UNAWEZA kueleza kwa vyovyote vile kwa kadiri mawazo yanavyokutuma tafsiri ya kitendo cha mkazi huyu wa Cedar Buff katika Jimbo la Virginia nchini Marekani kulipa kodi kwa staili ya aina yake.
Ni mapema asubuhi ya Jumatano wiki iliyopita mfanyabiashara huyo Nick Stafford anawasili katika Idara ya Magari (DMV) tawi la Lebanon akiwa na toroli tano zilizojaa sarafu 300,000 zenye uzito wa pauni 1,600 ili kulipa kodi ya dola 2,987.45 sawa na Sh milioni 6.7.
Hakuondoka hapo hadi siku iliyofuata saa 7 usiku kwa vile kazi ya kuzihesabu iliyofanywa na wafanyakazi wa tawi hilo ilifanyika hadi usiku wa manane.
Yeyote anaweza kufikiria kuwa ili kukusanya sarafu nyingi kiasi hicho, kuzisafirisha na kusubiri siku nzima wakati wafanyakazi wa jimbo wakizihesabu kwa mkono, Stafford lazima atakuwa na sababu ya kufanya hivyo; kumaliza hasira zake! Ndiyo ukweli.
Wakati akiziwasilisha idarani hapo, mashine ya kuhesabu sarafu ilishindwa kuzihesabu hali iliyowalazimu wafanyakazi kutumia mkono, kazi iliyochukua saa saba kukamilika.
Hatua hiyo inajiri kufuatia mgogoro kati yake na idara hiyo kuhusu namna ya kuwasiliana na maofisa ili kulipa kodi. Kilichoonekana kwa mtazamo wa wengi waliosikia kisa hicho ni urasimu katika idara hiyo ya serikali.
Sakata hilo baina ya mtu mmoja dhidi ya timu nzima ya ofisi hiyo ya serikali inarudi nyuma Septemba mwaka jana wakati mfanyabiashara huyo alipomnunulia mwanawe gari, hii ni kwa mujibu wa tovuti yake mwenyewe.
Akifafanua zaidi, Stafford anasema mgogoro wake na DMV ulizuka kwa sababu idara hiyo haikuwa tayari kumpatia nambari za simu za kuwasiliana moja kwa moja ili kusajili magari matatu na kulipa ushuru. Alitaka mawasiliano ili afahamu wapi ni mahali sahihi pa kusajiri magari yake jimboni humo ukizingatia ana nyumba nne katika kaunti mbili tofauti.
Hivyo, katika tafuta tafuta yake katika mtandao wa DMV aliangukia katika tawi la ofisi hiyo la Lebanon, ambapo alikuta namba ya kuwasiliana – (804) 497-7100. Lakini namba hiyo ilimuelekeza akipigie simu kituo hicho kwa namba atakayopewa, akasubiri kupigiwa kwa saa nne bila mafanikio.
Baada ya juhudi za siku kadhaa aliweza kuwasilisha ombi la kutaka kupewa nambari ya moja kwa moja, akapewa, alipoipiga aliambiwa kuwa asingeweza kuitumia kuuliza maswali.
Stafford aliulizia maeneo mengine ya DMV jimboni humo, lakini tawi la Lebanon lilikataa kumpatia namba za matawi hayo mengine.
Hilo lilimlazimisha afungue kesi katika Mahakama ya Kaunti ya Wilaya Russel kuwasilisha malalamiko yake, akiwashitaki wafanyakazi wawili wa DMV na tawi zima la Lebanon.
"Haijalishi iwapo utalipa dola 300 kwa mwaka kama kodi au dola 3,000 kwa mwaka kama mimi kwa sababu ni uti wa mgongo wa taifa lililo na demokraisa huru ni sharti liwe na serikali iliyo na uwazi,” alisema.
Wakati wa usikilizaji wa kesi, jaji mmoja alipinga maombi yake matatu aliyowasilisha ikiwamo kutaka DMV na wafanyakazi wake wapigwe faini kwa kunyima raia haki ya kupata taarifa.
Lakini mahakama ilipoingilia Jumanne hiyo iliyopita, Stafford akakubali kufuta kesi akiamini ujumbe wake umefika. Aliweka mtandaoni namba zote za simu alizopewa na mwanasheria wa wilaya. Kwa kufanya hivyo, jimbo lilikuwa limekwepa kupigwa faini ya Dola za Marekani 500 kwa kukiuka sheria ya umma ya haki ya kupata taarifa.
Hivyo, kesho yake, Jumatano ndipo akaja na kituko hicho cha kuwasilisha shehena ya sarafu, kitendo alichokiri kuwa alifanya kusudi kama kulipa kisasi kwa wafanyakazi wa DMV, ambao walimsumbua kwa miezi kadhaa.
Kilichoshangaza zaidi alikodi watu 11 kumsaidia kuziweka sarafu katika toroli, ambazo zote tano ni mpya alizonunua maalumu kwa kazi hiyo.
Shughuli hiyo iliyojumuisha kukodi watu hao na kununua toroli mpya ilimgharimu Stafford dola 1,005 sawa na Sh milioni 2.3 bila kuhesabu dola karibu 3,000 alizolipa kama kodi ya mauzo kwa kununua magari mawili mengine.
Stafford anasema kuwa idara ya magari ililazimika kukubali malipo yake kwa sababu sheria ya Marekani kuhusu sarafu mwaka 1965 inasema sarafu ni fedha halali na zinaweza kutumika kulipa madeni, kodi na mishahara.
Hata hivyo, Stafford alisema kwamba wafanyakazi walitoa ushirikiano unaostahili ikiwamo kuweka mbele heshima licha ya yote yaliyotokea.