Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya madini ya Petra Diamonds imegundua aina adimu ya almasi ya rangi ya pinki yenye uzito wa karati 23.16 kutoka mgodi wake wa Williamson uliopo Mwadui, Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo ya madini, almasi hiyo ya pinki, moja ya madini ya rangi yanayosakwa zaidi duniani ni mfano wa ubora wa hali ya juu na ugunduzi mkubwa na muhimu zaidi kufanywa na Petra kutoka mgodi huo hadi sasa.
“Almasi za pinki hupatikana katika migodi michache duniani na uadimu wake huzifanya kuwa moja ya madini yenye rangi yanayotafutwa zaidi duniani,”taarifa ya kampuni hiyo ilisema.
Rangi ya pinki katika almasi inadhaniwa kuletwa kutokana na mabadiliko ya muundo wa molekuli, ambao unaaminika kusababishwa na aina fulani ya mtikisiko wa ardhi (seismic shock) unaotokea wakati wa kipindi cha uumbaji wa almasi.
Pande hilo la almasi litauzwa katika mnada huko Antwerp nchini Ubelgiji Desemba mwaka huu.
Jiwe hilo jipya linasemekana kuwa na ubora zaidi kuliko almasi pinki yenye ubora wa juu na uzito wa karati 16.4 iliyogunduliwa katika mgodi huo Septamba 2014, ambayo iliuzwa kwa dola milioni 2.2 sawa na Tsh bilioni 4.7.
Novemba 10 mwaka huu, mteja mmoja wa China, ambaye hakuweza kutambulika alinunua almasi ya pinki yenye umbo la mto na uzito wa karati 16.08 katika mnada huo kwa bei iliyovunja rekodi ya dunia. Aliinunua kwa Pauni milioni 19 za Uingereza sawa na Sh bilioni 61 za Tanzania kama zawadi kwa binti yake.
Katika miaka karibu 250 ya historia ya minada, ni almasi tatu tu safi za pinki zilizokuwa na uzito wa zaidi ya karati 10 zilizoonekana kwa mauzo, kwa mujibu wa taasisi ya Christie’s.