32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYOYASHUHUDIA PROFESA MBARAWA MSCL YAFANYIWE KAZI

Na BENJAMIN MASESE – MWANZA


profesa-makame-mbarawaHIVI karibuni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alikutana na watumishi wote wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) huko mkoani Mwanza ili kujua hali ya biashara ya meli kwa Kanda ya Ziwa.

Akiwa huko alipata taarifa kwamba moja ya meli inayofanya kazi inatengeneza faida ya Sh 100,000 kwa safari moja huku gharama inayotumika ni Sh milioni 3.7.

Taarifa hiyo ilionekana kumchefua Profesa Mbarawa na kuanza kuwahoji wakuu wa idara na kubaini maelezo yao yanatia shaka. Akatangaza kwamba atafanya mabadiliko ya haraka kwa kuwaondoa watumishi watatu katika nafasi zao ili kutafuta wengine wenye weledi kuifufua MSCL.

Mbarawa aliwatilia shaka baadhi ya watumishi, hususani wakuu wa idara na kutaka kumweleza wanaishi maisha gani ikiwa watumishi wengine hawajapata mishahara yao kwa kipindi cha miezi 11 sasa.

Profesa Mbarawa alipata shaka juu ya ufisadi MSCL baada ya kuuliza ndani ya akaunti yao kuna kiasi gani cha fedha, ndipo alipoelezwa kwamba kuna Sh 600,000 pekee ingawa kwa sasa kiwango kimepanda hadi Sh milioni 16 baada ya kuletwa Kaimu Meneja, Erick Hamiss aliyetoka Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB).

Hakika kila kilichohojiwa na Profesa Mbarawa na kujibiwa na wakuu wa idara, majibu yao yalionekana wazi kumuumiza kichwa, hasa waliposema zaidi ya meli nne hazifanyi kazi na zinahitaji fedha kwa matengenezo.

Waziri huyo alihitimisha kwamba muhimu ni kuwaondoa watumishi wazembe na kutafuta vijana TIB ili kupelekwa MSCL kufufua kampuni hiyo kama ilivyofanywa  kwa Shirika la Reli (TRL).

Katika kuweka mambo sawa, Mbarawa alitoa Sh milioni 100 ili kukabarati meli nne zilizokuwa zimekufa ambazo ni Mv Clarious, Mv Serengeti, Mv Sangara na Mv Ukerewe zinazohitaji ukarabati wa injini, mifumo ya umeme na ufundi na gia boksi.

Lakini Mbarawa aliwatahadharisha watumishi wachache wanaofuja fedha katika kampuni hiyo na wazembe wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kukaa tayari kuchukuliwa hatua za kisheria kwani hivi sasa Serikali haitamvumilia yeyote anayekiuka maadili ya kazi.

Hata hivyo, ilibainika kwamba MSCL haina wataalamu wazuri na wenye weledi, taaluma na ujuzi.

Nahitimisha kwa kumweleza Profesa Mbarawa kwamba alichokishuhudia MSCL  kinapaswa kufanyiwa kazi haraka kwani hadi sasa Kaimu Meneja Hamiss ni kama amewekwa kwenye zizi lililojaa wanyama wakali.

Sote tunajua ujio wa kiongozi huyo umefanikiwa kuziba mianya ya rushwa na ndiyo maana fedha kwenye akaunti zilipanda ghafla kutoka Sh 600,000 hadi milioni 16 ndani ya wiki mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles