KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu imemtia hatiani na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa, Esther Lymo (47) baada ya kujiridhisha kwamba alimuua mtoto wa dada yake, Naomi John (7) kwa kukusudia.
Hukumu hiyo ilisomwa jana Mahakama Kuu iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Msajili, Pamela Mazengo.
“Mahakama inakubaliana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, umethibitisha kwamba mshtakiwa ulitenda tendo hilo na mauaji ya kukusudia.
“Hakuna ubishi kwamba mshtakiwa ulikuwa eneo la tukio, mahakama imeangalia mwenendo wa mshtakiwa, ni kweli kwamba mshtakiwa ndiye alimpiga marehemu, kitendo cha kuhangaika kupika uji kinaonyesha uliona kuna tatizo.
” Katika ushahidi wa utetezi kuna mambo mengine yanaunga mkono ushahidi wa Jamhuri,”alisema Hakimu .
Kabla ya kupewa adhabu hiyo mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu sababu ni mkosaji wa mara ya kwanza na ni mama anayetegemewa huku upande wa Jamhuri wakiomba apewe adhabu kali.
Katika majumuisho wazee wa baraza kwa nyakati tofauti walitoa maoni yao kwamba kutokana na ushahidi wa mtoto wa miaka tisa ambaye alishuhudia tukio la kupigwa kwa marehemu Naomi John, inaonesha wazi mshtakiwa alikusudia kufanya mauaji.
Walidai watoto walikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kusoma lakini malengo hayo hayakutekelezeka kwa sababu watoto, Naomi na Andrew hawakupelekwa shule matokeo yake walikutana na huo ukatili wa kuteswa na mshtakiwa.
“Kulingana na ripoti ya daktari kuonyesha marehemu alikutwa na majeraha mwilini na mshtakiwa kukiri alimchapa marehemu kwa fimbo ya mpera, hili linaonesha aliua kwa kukusudia,” walidai wazee hao katika maoni yao.
Katika ushahidi wa upande wa mashtaka mshtakiwa anadaiwa kumpiga marehemu, kumng’ata mwilini na kumwagia maji ya moto ya chai.
Mshtakiwa anadaiwa ilikuwa tabia yake kuwafanyia ukatili watoto hao Andrew na marehemu Naomi.
Mtoto katika ushahidi alidai walikuwa wanaishi pamoja na Junior, dada Sia na Naomi John ambaye amfahamu walikuwa wanakaa naye pale, lakini alikufa akazikwa.
Alidai Naomi alipigwa sababu alimwaga maji yakasambaa nyumba nzima akaambiwa ayafute, alianza kuyafuta, alipofika sehemu akagoma kuendelea kufuta ndipo mama yao mdogo akaanza kumpiga na fimbo ya mpera.
Alidai Mamdogo alimng’ata mgongoni akamnyanyua juu kisha akamwachia, akamweka katika maji akamtoa na kumweka barazani, akamwagia chai ya moto.
“Naomi alipoachiwa alianguka chini, alikuwa kachoka, akamchukua akampeleka ndani, alimpeleka bafuni akamtoa akaenda kumlaza kitandani, akamwashia feni, Naomi alikuwa kachoka sana.
“Aliniita mamdogo akanituma dukani nikanunue unga wa kumkologea uji, niliporudi dukani nilimkuta Naomi anatoka povu puani.
“Mama alienda kununua dawa, aliporudi alimkuta Naomi kafariki,”alidai.
Anadai alijua kafariki sababu aliwaona dada zao wanalia, wakamchukua Naomi wakampeleka hospitali huku yeye akiwa kaachwa nyumbani.
Alidai Naomi hakuwa anakosa mara zote, isipokuwa mama yao mdogo alikuwa akimpiga hata yeye na ubapa wa panga fupi na kumfinya kwa kutumia kucha na kisu cha kukatia ugali.
Shahidi huyo alionesha mahakama kovu katika mkono wake lililotokana na kupigwa na ubapa wa panga. Tukio hilo likitokea mwaka 2016 maeneo ya Tuangoma Kigamboni, Dar es Salaam.