AMUUA MDOGO WAKE KWA MPINI WA JEMBE

0
1167

Na Gurian Adolf-Sumbawanga

JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Kilida Kona wilayani Sumbawanga, Japhet Kigula kwa tuhuma za kumuua mdogo wake kwa kumpiga na mpini wa jembe kichwani wakati akimuadhibu.

Akithibitisha tukio hilo jana mjini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema tukio hilo lilitokea Juni 26, mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji hicho, ambapo alimtaja marehemu  kwa jina la Makumbi Kigula.

“Taarifa zinaeleza kuwa siku mbili kabla ya tukio mtuhumiwa ambaye alikuwa amesafiri kutoka mkoani Mwanza alimwita mdogo wake nyumbani kwake ili waweze kufanya mazungumzo ambayo hayakuwekwa bayana lakini kijana huyo hakuweza kwenda hali ambayo ilimkera Japhet.

“Hatua hiyo ilionekana kutomfurahisha mtuhumiwa ambapo alihoji hatua ya mdogo wake kuchelewa wito. Kutokana na hali hiyo, Japhet akisaidiwa na mmoja wa watumishi wake wa ndani walimkamata kijana huyo na kumfunga kamba mikono na miguu kisha kuanza kumwadhibu kwa kutumia mpini wa jembe katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kuvuja damu nyingi kichwani na puani,” alisema.

Kitendo hicho kiliwafanya majirani kuingilia kati na kuamua kumkimbiza marehemu katika Zahanati ya kijiji na ilipofika juzi mchana alifariki dunia.

Baada ya tukio hilo polisi walifika kijijini hapo na kumtia mbaroni mtuhumiwa ambaye bado wanaendelea na mahojiano na pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Katika tukio jingine, Polisi inamshikilia dereva Josephat Salya mkazi wa Sumbawanga mjini kwa tuhuma za kumgonga kwa gari mtoto Eliud Steven(5) mkazi wa Kijiji cha Kipundu Tarafa ya Namanyere wilayani Nkasi.

Tukio la kumgonga mtoto huyo lilitokea juzi saa 10:05 jioni katika kijiji hicho wakati mtoto huyo akiwa anatembea barabarani.

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando alisema kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha  gari lenye namba za usajili T 790 DEM T aina ya Tata Truck mali ya Assif Ashraf ambapo lilimgonga mtoto huyo na kufariki dunia papo hapo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here