24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Amri ya DC kukata mishahara watumishi kulipa ultrasound iliyoibwa yatenguliwa

Derick Milton – Simiyu

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, ametengua agizo la Mkuu wa Wilaya (DC) ya Bariadi, Festo Kiswaga, aliyeagiza watumishi 137 wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi ya Somanda kukatwa mshahara ili kununua mashine ya ultrasound iliyoibwa hospitalini hapo.

Katika kikao chake cha juzi na watumishi wa hospitali hiyo, Kiswaga alitoa siku saba watumishi wote kuchanga kulingana na mishahara yao na fedha zitakazopatikana zinunue mashine hiyo iliyoibwa Agosti 5, mwaka huu katika wodi ya wajawazito.

Ikiwa ni ndani ya saa 24 tangu agizo hilo kutolewa, jana Sagini naye alikutana na watumishi wa hospitali hiyo na kusema haiwezekani watumishi wote wahusike na wizi huo.

Alisema Serikali ina vyombo vya ulinzi na vina wafanyakazi wanaolipwa mishahara kwa kazi ya kuchunguza, hivyo ametaka suala hilo liachiwe vyombo hivyo vifanye kazi yake na kumpata mhusika wa wizi wa kifaa hicho.

Sagini alisema uamuzi wa Kiswaga unawaonea baadhi ya watumishi ambao walikuwa likizo, hawakuwepo kazini, wagonjwa au walikuwa na ruhusa.

Alisema yeye akiwa ndiye mkuu wa watumishi Mkoa wa Simiyu, alishtushwa na uamuzi wa Kiswaga na asingeweza kunyamaza ilihali kuna wataalamu ambao kazi yao ni kufanya uchunguzi kwa matukio kama hayo.

“Tulishtuka kidogo na uamuzi wa DC, lakini tuliona alikuwa sahihi kutokana na nyie kushindwa kutoa ushirikiano ili mashine hii irudishwe, wengine mkaamua kwenda kulalamika kwenye vyama vyenu vya wafanyakazi, ila hata mimi kama mkuu wa watumishi nisingelinyamaza.

“Uamuzi wa DC ukifanyika utakuwa unaingilia majukumu ya vyombo vya kiuchunguzi na wote wapo hapa, hawajashindwa kufanya hii kazi na kumpata mhusika, sasa hakuna mtu yeyote atakayechangishwa ila vyombo vifanye kazi yake,” alisema Sagini.

Aliwataka watumishi hao kuacha tabia ya wizi wa mali za umma, ambao alieleza umekuwa ukijitokeza mara kwa mara. Mwaka 2016 iliibwa darubini (Microscope) ambayo baadaye ilipatikana.

Aliwataka watumishi kulisaidia Jeshi la Polisi katika kuhakikisha mhusika anapatikana na anachukuliwa hatua, ikiwa pamoja na kuwataka kurejesha kifaa hicho kama ambavyo walifanya kwenye darubini mwaka 2016.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Mkoa wa Simiyu, Catherine Dickson, alimshukuru Sagini kwa uamuzi wake huo.

“Kilichokuwa kimeamriwa awali kimsingi kipo kinyume na utaratibu kisheria, sawa hatukubaliani na ultrasound kuibwa, lakini DC alikuwa ameenda mbali sana kutokana pengine na uchungu aliokuwa nao.

“Lakini tunashukuru uongozi wa mkoa kwa sababu unatambua sheria, kanuni na taratibu na umetoa tamko na tumefarijika sana kama chama cha wafanyakazi,” alisema Catherine.

Mara baada ya kikao hicho, baadhi ya wafanyakazi walimshukuru katibu tawala na uongozi wa mkoa kwa hatua hiyo.

Walieleza kuwa uamuzi wa DC uliwaweka njia panda na kuingiwa na hofu kubwa kutokana na wengine kutokuwa na uwezo wa kuchangia.

“Tunashukuru kwa msamaha uliotolewa, tangu jana nimelala vibaya, ‘pressure’ ipo juu, hadi sasa kichwa kinaniuma.

“Mimi uwezo wangu ni mdogo, kwanza kifaa chenyewe tunachoambiwa wote tulipe sikijui, yaani naongea kwa uchungu hadi nasikia kulia kwa furaha niliyonayo baada ya tamko hili,” alisema Frola Paskazia.

Agosti 5, mwaka huu, mchana, mashine hiyo inadaiwa kuibwa ikiwa katika wodi mpya ya wajawazito hospitalini hapo.

Juzi Kiswaga alitoa siku saba kwa watumishi wote wa hospitali hiyo kuchanga na kuhakikisha wananunua mashine hiyo ambayo inagharimu zaidi ya Sh milioni 30.

Kiswaga alisema yuko tayari kufukuzwa kazi kwa hatua yoyote ambayo atachukua kwa watumishi hao, ikiwa watashindwa kuhakikisha wanarudisha mashine hiyo kupitia michango yao ndani ya muda ambao ametoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles