FARAJA MASINDE
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza orodha ya washindi wa tuzo ya kimataifa ya utafiti wa sayansi ya maisha, kwa ajili ya mashirika au watu waliotoa mchango muhimu katika kuboresha ubora wa maisha ya watu duniani.
Watu waliofanikiwa kuwamo kwenye orodha hiyo ya mwaka 2019 ni watatu tu, wanaotoka mataifa tofauti akiwamo Tu Youyou, raia wa China, aliyegundua dawa ya Artemisinin, na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani kote.
Takwimu zinaonesha kuwa dawa ya Artemisinin imepunguza kiwango cha vifo vinavyotokana na malaria kwa asilimia 66 na kiwango hicho kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa asilimia 71 barani Afrika.
Oktoba mwaka huu, Unesco ilitangaza washindi watatu ambao ni kutoka mataifa ya China, Marekani na Ireland, waliofanya utafiti wa kisayansi ambao umekuwa na matokeo chanya kwa jamii. Tuzo hiyo ya kimataifa ilizotangazwa mjini Equatorial Guinnea baraniAfrika, ikiwa ni ya 50 sasa kutolewa na Unesco, ikilenga wagunduzi wa sayansi waliotumia sehemu kubwa ya maisha yao kufanya tafiti zilizosaidia kuleta tija kwa jamii, ikiwamo usawa kwenye maisha ya binadamu.
Mbali na Profesa Tu Youyou wa China, aliyenyakua tuzo hiyo, wengine ni Daktari kutoka nchini Marekani, Cato Laurencin na Profesa Kelvin McGuigan kutoka Ireland.
Kwa mujibu wa Unesco, Profesa Tu Youyou, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya Tiba ya mwaka 2015, anatambuliwa kwa utafiti wake juu ya magonjwa ya vimelea ambapo aligundua dawa mpya ya kupambana na ugonjwa wa malaria, ambayo ilitibu maelfu ya wagonjwa nchini China na ulimwenguni kote miaka ya 1980.
Tuzo hiyo pia ilikwenda kwa Dk. Cato Laurencin, wakitambua mchango wake wa msingi katika upatikanaji wa huduma bora za klinik na mifumo sahihi ya utoaji wa dawa.
Kwa mujibu wa Unesco, McGuigan wa Ireland anatambulika kwa utafiti wake uliosadia kupunguza makali juu ya maendeleo na utekelezaji wa teknolojia ya kuzuia maji ya jua (SODIS) kupambana na magonjwa yanayotokana na kukosa maji safi na salama ya kunywa katika Bara la Afrika na Asia.
Washindi hao kwa pamoja watazawadiwa kiasi cha Dola za Marekani 350,000 ambapo sherehe ya utoaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Februari mwakani katika Jiji la Addis Ababa, nchini Ethiopia, kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika.
Tu Youyou mwenyewe anakiri kuwa alilazimika kujitolea maisha yake kwa kufanya kazi bure kwa nia moja tu ya kuhakikisha anaaacha alama kwenye maisha yake, jambo ambalo amefanikiwa kulitimiza na hii leo kuonekana shujaa.
Tu Youyou ni mwanasayansi wa kwanza nchini China kupokea tuzo ya Nobel katika kipengele cha ugunduzi wa Sayansi ambapo wakati anafanya ugunduzi huo hakuwahi kuwa daktari, kuwa na shahada ya dawa wala kupata mafunzo ya ugunduzi wa kisayansi kutoka vyuo vya nje ya China, jambo ambalo liliwasisimua watu wengi mara baada ya ugunduzi wake kuzaa matunda.
Tu Youyou alizaliwa 1930 katika Mji wa Ningbo, Pwani ya Mashariki mwa China. Katika familia yake jambo la kumsomesha lilikuwa ni mtihani mzito kwake na kwa kaka zake wanne kutokana na changamoto ya kifedha.
Akiwa na miaka 16 alilazimika kusitisha masomo kwa muda wa miaka miwili kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu.
Baada ya kurejea shule kwa mara nyingine, ndipo aliamua kujikita kusomea masuala ya dawa, lengo likiwa ni kusaka tiba ya magonjwa yaliyomtesa na kumtenga mbali na shule.
Akiwa katika Chuo cha Ufundi cha Beijing, akijifunza namna ya kuainisha mimea ya dawa, kutoa viungo vyenye kazi na kuangalia muundo wa kemikali.
Alipohitimu, mwaka 1955 akiwa na miaka 24, alipewa kazi katika Chuo kipya cha Tiba ya Jadi ya Kichina, ambapo alitakiwa kukaa kwa muda mrefu zaidi.
Kuanzia 1959 hadi 1962, alichukua kozi ya dawa ya jadi ya Wachina kwa watafiti waliopata mafunzo katika njia za kisasa za Magharibi.
Anasema: “Kuna wakati ilibidi nimuache binti yangu wa mwaka mmoja kwa wazazi wangu, na kumweka mtoto wa miaka minne kwenye kitalu, na hii yote ni kutokana kwamba kazi ndiyo ilikuwa kipaumbele changu hivyo, nilikuwa tayari kujitolea maisha yangu yote.”