23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Aliyefiwa mtoto, kufukuzwa kazi akidai haki amlilia Rais Magufuli

Na Bakari Kimwanga -Dar-es-salaam

AMA kweli hujafa hujaumbika. Ndivyo unaweza kusema, baada ya Hussein Liongo, kujikuta akifukuzwa kazi na kufiwa na mtoto wake ndani ya siku moja kwa kile alichoeleza manyanyaso ya mwajiri wake, Kampuni ya Akberalis Hardware & Electric Ltd.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika mahojiano maalumu, Liongo alisema kuwa tangu mwaka 2017, amekuwa akiishi maisha magumu huku mwajiri wake akishindwa kutekeleza amri ya mahakama inayomtaka kulipa stahiki zake.

Alisema kuwa kwa sasa amekuwa akiishi kwa kuhangaika,  huku akimwomba Rais Dk. John Magufuli kuwaangalia baadhi ya wamiliki wa kampuni ambao hutumia kivuli cha uwekezaji kunyanyasa wafanyakazi.

“Oktoba Mosi, 2017 ilikuwa siku mbaya sana katika maisha yangu, kwanza nilikuwa nauguliwa na mtoto wangu ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na siku hiyo mkurugenzi wa Kampuni ya Akberalis, Juzer Alibhai, aliahidi kutulipa mishahara yetu, lakini katika hali ya kustaajabisha ilipotimu saa 5 asubuhi, alisema hawezi kutulipa huku akitutaka tuendelee na kazi.

“Lakini wakati huohuo nilitoka kupigiwa simu na mke wangu ambaye alikuwa hospitali akiniambia kuna baadhi ya dawa natakiwa kupeleka, ilipofika saa 5:30, nilimwambia bosi wangu (Juzer) nina mazungumzo naye.

“Lakini katika hali ya kushangaza nilijikuta natukanwa na kudhalilishwa mbele ya wafanyakazi wenzangu na kunieleza amenichoka kama kuuguliwa na mtoto wangu yeye haimuhusu, ila Mungu alinipa ustahamilivu nikanyamaza kimya.

“Baada ya dakika 20, niliitwa na mmoja wa wafanyakazi wenzangu ambaye yupo karibu na bosi na kunikadhi barua ya kufukuzwa kazi. Na ndani ya muda huo huo nikajikuta tena napokea simu ya mke wangu akiniambia mtoto wangu Sumaiya, amefariki dunia.

“Niliona dunia chungu, sikuwa na la kufanya, kazi nimepoteza na mtoto nimepoteza ndani ya siku moja. Hata hivyo nilishukuru msamaria mwema mmoja nilimweleza yaliyonifika, nashukuru alinisaidia ikiwamo kulipa gharama za matibabu Muhimbili na hatimaye kufanikisha shughuli za mazishi ya mtoto wangu,” alisema Liongo.

Baada ya kumaliza shughuli za msiba, alisema alikaa chini na kuanza kupata ushauri ambapo alikwenda kufungua shauri Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) namba CMA/DSM/ILA/R.1091/17/1057, ambayo Januari 2, 2019 chini ya Jaji Mwakisopole E.I, ilitoa uamuzi na kuamuru alipwe stahiki zake Sh milioni 1.9 ndani ya siku 14.

Pamoja na uamuzi huo hadi sasa mwajiri wake huyo amekuwa akiminya haki yake na kutomlipa kwa wakati kama alivyoamuriwa kwa mujibu wa sheria.

“Nimekuja hapa nikiamini nitapata haki zangu kwa kilio changu kufika kwa Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa au hata Waziri wa Kazi, ili waone au kuingilia kati suala langu. Leo mimi raia mnyonge nimefukuzwa kazi na kupoteza mtoto wangu, lakini huyu bwana (Mkurugenzi Akberalis Hardware & Electric Ltd) hataki kunilipa haki zangu.

“Si yeye tu, tena amezungukwa na wajanja ambao wamekuwa wakimshawishi kutonilipa haki zangu, nashindwa kujua nimekosea nini mimi maskini, naishi kwa tabu, nyumba nimepanga na huenda tu navumiliwa kwa haya yaliyonikuta, lakini mbele yangu naona giza nene kuhusu maisha yangu.

“Kaka yangu (mwandishi) wakati mwingine naishi kwa shida na hata kuhisi labda nimekosea kwa Mungu wangu na sistahili kuwapo katika uso wa dunia hii.

“Roho inaniuma sana na kujiona ni sawa na kifaranga kilichoondokewa na mama yake katikati ya jangwa, najua kwa sababu mimi maskini sina sauti mbele ya tajiri, ila najipa moyo ipo siku Serikali yangu kupitia Rais wetu John Magufuli muujiza utashuka na haki yangu nitapata,” alisema Liongo.

MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi wa Akberalis Hardware & Electric Ltd, Juzer Alibhai, alimtaka mwandishi amtafute baadaye kwa kuwa yupo barabarani anaendesha gari.

MTANZANIA: Habari naitwa …(jina la mwandishi) je, unamfahamu Hussein Liongo?

Juzer: Unasema?… Nipo barabarani nitafute baadaye.

Hata hivyo baada ya saa moja alipopigiwa tena, alikata simu na baada ya muda alipiga mtu aliyejitambulisha kwa jina la Idrisa Kassim, ambaye alidai ni meneja wa Kampuni ya Akberalis Hardware & Electric Ltd na ameelezwa na bosi wake atoe ufafanuzi.

“Ni kweli tunamtambua Liongo, alikuwa mfanyakazi wa Akberalis Hardware & Electric Ltd, lakini hata hilo la kutolipwa anatakiwa kurudi tena CMA ili aeleze suala la kutolipwa kama tuzo ilivyotaka. Ninaomba niishie hapo, asante,” alisema Kassim.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles