29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Anayempikia Trump hula mayai 24 asubuhi, kuku wanne mchana

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

ANAITWA Andre Rush, umri wake ni miaka 45. Ni wananchi wachache wa Marekani wasiomfahamu huyu jamaa.

Licha ya umaarufu alionao, majukumu yake ya kazi huishia jikoni tu. Hicho ndicho kilichomweka ndani ya Ikulu ya Marekani, kuhakikisha milo mitatu inapatikana, tena kwa wakati, kwa kila mfanyakazi.

Ni tofauti na wafanyakazi wengine wa Ikulu ya nchi hiyo, ambao aghalabu utawaona katika kila msafara wa Rais Donald Trump.

Rush ataonekana hadharani siku za sherehe na hafla zingine, jukumu lake kubwa likiwa ni kuandaa keki au msosi ‘uliokwenda shule’ kwa maofisa na wageni waliohudhuria.

Katika siku za kawaida, utamkuta jikoni, akihusika kwa kila hatua ya chakula anachokula Rais Trump na watu wengine ndani ya Ikulu.

Hiyo inamaanisha ana ratiba ya chakula ya kila siku, anatakiwa kusimamia ubora wa mlo wenyewe, kwa maana ya usalama wa kiafya na zaidi ya hapo, aingie jikoni kuanza kukarangiza.

Jamaa amekuwa akiifanya kazi hiyo ya kuwapikia wakubwa Ikulu ya Marekani tangu mwaka 1997, ikimaanisha kuwa si Rais Trump pekee, bali amewahudumia viongozi wote waliopita, wakiwamo George W. Bush na kipenzi cha Waafrika, Barack Obama.

Wasifu wa Rush unamtaja kuwa ni sajenti mstaafu na alilitumikia Jeshi la Marekani kwa miaka 24, kabla ya kugeukia shughuli ya kuandaa madikodiko.

Kwa mara ya kwanza, baada ya kustaafu utumishi wake jeshini, Rush alijitosa katika upishi mwaka 1994 na moja kati ya matukio yaliyompa jina ni lile la kutengeneza keki yenye urefu wa futi 16.

Lakini pia, baba huyo wa watoto wanne amejijengea umaarufu mkubwa kutokana na mwonekano wake wa kuvutia unaotokana na mazoezi ya kutanua misuli.

Hata umaarufu wake uliongezeka mara dufu Juni, mwaka jana, baada ya mkono wake uliojengeka kimazoezi kuonekana na kuwavutia wengi. Siku hiyo alikuwa katika majukumu yake ya upishi.

Akilizungumzia hilo la mwili wake mkubwa unaoweza kuufananisha na waigizaji wa filamu za mapigano kama Arnold Schwarzenegger, anasema:

“Kuna kipindi Rais Bush alinipongeza kwa jinsi nilivyo fiti na aliniuliza huwa nafanya nini kuwa hivi. Hata Rais Obama na viongozi wengine wakubwa wamekuwa wakiniuliza. Ninachowaambia ni kujitoa kwa kwenda mazoezini (gym). Hakuna zaidi ya hapo.

“Huwa napiga ‘pushapu’ 2,222 kila siku na nilianza kufanya hivyo ikiwa ni kampeni ya kuwakumbuka maveterani wa kijeshi 22 wanaopoteza maisha kila siku kwa kujiua,” anasema.

Katika mahojiano yake na jarida la afya la men’s health, Rush anasema katika idadi hiyo, huwa anapumzika dakika tatu tu, zikizidi sana 10, kila anapofikisha 200.

Aidha, haishii katika pushapu, bali ili kujiweka fiti zaidi, amekuwa akihudhuria mara kwa mara vituo vya mazoezi (gym).

“Huwa nakwenda gym kila siku na huko natumia saa moja au mbili hivi,” anasimulia Rush na kuongeza: “Kutokana na mazoezi makali hayo, huwa nakula chakula kingi.”

Akiliambia jerida hilo la men’s health nasema asubuhi pekee huwa inakaa poa endapo anapata mayai ya kuchemsha 12 au 24 na maziwa.

Si kwamba mchana utapita hivi hivi, lazima msomi huyo wa shahada ya uongozi wa biashara apate kuku wanne wa kukaanga ili mambo yaende sawa katika majukumu yake ya kazi za jikoni, huku akisubiri chakula cha usiku, ambacho huenda akarudia kama mchana au akabadilisha.

Mbali ya majukumu yake, Rush amekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kuwasaidia maveterani wa jeshi, ambao kwa Marekani wamekuwa wakiripotiwa kukabiliwa na msongo wa mawazo unaosababisha wajiue.

Hivyo basi, alichoamua kukifanya mpishi huyo ni kuandika kitabu cha vyakula kiitwacho ‘Combat Food Medic’, akitazamia kutoa elimu ya milo inayoweza kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo.

“Kupika kulikuwa na msaada mkubwa kwangu katika tiba (dhidi ya msongo wa mawazo),” anasema Rush kuliambia jarida la Men’s Health.

Kuhusu familia yake anasema: “Watoto wangu nao wako fiti pia… Nawafundisha namna ya kupika vyakula vyenye afya…”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles