26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

ANGLIKANA WAOMBA MSAADA WA SERIKALI KUMNG’OA MOKIWA

Na Patricia Kimelemeta


BARAZA la Walei wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam limeiomba Serikali kusaidia kumng’oa madarakani

aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Valentino Mokiwa.

Ombi hilo limetolewa jana na Katibu wa Walei wa dayosisi hiyo, Thomas Gambo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Gambo alisema wahudumu, mapadri, mashemasi na wainjilisti wa kanisa hilo hawatakiwi kumpa ushirikiano Mokiwa na Serikali inapaswa kuingilia kati kusaidia kumwondoa madarakani.

Mokiwa alivuliwa uongozi Januari 7, mwaka huu baada ya kutuhumiwa kuhujumu miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kanisa hilo, hatua ambayo aliipinga kwa maelezo haikufuata utaratibu.

Gambo alisema tayari wamekwisha mwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, wakimwomba asaidie kumwondoa madarakani Mokiwa na kwamba wanaiomba Serikali iingilie kati.


“Tayari tumewasilisha barua yetu kwa IGP ya kutomtambua Askofu Mokiwa kwenye nafasi hiyo kwa sababu alishavuliwa madaraka yake tangu Januari 7, mwaka huu, hivyo tunawataka viongozi wengine wasimpe ushirikiano”, alisema Gambo.

Aidha, Katibu huyo wa Walei alisema Mokiwa ametoa taarifa potofu dhidi ya Askofu Mkuu, Dk. Jacob Chimeledya.

Alisema uongozi wa kanisa unamtuhumu Mokiwa kwa madaraka yake kwa kuhodhi mali za kanisa zikiwamo nyumba ya Askofu Oysterbay huku nyingine zikiibiwa na kupotea.

“Mgogoro huu ulipoanza tuliwasilisha malalamiko yetu Halmashauri Kuu ya kanisa lakini hatukuridhishwa uamuzi ndio maana tukapeleka mashtaka uongozi wa jimbo kama Baraza la Rufaa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Katiba ya Kanisa la Anglikana Tanzania (KAT) Juni 8,2015.

“Katika mashtaka hayo tuliliomba pia baraza kumvua madaraka Mokiwa tangu mwaka 2015. Tunamuomba Mokiwa asiendelee kuvuruga kanisa na waumini wake, bali anapaswa kutii uamuzi uliofikiwa wa kuvuliwa madaraka kwa sababu ulizingatia taratibu na katiba ya kanisa letu," alisema Gambo.

Msemaji wa Askofu Mokiwa aliyejitambulisha kwa jina la Yohanna Sanga, alipoulizwa kuhusu jambo hilo alisema kuna kikundi cha watu wachache kinachowashawishi walei na waumini kumchafua bosi wake.

Alisema zipo taratibu zinazopaswa kufuatwa inapotokea kiongozi wa kanisa anatuhumiwa ambazo ni pamoja na kupeleka malalamiko Halmashauri ya Kudumu, Kikao cha Sinodi na Nyumba ya Maaskofu ambavyo ni vyombo vyenye mamlaka kutoa maamuzi ya kikanisa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles