24.6 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Anayoyafanya Samatta wachezaji wa Tanzania wanayaona?

Mbwana Samatta
Mbwana Samatta

NA BADI MCHOMOLO,

KILA kukicha Watanzania wanapenda kusikia habari za mchezaji wao wa kimataifa, Mbwana Samatta, ambaye anakipiga katika klabu ya Genk ya nchini Ubelgiji.

Huyu ni mchezaji pekee ambaye anaipeperusha vema bendera ya Taifa kutokana na jitihada zake za kutaka kucheza soka barani Ulaya.

Kujiamini kwake kumemfanya atimize ndoto zake, inawezekana kuwa bado hazijatimia lakini Watanzania wengi wanaamini ndoto zake zimetimia.

Kwa maelezo ya Samatta ni kwamba, ndoto zake aje kucheza soka la kimataifa hasa katika Ligi Kuu nchini England.

Dalili za kutimia kwa ndoto zake zinaanza kuonekana kwa kuwa mchezaji huyo hadi sasa anaonesha uwezo wa hali ya juu katika msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji, huku klabu yake ikishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo minne.

Katika michezo hiyo ambayo amecheza, nyota huyo anaongoza kwa ufungaji huku akiwa na mabao 3 katika michezo hiyo aliyocheza, wakati huo anapambana na wapinzani wake watatu ambao wote wana mabao matatu kila mmoja, nyota wa Mouscron ambaye anajulikana kwa jina la Filip Markovic, Jeremy Perbe wa Gent na David Pollet wa klabu ya Charleroi.

Samatta alivyoanza kuitumikia klabu ya Simba SC ya nchini Tanzania wala hakuwa na haraka kwa kuwa alikuwa anajua nini anakifanya akiwa uwanjani.

Katika michezo yake ambayo alicheza tangu asajiliwe na klabu hiyo alionesha uwezo wake mkubwa na kuwashawishi klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo kuweza kufanya naye mazungumzo kwa ajili ya kumsajili.

Hata baada ya Mazembe kumsajili mchezaji huyo pia alionesha uwezo wake wa hali ya juu huku akiwa na lengo la kutaka kusonga mbele katika ligi kubwa hasa barani Ulaya.

Hata hivyo, amefanikiwa kufanya hivyo japokuwa bado kuonekana katika ligi ya nchini England, lakini kuna uwezekano mkubwa wa msimu ujao kupata timu nchini humo kama ataendelea na kazi yake ya kujituma na kupachika mabao.

Lakini kwa wachezaji wengine wa hapa nchini akili zao ni kuja kucheza soka katika klabu ya Simba, Yanga na Azam FC, lakini si wengi ambao wanafikiria kuja kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kama ilivyo kwa Samatta.

Ninaamini kama wapo wachezaji wengi ambao wana mawazo kama Samatta, basi soka letu lingebadilika na lingekuwa na ushindani wa hali ya juu kwa kuwa wangeonesha uwezo mkubwa hasa pale wanapokutaka na timu nyingine za mataifa mbalimbali.

Ninatamani kuona siku moja kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ akiita kikosi chake huku wachezaji mbalimbali wakiwa wanatoka katika klabu kubwa barani Ulaya na sehemu nyingine na kuungana pamoja kwa ajili ya kuja kulisaidia taifa lao.

Lakini wachezaji hawa ambao wanacheza Ligi Kuu nchini Tanzania wakiendelea kufikiria kucheza soka katika klabu ya Simba, Yanga na Azam, basi tutashindwa kufanya vizuri kimataifa kama watashindwa kujituma na kupata nafasi ya kucheza soka nje na kupata changamoto mpya. Ni vizuri wachezaji wetu wakawa na wivu kwa mafanikio ya Samatta na wawe na lengo la kwenda kucheza soka nje, inawezekana kama watakuwa tayari na kujitoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles