakata wa mwezi Novemba baada ya mazungumzo yetu yaliyoanza saa 10: 00 jioni na kumalizika majira ya saa 7:00 usiku.

Mbali na mazungumzo yetu, nimekuwa msomaji mzuri wa hotuba zote za Mzee Mkapa alizokuwa akitoa kila mwisho wa mwezi wakati akiwa madarakani na zile alizotoa katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Niliendelea kuwa mtoto na rafiki wa Mzee Mkapa hata nilipohamishiwa Wilaya ya Hai na baadae kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Mara kadhaa nilipata tena nafasi ya kuzungumza naye kwa kirefu, japo sikuwahi kupata wasaa kama ule wa saa 10 kule Turiani.

 Mzee Mkapa aliendelea kuwa rafiki yangu, mwalimu wangu na kila tulipoonana hatukuacha kuzungumza na kwa kweli nilijenga utamaduni wa kumdodosa na kujifunza mengi.

Leo Mzee Mkapa hayupo nasi. Niseme nini zaidi? Nimempoteza baba, rafiki na mtu aliyependa kuniona nikifanya vizuri kwenye kazi zangu na hasa akinisisitiza kuwasaidia wananchi wanyonge kutoka kwenye umaskini na kuwatatulia shida zao.

Hakika nchi imepoteza mzee mwenye maono, msimamo na mwana mageuzi wa kweli aliyeipenda nchi yake kwa dhati ya moyo wake.

Miaka 10 ya utawala wake alitufikisha mahala pazuri, alijenga taasisi ambazo zitaishi daima mioyoni mwa Watanzania, aliipenda imani ya kanisa lake na kuheshimu imani za watu wengine.

Natoa pole kwa Mama Anna, watoto wake na nampa pole Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kumpoteza kiongozi mashuhuri kwenye nchi na mlezi wake aliyemuamini na kumpa dhamana ya unaibu waziri akiwa na umri usiozidi miaka 40 kabla ya kumfanya waziri kamili.

Nampa pole mkuu wangu kikazi wa zamani, William Erio, Mkurugenzi wa NSSF ambaye kupitia yeye, Mzee Mkapa alinipenda na kuniamini.

 Nampa pole nyingi dada yangu Dk.Ellen Senkoro, Mtendaji Mkuu wa Mkapa Foundation ambaye wakati wote wa shughuli za Mzee Mkapa alipenda kunialika kwenye shughuli za mzee wangu huyu.

Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele Mzee Mkapa.

Hii dunia sisi ni wapitaji. Miaka yetu hakika ni ya kukopeshwa. Pumzika baba yangu, pumzika rafiki yangu, pumzika kiongozi wetu, Tutaonana kwenye ile asubuhi njema na iliyo kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles