MURUGWA THOMAS-URAMBO
MAHAKAMA ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, imeahirisha shauri la uhujumu uchumi ambalo linawakabili watuhumiwa watano akiwemo George Mbuga ambaye alidanganya amekufa ili alipwe mafao kwa mkupuo hadi Januari 23, mwaka huu, akiomba apatiwe dhamana
Shauri hilo la uhujumu namba 15/2019 liliahirishwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Hassan Momba baada ya kusikiliza maelezo ya watuhumiwa kwamba wamewasilisha maombi ya dhamana mahakama kuu.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Joseph Mbwana uliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo na kusema kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Akihairisha shauri hilo hakimu Momba alisema kuwa ametoa muda mfupi ili iwe rahisi kwa watuhumiwa kufuatilia maombi yao dhamana Mahakama Kuu kwani ni haki yao.
Watuhumiwa wengine wa shauri hilo waliopandishwa kizimbani ni wakikabiliwa na tuhuma nane ni pamoja na Philomena Machelela, Andeori Kibuli, Thomas Paul na Alfayo Mfuru.
Awali katika shauri upande wa mashitaka uliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa makosa nane yakiwemo ya kula njama, kughushi nyaraka na kujipatia fedha Sh milioni 63.19.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 15/2019 ilidaiwa kuwa Mbuga na wenzake walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 8, 2018 na Aprili 16, mwaka jana wilayani Urambo Mkoa wa Tabora.
Upande wa mashtaka ulidai katika kosa la kwanza kuwa watuhumiwa kwa pamoja walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume cha sheria chini ya kifungu 384 ya sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 2002.
Shtaka la pili dhidi ya watuhumiwa wote ni kuongoza genge la uharifu na kujipatia kiasi cha Sh milioni 63. 197mali ya Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mashtaka mengine kwa washitakiwa hao ni kulitia hasara shirika la umma kiasi cha Sh milioni 63.197, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutoa taarifa za uongo na kughushi nyaraka.
Mwisho
CCM yawaonya wanaojipitisha majimboni
Na SAMWEL MWANGA
-MASWA
CHAMA Chama Mapinduzi (CCM) mkoani Simiyu kimewaonya wanachama wake ambao kwa sasa wameshaanza kujitipisha katika baadhi ya majimbo mkoani humo kwa lengo la kusaka nafasi za ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.
Onyo hilo limetolewa jana wilayani Maswa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Enock Jacob katika mkutano wa wazee wa Mji wa Maswa na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo(CCM), ambapo alisema kuwa kuna baadhi ya wanachama wa chama hicho wameshaanza kujipitisha majimbo kushawishi ili waweze kuchaguliwa kuwa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
Alisema ni lazima watambue kuwa muda wa kampeni za ndani haujaruhusiwa na yule atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba ya CCM.
Alisema ni vizuri wabunge na madiwani hasa wa chama hicho wakaachwa wakafanya kazi zao ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi zao walizozitoa sambamba na kutekeleza ilani ya chama hicho ambacho kilipewa ridhaa na wananchi kuongoza dola kwa kipindi cha miaka mitano.
“Tuna taarifa kuwa wapo wanachama wenzetu wameshaanza kupitapita kwenye majimbo na wengine kuanza kuwachafua wabunge walioko madarakani jambo ambalo halikubaliki kwani CCM ina utaratibu wake wa kupata wagombea wa udiwani, ubunge hatuwezi kuikubali hali hii tutachukua hatua,” alisema Jacob
Alisema kuwa anayetakiwa kufanya kazi za ubunge kwa miaka mitano ni mbunge pekee yake na kazi za udiwani ni diwani peke yake kwa sababu wamechaguliwa na wananchi na atakayejipitisha kwa wananchi kabla ya viongozi hao kumaliza muda wao wa miaka mitano chama hicho hakitawakubali.
Aliongeza kuwa wanaotia fujo kwenye majimbo na kata za madiwani ni maadui wa CCM huku akiwataka makatibu wa Wilaya wa CCM kuchukua hatua kwa mwanachama yeyote atakayeonekana kufanya vurugu za kuwachafua wabunge na madiwani wa chama hicho.
Pamoja na hali hiyo amempongeza Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanlaus Nyongo, kwa kuweza kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo kwa kuiletea maendeleo wilaya hiyo ambayo kwa sasa imetafsiri kauli ya Rais Dk John Magufuli ya Tanzania ya viwanda kwa kujenga kiwanda cha chaki, vifungashio pamoja na kiwanda cha kuchakata ngozi na unga lishe.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika jimbo hilo, Nyongo ambaye ni alisema wabunge wamepewa kazi ya kutekeleza ilani na ataendelea kuhakikisha wana Maswa wanapata maendeleo.