27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyemuua Mwangosi jela miaka 15

Mjane  wa Marehemu Daud Mwangosi, Itika  Mwangosi, akisalia kabla ya  kuzungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa jana baada hukumu ya miaka 15 jela ya Askari Polisi  aliyemuua mume wake.
Mjane wa Marehemu Daud Mwangosi, Itika Mwangosi, akisalia kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa jana baada hukumu ya miaka 15 jela ya Askari Polisi aliyemuua mume wake.

Na RAYMOND MINJA, IRINGA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa, imemhukumu kwenda jela miaka 15 askari polisi Pasficus Simon, kwa   kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, 2012 eneo la Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa, baada ya askari kuzuia mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akisoma hukumu hiyo jana kwa zaidi ya saa moja, Jaji Paul Kihwelo, alisema katika kutoa adhabu hiyo mahakama ilipitia maombi ya pande zote mbili.

Alisema upande wa mashtaka ulitaka mshtakiwa afungwe maisha jela, huku upande wa utetezi ukitaka aachiwe huru kutokana na sababu mbalimbali alizotoa.

Alisema kuwa licha ya pande zote mbili kuvutana, kila mmoja akiegemea upande wake, suala la adhabu gani apewe mshtakiwa litabaki kuwa ni la mahakama kwa vile hukumu si suala la hesabu bali ni la sheria.

“Mahakama itajikita katika mambo   mbalimbali ikiwamo aina ya kosa, mazingira lilipotokea tukio, masilahi ya familia na masilahi ya taifa kwa ujumla,” alisema.

Jaji Kihwelo alisema mahakama hiyo iliangalia pia haki kwa vile adhabu huwa haitolewi   kulipiza kisasi, bali hutolewa kama onyo, funzo au kuikanya jamii kutokorudia kosa hilo, kwa sababu kwa kufanya hivyo atakuwa anavunja kanuni na taratibu za nchi, hivyo naye adhabu inaweza kumkuta.
Alisema kumwachia huru mshtakiwa kupitia sheria namba 38 kama wakili wa upande wa utetezi, Rwezeura Kaijage alivyoomba, haiwezekani, na si jambo la uungwana kwa vile kosa alilotenda mshtakiwa ni kubwa.

“Kuachiwa huru au kupewa adhabu nyingine, jamii huko nje itapoteza imani na mahakama ambayo ndiyo chombo cha mwisho kinachotegemewa katika kutenda haki.
“Kumfunga mshtakiwa kifungo cha maisha jela au kifungo cha muda mrefu kama walivyoomba Jamhuri, haitasaidia kurudisha uhai wa marehemu Daud Mwangosi.

“Tunajua machungu waliyopata familia ya marehemu na tunajua machungu watakayopata ndugu wa mshtakuwa baada ya adhabu kutolewa, lakini niseme tu mahakama itaangalia mizania na kuangalia adhabu gani inayomfaa mshtakiwa wa kosa hili,” alisema Jaji Kihwelo na kuongeza:
“Kosa lililotendeka ni kubwa, na marehemu aliuawa kifo cha kinyama ambacho hakielezeki. Na kwa kuwa mtuhumiwa alifanya uzembe na kusababisha kifo, kwa kuwa ameshatumikia miaka minne gerezani, mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 15 gerezani na upande wowote ambao unaona haki haijatendeka, unaruhusiwa kukata rufaa.”

Baada ya Jaji Kihwelo kutoa hukumu hiyo, baadhi ya askari walionekana hawakufurahishwa, huku wengine walionekana kumwaga machozi.

Wengine walifunika nyuso zao kwa mikono huku wengine wakikimbilia kumfunika kwa shuka mshtakiwa na kumzingira ili waandishi wa habari wasiweze kumpiga picha.

Akizungumzia hukumu hiyo huku machozi yakimmiminika na kushindwa kuzungumza kwa kirefu kutokana na kulia, mke wa marehemu, Itika Ruben Mwangosi, aliishukuru mahakama na  waandishi wa habari kwa ushirikiano waliouonyesha kwake tangu kifo cha   mume wake hadi siku ya hukumu hiyo.
Rais wa Klabu za Waandishi Tanzania (UTPC), Deodatus Msokolo, alisema   adhabu iliyotolewa ni jambo la msingi kwa tasnia ya waandishi wa habari, ambayo dunia na Tanzania kwa sasa inajua kuwa Jeshi la Polisi lilimuua mwandishi wa habari kinyama.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliendelea kulaani hatua ya polisi kutumia nguvu kubwa kuwadhibiti wanahabari waliofika mahakama hapo   kuripoti kesi hiyo, huku wengine wakiwaelekeza waandishi kufanya kazi kama wanavyotaka wao (polisi).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles