Aliyeipiga tatu Yanga aitwa Stars

0
880
Straika wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi

WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

BAADA ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ katika mchezo dhidi ya Yanga, straika wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi, amejumuishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘ Taifa Stars’ kitakachoikabili Rwanda, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa).

Nchimbi alifunga mabao hayo, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3.

Kaimu Kocha Mkuu wa Stars,  Etienne Ndayiragije juzi alitaja kikosi cha timu hiyo kitakachoikabili Rwanda Oktoba 14, mwaka huu jijini Kigali.

Nchimbi hakuwepo katika kikosi kilichoitwa awali kwa ajili ya michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani(Chan) na ile ya Afcon, lakini mabao yake ya juzi yameonekana kumshawishi Ndayiragije.

Stars baada ya mechi na Rwanda, itakuwa na kibarua kingine Chan dhidi ya Sudan, mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 18, jijini Khartoum.

Mchezo wa kwanza ulipigwa jijini Dar es Salaam, ambapo Sudan iliichapa Stars bao 1-0.

Akizungumzia kuitwa kwake Stars, Nchimbi, alisema alimshukuru Ndayiragije kwa kumuamini kuwa anaweza kuisaidia timu ya Taifa.

“Nipo katika Ligi Kuu kwa muda mrefu, kufunga hat trick ilikuwa ni malengo yangu siku zote,  nashukuru nimefanikiwa na nimeitwa timu ya Taifa, nitajitoa huko pia pale nitakapopata nafasi,”alisema Nchimbi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here