26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

ANNE MAKINDA, DK. NAGU WASIMULIA YANAYOWAKUTA WANASIASA WANAWAKE

SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amesimulia masahibu aliyoyapata katika siasa na kusema kuwa akiyakumbuka huwa anatamani kulia usiku kucha.

Amesema safari ya mwanamke katika harakati za uongozi bado ni ndefu na kwa wale wanaotaka kuingia, ni lazima wapambane kwa kila mbinu na kuepuka kuonyesha udhaifu wao hadharani.

Makinda alisema hayo jana wakati wa mjadala wa Kongamano la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) uliokuwa ukijadili ‘mwanasiasa mwanamke na harakati za usawa wa kijinsia Afrika’.

“Sisi tumekuwa wabunge, ukikumbuka yaliyokupata unatamani ulie usiku maana ukilia mchana unaonekana una ‘weakness’ (upungufu).

“Tuliposimama mwaka 1995 baada ya kuingia kwa vyama vingi, niligombea ubunge, ilikuwa shughuli na baada ya hapo nilishtakiwa mahakamani kwa miaka minne watu wanapinga matokeo.

“Si rahisi wanawake kugombea, lakini kama wameamua lazima wapambane kwa kila mbinu na kuepuka kuonyesha udhaifu wao hadharani. Mtu akisema anataka kuwa mbunge ajiandae, si kusubiri zimebaki wiki mbili ama miezi mitatu halafu ndio aibuke na kusema anataka kuwa mbunge, kwa nini usishindwe?” alihoji.

Alisema pia kwa muda mrefu wanawake wamekuwa nyuma katika harakati za uongozi, huku wengine wakionekana hawafai.

“Hatuwezi kuendesha siasa kwa bahati nasibu, lazima tukae pamoja kimkakati na tuondoe fikra potofu kwamba mwanamke si kitu chochote, kuendelea kushangilia na kusindikiza hiyo si kazi yetu,” alisema.

 NAGU

Aidha, akichangia mjadala huo, Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu (CCM), alisema wanaume hawawezi kumaliza changamoto peke yao, hivyo aliwataka kukubali kushirikiana na wanawake.

“Wanaobeba umasikini wa Tanzania ni kina mama, hivyo tukubali kwamba wanawake lazima wawe sawa na wanaume. Mfumo dume ni pingamizi kwa mambo mengi.

“Nilipokuwa Waziri wa Utumishi, kama kuna nafasi za wakurugenzi ziko wazi, walikuwa wanaleta majina ya wanaume tu, wanasema hakuna wanawake wenye sifa,” alisema Dk. Nagu.

Pia alisema mwanamke akiamua anaweza na kutolea mfano kuwa yeye alianza kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, lakini sasa hivi anawakilisha jimbo.

“Mimi nilishindana na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, lakini nikashinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC). Kuna watu wanaoamini kwamba nimefanya makosa kushindana naye na hilo linatokana na mila na desturi, kwamba kwa vile ni mwanamke sina haki, ningemwachia yeye, hiyo haiwezekani.

“Kwani nani alizaa hao marais, aliyewalea na kuwakuza, si wanawake, kama wana akili wamezipata kwa kina mama, inawezekanaje huyu anayekuzaa ana uwezo mdogo na wewe uliyezaliwa uwe na uwezo mkubwa?” alihoji Dk. Nagu. 

ANNA ABDALLAH

Mbunge na Waziri mstaafu, Anna Abdallah, alisema katika ngazi za uamuzi wanawake wako wachache, lakini wakitumia vizuri nafasi zao watawainua wenzao.

“Unapokuwa katika chombo cha maamuzi usikubali kusikia maneno ya kudhalilisha wanawake wenzako, mimi nilikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa karibu miaka 20, wakati wa kupitisha majina mtu anasema mwanamke fulani hafai, ukiuliza sababu unajibiwa eti anapenda wanaume.

“Sikuona aibu, niliwauliza mwanamume gani hapendi mwanamke? Tukifika hapo wananyamaza kimya. Niliwaambia hiyo si sifa na tusipeane maneno ya kudhalilishana, tukikataa, kule kwenye vyombo vya maamuzi wanawake watapita,” alisema.

Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Ulingo wa Wanawake, alisema hivi sasa wamejikita kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila kujali itikadi zao za vyama.

“Tusiwarudishe nyuma wanawake wenzetu, kama uko juu washike mkono wenzako uwapandishe. Na sasa hivi sijali chama, akitoka Chadema nitampa nguvu na akishinda nampelekea salamu za pongezi kwa sababu ameshinda mwanamke,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, aliwataka wanawake walioko kwenye ngazi za uamuzi kuwatetea wenzao na kuacha woga.

“Kwa mambo yanayotuhusu wanawake lazima tuwe wamoja bila kujali itikadi za vyama. Hata kama kwenye chama chako wakisema upinge, ni bora na chama chenyewe uondoke.

“Hata nilipokuwa kiongozi na mwanachama mzuri wa CCM, kama kuna jambo zuri nilikuwa nahoji tunalikatalia nini.

“Akisema mtu wa chama kingine hata kama jambo zuri wao wanapinga, ule ni ujinga, kama jambo zuri linatoka kwa mpinzani wako liunge mkono, liendelezeni,” alisema.

 KAFANABO

Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia cha UDSM, Dk. Eugenia Kafanabo, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mjadala huo, alisema viongozi hao wamewafumbua macho kwani mambo mengi walikuwa hawayafahamu na kuahidi kuandaa kongamano jingine ili watu wengi waweze kuelimika zaidi.

“Watoa mada wamefungua vichwa vyetu na wametupa elimu ambayo wengi tulikuwa hatuna, tutakwenda kuwaelimisha na wengine,” alisema Dk. Kafanabo.

Kongamano hilo linatarajiwa kuhitimishwa leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles