Aliyemtumbua Serena ataka ubingwa

0
797

karolina-pliskovaLAS VEGAS, Marekani

NYOTA wa mchezo wa tenisi, Karolina Pliskova, ambaye alihitimisha safari ya gwiji, Serena Williams katika michuano ya US Open, amedai kuwa anataka kunyakua taji la mashindano hayo.

Raia huyo wa Czech, alimchakaza Serena kwa seti 6-2 7-6 (7-5) katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi.

Kabla ya kumpoteza Serena, Pliskova, mwenye umri wa miaka 24, hakuwahi kuvuka raundi ya tatu katika michuano hiyo mikubwa nchini Marekani.

Baada ya kumtupa nje mwanadada mwenzake huyo ambaye anashika nafasi ya kwanza kwenye viwango vya ubora kwa upande wa wanawake, Pliskova anatarajiwa kumvaa Angelique Kerber katika mtanange wa fainali.

Kerber wa Australia alitinga fainali ya US Open, baada ya kumfunga Carolina Wozniacki kwa seti 6-4 6-3.

“Mara kwa mara niliota kuchukua ubingwa kwa kutinga nusu fainali na hatimaye kucheza mchezo wa fainali. Ni matokeo makubwa kwangu,” alisema mrembo huyo.

“Naamini sitoishia hapo, bado kuna hatua moja mbele. Nitafanya vyovyote kuhakikisha nanyakua ubingwa.”

Pliskova amekuwa tishio katika mchezo wa tenisi katika siku za hivi karibuni na kitendo chake cha kumfunga Serena kimemfanya kushinda michezo 11.

“Ikiwa utajiamini unaweza kumfunga yeyote hasa kwa upande wa wanawake. Si mchezo wa tenisi tu ila muda mwingine ni suala la kiakili,” alisema.

“Hivyo sasa naamini kuwa naweza kuwapoteza hata wachezaji wakubwa.”

Walipokutana kwa mara ya mwisho, Kerber alipoteza mchezo mbele ya Pliskova.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here