NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
MWANAFUNZI Hassan Gwaay wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora aliyeshika nafasi ya kwanza katika watahiniwa kumi bora waliofanya vizuri kitaifa kwenye masomo ya sayansi katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotangazwa jana, amesema matokeo aliyoyapata hakuyategemea.
Hassan alitangazwa kushika nafasi hiyo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (Necta), Dk. Charles Msonde, wakati alipokuwa akitangaza matokeo hayo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka nyumbani kwao mkoani Manyara, Hassan ambaye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia yao, alisema anamshukuru Mungu kumwezesha kuongoza nafasi hiyo.
Hassan alisema alipata nafasi hiyo kupitia mchepuo wa PCM ambapo alikuwa akisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu na katika matokeo ya jumla amepata daraja la 1.3
“Matokeo yamenishangaza…sikutegemea kama ningeweza kuwa mwanafunzi bora katika masomo ya sayansi kwa mwaka huu, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata ufaulu wa kiwango cha juu, nimefurahi sana,” alisema Hasaan.
Alisema anaamini matokeo hayo ni mwanzo mzuri wa kumwonesha njia ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi mkubwa nchini.
“Tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana masomo ya sayansi, lengo langu ni kuwa mmoja kati ya engineers (wahandisi) wakubwa nchini,” alisema Hassan.
Alisema pamoja na kufaulu vizuri lakini hana ndoto za kusoma katika vyuo vya nje ya nchi kwa kuwa anaamini uwezo wa elimu inayotolewa na vyuo vya hapa nchini.
Akizungumzia historia yake ya elimu, alisema alijiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Tabora baada ya kufaulu vizuri katika Shule ya Sekondari Benjamini William Mkapa iliyopo Mererani Manyara ambako alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Shule hiyo ni ya kata, kidato cha nne nikapata ufaulu wa divisheni 1.10, ndipo nikachaguliwa kujiunga na Tabora Boys, nikiwa shuleni Tabora mara nyingi darasani nilikuwa nashika nafasi ya nne ama ya tano,” alisema Hassan.
Alisema alipofika kidato cha sita katika mitihani ya maandalizi (mock) alipata divisheni 4.3 huku akitaja sababu kubwa ya mafanikio yake ni kujali muda na kupanga vizuri ratiba za kujisomea.
“Mimi nilikuwa nina ratiba mbili, ratiba ya kwanza iliyokuwa ikiniongoza ilikuwa ni ya shule ambayo tulikuwa tukiingia darasa kuanzia saa moja hadi saa tano na baadaye tunarudi tena hadi saa kumi jioni,” alisema Hassan.
Alisema ratiba ya pili ilikuwa ikiongozwa na yeye mwenyewe ambapo baada ya muda wa kutoka darasani saa kumi alikuwa akijisomea hadi saa 12 na kupumzika kidogo baadaye anarudi kujisomea hadi saa mbili usiku.