ALIYEDAIWA KUFUFUKA BAADA YA KUFARIKI DUNIA AOMBEWA

0
604

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SEIF  Ramadhan (33), mkazi wa Mtaa wa Relini, mjini Dodoma, aliyedaiwa kufa na kuzikwa kisha akaonekana, amefanyiwa dua nyumbani kwao.

Dua hiyo ilifanyika jana nyumbani kwao Mtaa wa Relini na kuongozwa na Sheikh wa Msikiti wa Kizota, Ahmed Mkoma.

Katika dua hiyo walihudhuria ndugu, jamaa, majirani na marafiki huku Seif akiwa amevaa kanzu na baraghashia.

Wakati dua ikiendelea, Seif alikuwa ameinama huku akimuomba Mwenyezi Mungu kimya kimya.

Katika maelezo yake, Sheikh Mkoma alisema wameamua kufanya dua hiyo na kutoa sadaka ya chakula kwa sababu jamii iliamini kijana huyo alikuwa amekwisha kufariki dunia.

“Tunafanya dua pamoja na hii riziki kwa ajili ya kumshukuru Allah kwa huu muujiza uliojitokeza. Tunajua kuna mengi yanasemwa, lakini yaache yasemwe, kikubwa ni Seif kuwa mzima,’’alisema Sheikh Mkoma.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya dua hiyo, mama mzazi wa Seif, Sarah Michael, alisema dua hiyo ilifanyika  kumshukuru Mungu kwa kijana wao kuonekana akiwa hai.

Alisema   yote yanayosemwa juu ya mtoto wake anamwachia Mungu ila jambo analoshukuru ni kuonekana kwa mwanae akiwa hai.

“Tumefanya dua na yote yanayosemwa tunamwachia Mungu, ila jambo la kushukuru ni kuonekana kwa mtoto wetu akiwa na afya njema,” alisema Sarah.

Alipoulizwa kuhusu kaburi lililopo nyumbani kwake ambalo alizikwa mtu mwingine ikidhaniwa ni Seif, alisema ataendelea kuliacha kwa kuwa mtoto wake ameshapatikana.

“Siwezi kufukua kaburi kwa sababu mwanangu yupo, sasa presure ya nini!’’alisema Sarah.

Diwani wa Kata ya Kizota, Jamali Yaled (Chadema), aliwataka wananchi kuwa watulivu huku akiitaka familia ya Seif kulitunza kaburi alimozikwa mtu mwingine waliyedhani ni Seif.

“Inawezekana Mungu amepanga huyo aliyezikwa humo  aje azikwe na watu wengi.

“Kwa hiyo, ndiyo maana kuna kauli inasema ‘tuwe na mwisho mwema’ kwa sababu  kama mlichukua mwili wa mtu mwingine mkadhani ni wa kwenu, basi huyo mtu ndiyo mwisho mwema wake kwa vile  amezikwa na watu wengi,’’alisema Yaled.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here