31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Anayetuhumiwa kumteka Mo ahoji kwanini anasota gerezani peke yake

 KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

DEREVA teksi Mousa Twaleb anayedaiwa kushiriki kumteka Mohammed Dewji (Mo) amehoji alimtekaje mfanyabiashara huyo, alitakatishaje fedha na kwanini anasota gerezani peke yake.

Mshtakiwa huyo aliwasilisha hoja hizo jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na jalada liko kwa DPP kwa hatua za usomaji kwa ajili ya kutoa maelekezo.

“Kila siku wanasema upelelezi umekamilika na mimi niko ndani, wanadai nimemteka Mo, kama kumteka mbona niko ndani mwenyewe? Nadaiwa kutakatisha na kumteka inakuwaje?” alihoji mshtakiwa huyo.

Hakimu Shaidi alisema hilo hawezi kulijibu, ajibu Wakili Nguka namna gani ulimteka na kutakatisha.

Nguka akijibu alidai kujua alitakatisha vipi iko ndani ya jalada.

Hakimu alishauri mshtakiwa aandike barua kwa DPP kulalamikia shauri lake.

Alisema kila siku wanasema kuna watuhumiwa wengine hawajakamatwa, yeye ndiye yuko ndani.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 8, kwa kutajwa.

Awali upande wa Jamhuri ulidai wanaendelea kuwatafuta washtakiwa wengine ili waunganishwe katika kesi hiyo.

Watuhumiwa wengine wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara huyo ambao upande wa mashtaka unawatafuta, ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini.

Washtakiwa hao ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018, katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwa makusudi washtakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia inadaiwa Oktoba 11, 2018 maeneo ya Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Pia inadaiwa Julai 10, 2018 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mo alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles