23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Amref yatoa baiskeli 710 mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini

NA DERICK MILTON, DAR ES SALAAM.

Licha ya jitihada za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu nchini, bado kuna kiwango kikubwa cha wananchi wenye maambukizi ya ugonjwa huo ambao hawajajitokeza au kuibuliwa hasa maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa uibuliwaji wa wagonjwa wenye kifua kikuu kwa mwaka 2020 ni asilimia 26, ambapo lengo ni kufikia asilimia 47 mwaka 2023.

Kupitia mradi wake wa USAID Afya Shirikishi unaotekelezwa kwa muda wa miaka mitano (2021-2025) katika mikoa nane ikiwemo Zanzibar, Shirika la Amref Health Africa Tanzania, limetoa baiskeli 710 katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mbali na baiskeli Amref imekabidhi vifaa ambavyo ni vikasha 859 ambavyo vitatumika kubebea sampuli za kufanyiwa vipimo vya kifua kikuu, vifaa mbavyo vimetolewa leo Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa miradi Amref, Dk Godson Zacharia, amesema  Pamoja na kifua kikuu, mradi huo umelenga kuimarisha matumizi bora ya uzazi wa mpango kwa jamii katika mikoa husika.

Dk Zacharia amesema  mikoa ambayo mradi huo utatekelezwa ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Katavi, Kigoma, Mwanza, Geita, Songwe na Zanzibar.

“Jumla ya watoa huduma ngazi ya jamii 735 wamepewa mafunzo mbalimbali ikiwemo kubaini wagonjwa, jinsi ya kujikinga pamoja na kutoa elimu na tumewapatia baiskeli hizi kama moja ya vitendea kazi kuweza kuwafikia walengwa kwa wakati.

“Lakini mradi huo utawahusisha madereva pikipiki 400 ambao wao watahusika kusafirisha sampuli za makohozi na kuzipeleka kwenye vituo vikubwa vya kutolea huduma za Afya kwa ajili ya vipimo kutoka maeneo ya vijijini ambako hakuna huduma za Afya,” amesema Dk. Zacharia.

Amesema kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza maambukizi na kuendelea kwa kifua kikuu , kupitia uimarishaji wa utoaji huduma katika ngazi ya jamii kuimarisha upatikanaji na matumizi ya huduma bora za uzazi wa mpango.

“ Pia mradi umelenga kuimarisha uwazi, utoaji mrejesho, na upatikanaji wa takwimu zinazo husiana na programu za kuimarisha sera na miongozo ya taifa ya kifua kikuu na kuongeza uongozi na uungaji mkono wa kisiasa katika vita dhidi ya ugonjwa huo kama kipaumbele cha jamii,” ameongeza Dk Zacharia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Amref Dk. Florence Temu, amesema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani(USAID) ambapo wanaamini kupitia kwa watoa huduma idadi ya kubwa ya wagonjwa itaibuliwa.

Amesema kuwa watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa watu muhimu katika kuboresha huduma za Afya ikiwa watawezeshwa vitendea kazi, ambapo ameeleza lengo ni kuhakikisha wanaisadia serikali kufikia malengo yake ya mwaka 2023.

“ Ni matumaini yetu kuwa vifaa hivi vitakwenda kufanya kazi ambayo imekusudiwa, watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa watu muhimu sana kwani ndiyo wanajua na wananchi kwa kiasi kikubwa, tuna imani kuwa tunaenda kuisaidia serikali kufikia lengo lake,” amesema Dk. Temu.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM) Dk. Grace Magembe, amewataka waganga wakuu wa mikoa ambayo mradi unatekelezwa kuhakikisha wanasimamia vifaa hivyo.

Amesema kuwa haitakuwa jambo jema kusikia baiskeli hiyo zinafanya kazi nyingine tofauti na ile iliyokusudiwa, huku akizitaka halmashuari zinazohusika kusaidia katika utangenezaji wa vifaa hivyo pindi vitakapoaribika.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani(USAID), Ananthy Thambinayagam, amesema kuwa wamelenga kufikia mwaka 2023 kiwango cha asilimia 46 cha watu walioibuliwa  kiwe kimefikiwa.

Amesema kuwa Shirika hilo kupitia programu mbalimbali limeendelea kuisaida Tanzania katika nyanja cha uchumi, siasa pamoja na kijamii ili kuweza kuwa na jamii yenye afya bora.

Tabu Juma kutoka jijini Dar es Salaam akiongea kwa niaba ya watoa huduma ameishukuru Amref kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na wakati kama ilivyopangwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles