23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyetaka kupindua Ikulu afikishwa mahakamani

picha-ya-ikuluNA Kulwa Mzee

-Dar es Salaam

SERIKALI imemfikisha mahakamani mfanyabiashara Leonard Kamili maarufu Materu (31) kwa tuhuma za kutishia kuipindua Ikulu kwa maneno.

Mshtakiwa huyo anayedaiwa kutoa maneno hayo kwa nia ya kumtisha Rais Dk. John Magufuli alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Margareth Bankika.

Mshtakiwa huyo ni mkazi wa Moshi Baa kwa Diwani, jijini Dar es Salaam, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo.

Wakili Lukondo, alidai kuwa mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Akisoma mashtaka hayo Lukondo alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, Julai 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika jijini Dar es Salaam.

Wakili huyo alidai mshtakiwa huyo siku hiyo huku akijua alichapisha taarifa  na kuiweka katika mtandao huo ikiwa na maneno ya uongo yasemayo: “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu” alisema.

Inadaiwa ujumbe huo ulikuwa na nia ya kumtishia Rais Dk. John Magufuli.

Mshtakiwa akiwakilishwa na Wakili Neema Lamwai, alikana kutenda kosa hilo, ambapo Wakili wa Serikali Diana alidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hakimu Margareth alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa ambayo yalimtaka awe na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.

Mshtakiwa huyo alitimiza masharti ya dhamana, hivyo ameachiwa kwa dhamana hadi Septemba 20, mwaka huu, kesi itakapokuja kwa kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles