26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

ALINUSURIKA KIFO MEI 5, 2013 AMEFARIKI MEI 6, 2017

 

 

Na JANETH MUSHI, ARUSHA

MEI 6 mwaka huu Taifa liliingia katika giza nene baada ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent waliofariki dunia baada ya basi aina ya Mitsubishi Rossa namba T 871 BYS kutumbukia kwenye korongo eneo la Marera, Rhotia wilayani Karatu.

Ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi na walimu hao walipokuwa wakienda wilayani Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema (joint examination) na wanafunzi wenzao wa shule ya Tumaini Junior.

Shule hiyo ambayo katika matokeo ya mwaka jana ya darasa la saba ilishika nafasi ya pili kwa mkoa, imepata pigo kubwa ambalo si rahisi kusahaulika.

Itakumbukwa kuwa miaka minne iliyopita katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph lililopo Olasiti mkoani Arusha, kulitokea tukio la kurushwa kwa bomu, ambapo ilikuwa ni Mei 5, mwaka 2013.

Bomu hilo liliua watu watatu na kujeruhi zaidi ya 50 miongoni mwao alikuwapo Arnold Alex Swai aliyefariki katika ajali iliyotokea Karatu.

Tukio hilo liliacha kumbukumbu mbaya kwa mtoto ambaye sasa ni marehemu kwa kuwa mlipuko wa bomu ulimsababishia madhara makubwa mwilini.

Ilikuwa ni mwaka jana tu ambapo Arnold alihudhuria hospitalini kwa ajili ya kutolewa vyuma vya mabomu mwilini mwake, huku akijiona amepona lakini kumbe bado kifo kilikuwa kinaendelea kumfuata.

Huyu ni miongoni mwa watoto 32 waliofariki katika ajali hiyo.

Mtoto huyu ambaye alikuwa akisali katika kanisa Katoliki Parokia ya Utatu Mtakatifu Joseph, lililopo eneo la kwa Morombo, taarifa za kifo chake zilimshtua Paroko wa Parokia hiyo, Castelino Peddey ambaye wakati wa mlipuko wa bomu alikuwapo kanisani.

Akimzungumzia Arnold, Paroko huyo anasema kwa masikitiko wamewapoteza vijana wao ambao pia walikuwa wahudumu kanisani (alter boys), hivyo kuwataka waumini wawaombee wapate pumziko la milele.

 

WAZAZI WASIMULIA AJALI ILIVYOKATIZA NDOTO ZA WATOTO WAO

Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa mtoto huyo, Alex Amos anasema familia ilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwanawe.

Huku akibubujikwa na machozi, baba huyo alisema Arnold alikuwa mtoto wa pekee wa kiume kati ya watoto wanne alionao.

"Hakika jina la Bwana lihimidiwe, sina la kusema zaidi ila nakumbuka Arnold alikuwa akiishi vizuri na dada zake na majirani ndiyo maana alijitolea maisha yake kutumikia kanisa,"anasema mzazi huyo.

Anabainisha kuwa miaka minne iliyopita kijana wake alikuwa katika Shirika la watoto wa Kipapa na huku akitekeleza huduma hizo alipatwa na matatizo ya kujeruhiwa na bomu.

Mzazi huyo anasimulia kwa uchungu kuwa mwanawe alijeruhiwa mguu wa kushoto na bomu akapatiwa matibabu akapona.

"Licha ya kupatwa na mkasa huo mwanangu hakukata tama, aliendelea kutumikia Kanisa na aliamua kujiunga na watumishi wanaosaidia mapadri wakati wa azimisho la Misa Takatifu pale kanisani," anasema.

Alex anamzungumzia mtoto wake kwamba alikuwa mtiifu, mpole, hakuwa mkaidi na alionyesha upendo na kuishi maisha ya utume kwa padri.

Akizungumza kwa tabu mama mzazi wa Arnold, aliyejitambulisha kwa jina la Agripina Swai anasema hivi karibuni Arnold aliondolewa mwilini chuma kilichowekwa mguuni mwake kama sehemu ya tiba.

Anasema alijua mwanawe angekuja kuwa mtumishi wa Mungu, hivyo kuondoka kwake kumepoteza ndoto hiyo.

ASHUHUDIA MTOTO WAKE AKIFARIKI

Mosses Kivuyo ni baba wa Irene ambaye ni miongoni mwa wanafunzi 33 waliofariki katika ajali hiyo, anasema alifanikiwa kulifikia gari la wagonjwa (Ambulance) na kushuhudia mtoto wake Irene akikata roho.

Mzazi huyo anasema hakujua kama mwanawe ni miongoni mwa waliokufa, lakini alijipa moyo na kisha kuanza safari ya kutoka Arusha kwenda Rothia kwa ajili ya kuona watoto hao akiwamo mwanawe na alipokuwa njiani, alipigiwa simu na wauguzi wakisema mtoto wake anatakiwa kufanyiwa upasuaji.

Anasema mtoto wake akiwa na majeraha makubwa yaliyoambatana na maumivu makali, alitoa namba ya simu akiomba baba yake apigiwe kujulishwa kwamba amepata ajali akiwa katika safari ya masomo.

"Nilipopata taarifa nilienda shuleni nikitokea nyumbani Kwa Morombi, nikaamua kwenda eneo la tukio lakini baadaye nikapigiwa simu kwamba hali ya mwanangu si nzuri, yupo katika Hospitali ya Lutheran Karatu.

"Na mtoto ndiye alitoa namba ili nijulishwe kwamba anafanyiwa upasuaji kwa sababu alikuwa ameumia kichwa na mdomo," anasema mzazi huyo kwa uchungu.

Anasema alifika hospitalini akakuta mtoto anapandishwa katika Ambulance ili apelekwe Arusha lakini kabla gari halijaondoka mwanawe alikata roho akimshuhudia.

Kivuyo anasema binti yake Irene alikuwa wa kwanza katika familia yake yenye watoto watatu na alikuwa akilala bwenini shuleni hapo.

BABA WA  PRAISE

Baba Mzazi wa mwanafunzi Praise (14), Roland Mwaliambi akielezea alivyopokea taarifa za kifo cha mtoto wake, anasema alizipata akiwa jijini Dar es Salaam.

Anasema alipigiwa simu akiwa kikaoni, akafuatilia taarifa hizo na akajiridhisha kuwa mwanawe alikuwa amefariki dunia.

"Bahati nzuri wafanyakazi wenzangu walifanya utaratibu nikaondoka na ndege ya Coastal, hivyo nikawahi kufika mapema Arusha kuungana na familia.

"Hali ilikuwa mbaya, mke wangu hakuweza kulipokea kwa urahisi jambo hili, ilikuwa ngumu mno kwake, taratibu tunajaribu kurudi kwenye hali ya kawaida lakini bado," anasema.

Akimuelezea mtoto wake huyo, anasema tayari alikwisha jitambua na kujua anatakiwa kufanya nini anapokuwa shuleni na hasa katika masomo yake.

"Praise alijitambua mapema kwamba anahitaji kusoma na kufaulu, alikuwa na malengo ya kufika chuo kikuu. Lakini alipendelea kusoma na kuwa Padri. Hii ni kwa sababu alilelewa maisha ya kanisani na alikuwa akienda kutumikia kanisani Parokia ya Utatu Mtakatifu.

"Wakati napata taarifa za kifo chake tayari tulishachukua fomu za kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza Seminari ya Maua. Juni mwaka huu ilikuwa aende kufanya mitihani ya majaribio," anasema na kuongeza:

"Lilikuwa hitaji lake kubwa kusoma seminari, ndoto zimeishia hapo hata jana wakati akipoteza maisha kaka yake alikwenda shuleni hapa Arusha kuleta fomu zijazwe na walimu wa Lucky Vincent."

KUAGWA

Mei 8, Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwaongoza maelfu ya wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani katika ibada maalumu ya kuaga miili ya wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Akizungumza wakati akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Samia anasema Taifa linahuzunika kutokana na kuondokewa na nguvu kazi.

“Msiba huu si wenu peke yenu, Taifa zima linaomboleza pamoja nanyi kwa kuondokewa na nguvu kazi. Tulikuwa na malengo makubwa na wapendwa wetu hawa, kwa niaba yangu na niaba ya Rais amenituma niwafikishie salamu za pole na rambirambi zetu kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki mliofiwa na wapendwa wenu.

 “Tukio hili linatukumbusha wajibu wetu, ninapaza sauti kwa madereva wetu wawe makini wanapoendesha magari, wazingatie alama za barabarani lakini pia wasiendeshe magari wakiwa wametumia kilevi chochote. Ndio maana tunapiga vita matumizi ya dawa za kulevya maana pia ni chanzo cha matukio kama haya,” anasema.

Anabainisha kuwa ni jambo lisilopendeza katika nchi kusikia kila siku ajali inatokea na kupoteza maisha ya watu na kwamba kuanzia sasa Serikali itaweka alama zinazoonekana katika barabara zote ili madereva waweze kuchukua tahadhari.

 “Haipendezi kila siku kusikia ajali katika ,taasisi zote zinazohusika.  Wizara  kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani hakikisheni mnaweka alama za barabarani lakini pia magari ya abiria yakaguliwe na yabebe abiria kadiri ya uwezo wake,” anaagiza Samia.

Ni dhahiri kuwa Taifa linapaswa kujitafakari na kuzingatia ushauri uliotolewa na Waziri wa Elimu wa Kenya, Dk. Fred Matiagi ambaye wakati akitoa salamu za pole na rambirambi kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyata wa Kenya, alisema msiba huo ni wa wananchi wote wa EAC.

 “Nimetumwa na Rais Uhuru, tunahuzunika wote pamoja na ninyi wananchi wa Tanzania. Kwa siku hizi mbili tumefikiri kuhusu usalama wa watoto wetu, kuhusu usafiri wa watoto wetu ambao ni wanafunzi .Taifa la Kenya linaungana na wazazi ndugu na wananchi wote kuomboleza na kutoa pole, tunasema huu msiba unatuhusu wote,” anasema. 

Hivyo, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kushirikiana na Serikali kuhakikisha usalama wa watoto na kukaguliwa mara kwa mara kwa vyombo vya usafiri vinavyotumika kusafirisha wanafunzi ili kuepuka ajali zinazoepukika.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles