25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyezusha kifo cha Mkuu wa Majeshi kortini

yeye na wengine (1)*Ni mwanafunzi wa DIT, anyimwa dhamana

 

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MWANAFUNZI wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), Benedict Ngonyani, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusambaza taarifa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Davis Mwamunyange, amelishwa sumu.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza taarifa hizo za uongo kupitia mtandao wa Facebook, huku akidai Mwamunyange baada ya kulishwa sumu alipelekwa Nairobi kwa matibabu.

Ngonyani, ambaye ni mkazi wa Magomeni Mapipa, Dar es Salaam, ni mwananchi wa kwanza kufikishwa mahakamani tangu kuanza kutumika kwa Sheria mpya ya Mtandao.

Mwanafunzi huyo alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa na Jackline Nyantori na Anastazia Wilson, walimsomea mshtakiwa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage.

Kimaro alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo, Septemba 25, mwaka huu, Dar es Salaam, ambapo alisambaza taarifa kupitia mtandao wa Facebook, kwamba Jenerali Mwamunyange amelishwa sumu.

Wakili huyo alidai mshtakiwa huyo alifanya hivyo wakati akijua kwamba taarifa hizo ni za uongo na zililenga kupotosha umma.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo, ambapo Kimaro alidai Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa mamlaka aliyonayo amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa mshtakiwa kwa sababu kuna mambo ya taifa anayoyashughulikia.

Hakimu Mwijage alisema mahakama inakubaliana na hati hiyo, hivyo mshtakiwa atakwenda rumande na dhamana yake itatolewa pale DPP atakapoondoa hati yake.

Kimaro alidai upelelezi unaendelea na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa Serikali Mkuu wa TCRA, Kalungura, alitoa onyo kwa vijana wanaotumia mitandao akiwaasa kuitumia vizuri na si kutoa taarifa za uongo.

Alidai mtuhumiwa huyo alitoa taarifa kwamba Jenerali Mwamunyange amelishwa sumu yuko Nairobi, nchini Kenya kwa matibabu, huku akijua si kweli.

Alitoa wito kwa vijana ambao wengi wapo katika mitandao waitumie vizuri kwa kuwa ukituma matusi, taarifa za uongo ambazo hazijathibitishwa utakamatwa.

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela, alisema mtuhumiwa huyo ndio kafungua sheria hiyo mpya ya mtandao, hivyo anawaonya vijana kuacha kufanya mambo hayo katika mitandao.

“Mtuhumiwa hajatumwa na mtu, wala hakuna mamlaka husika iliyomwelekeza kufanya hivyo. Natoa onyo kwa vijana kuacha kutumia mitandao vibaya,” alisema.

Wakati huo huo, wafanyabiashara watano, raia wa kigeni, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 880 kwa  kuingiza vifaa vya mawasiliano nchini na kutoa huduma ya mawasiliano bila kuwa na leseni.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na TCRA, wakikabiliwa na kesi tatu tofauti za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao wote walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage, ni Ally Hamze (53), raia wa Afrika Kusini, Huang Bing (26).

Wengine ni Hafeez Irfan (32), Mirza Baig (41) na Irfan Baig (46), wote raia wa Pakistan na wakazi wa Dar es Salaam.

Jopo la Mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hellen Moshi, Wakili wa Serikali Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura na Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori, waliwasomea washitakiwa hao mshitaka yanayowakabili.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka kula njama, kuingiza nchini vifaa vya mawasiliano bila leseni, kuvisimika, kuendesha huduma za mawasiliano bila kibali kutoka TCRA, kuendesha huduma hizo na kukwepa malipo na kuisababishia serikali na mamlaka hiyo hasara ya Sh 883,953,000.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti hadi Septemba, mwaka huu, Dar es Salaam.

Hata hivyo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hizo haujakamilika, hivyo kuomba kuahirishwa hadi tarehe nyingine.

Hakimu aliahirisha kesi hizo hadi Oktoba 23, mwaka huu na washitakiwa wote walirudishwa rumande hadi tarehe hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles