23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Alichosema AG Feleshi, kina mashiko

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

TASNIA ya Habari katika miaka michache nyuma, imepita katika kipindi kigumu kidogo. Ni kutokana na kuanzishwa ama kutungwa sheria zilizojikita katika kunyang’anya uhuru wa mwanahabari, kumtisha na kumuwekea vikwanzo kwenye utendaji wake.

Kuwepo kwa sheria hizo kandamizi, haraka tasnia ya habari ilianza kuzama kutokana na kuelemewa na utitiri wa sheria zisizotekelezeka ama zenye kujenga hofu kwa mwanahabari.

Utataribu wa serikali kutuhumu, kushitaji, kuchunguza na kisha kuhukumu yenyewe bila kufikisha chombo husika mahakamani, kwa kiwango kikubwa kumechangia kurudisha nyumba tasnia ya habari nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Eliezer Feleshi (wakwanza kushoto) alipokutana na Ujumbe wa TEF na MISA-TAN uliiongozwa na Mwenyekiti wa TEF, Dodatus Balile Juni 13, 2022 ofisini kwake jijini Dodoma.

Vyombo vya habari kadhaa vimeingia kwenye ‘tanuri’ hilo na kujikuta vikilazimishwa kuondolewa sokoni, udhaifu wa kukosa Bodi ya Ithibati ambayo ingeweza kuokoa vifungo visivyo vya lazima, kulisababisha kwa kiwango kikubwa athari kwa tasnia ya habari ikiwa ni pamoja na watumishi kupoteza kazi lakini pia serikali pia kukosa kodi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi anaamini kwamba, uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari iliyo huru, kwa kiwango kikubwa kunaweza kurejesha tabasamu kwa tasnia ya habari na wamiliki wa vyombo hivyo.

Anaamini kwamba, Bodi ya Itibati ya Wanahabari iliyo huru, inaweza kusimamia tasnia ya habari nchini na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hiyo.

Mei 13, 2021 Innocent Bashungwa, alipokuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (Kabla ya tasnia ya Habari kuhamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) alisema, serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Bashungwa alisema hayo wakati akiwasilisha makadiro ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema, Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, inaelekeza kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.

“Kwa sasa wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi hii,” na kuongeza “Baraza Huru la Habari litaundwa baada ya Bodi ya Ithibati kuanza kazi.” alisema.

Tofauti na mtazamo wa serikali, Jaji Feleshi alipokutana na wadau wa habari ofisini kwake bungeni jijini Dodoma, tarehe 13 Juni 2022 alisema, tasnia ya habari inapaswa kuwa na bodi yake inayotokana na wanahabari wenyewe ili kusimamia maadili na miiko ya wanahabari.

Sehemu ya vifungu vinavyoonekana kikwazo katika tasnia ya habari, Picha kwa hisani ya Tovuti ya Gazetini.

Namnukuu “ni vizuri tasnia ya habari ikiwa na bodi yake itakayotumika kuhakikisha inasimamia maadili ya wanahabari,.…naona muwe na ‘regulator’, bodi yenu moja, ili mmoja wenu akienda kinyume na maadili (ya uandishi wa habari), mnamshughulikia nyinyi wenyewe.”

Ushauru wa Jaji Feleshi ulibebwa na ‘tamaa’ ya mwanasheria huyo kutaka kuona bodi ya wanahabari ikifanya kazi ya kusimamia wanahabari kwa uhuru na bila kuingiliwa na yeyote nje ya wanahabari.

Na hivi ndivyo ilivyo katika kada zingine nchini ikiwemo Bodi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bodi ya Uhasimu na zingine.

Ushauru wa Jaji Feleshi ndio hasa tamanio la wadau wa habari nchini, ambapo moja na mambo yanayotia hofu ni pendekezo la muundo wa bodi ya wanahabari isioendana na ridhaa ama matakwa ya wanahabari.

Bodi ya Wanahabari inaoshikiliwa na serikali, hauwezi kuwa na tija kwa wanahabari na tasnia ya habari kwa ujumla. Bodi ya Wanahabari ili iweze kufanya kazi yake, inapaswa kuundwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe.

Ikiwa kada zingine nchini zimeunda bodi zao zinazotokana na wanataaluma na wa kada hizo, kwanini isiwezekani tasnia ya habari ikaunda Bodi ya Habari inayotokana na wanataaluma pekee wa tasnia hiyo?

Ni kwa muda sasa tasnia ya habari imekuwa ikivuja jasho kutokana na kuelemewa na sheria kandamizi, uundwaji wa sheria hizo kwa kiwango kikubwa umekuwa ukilenga kumshambulia mwanahabari na taaluma hiyo.

Utitiri wa vyombo vingi vilivyoelekezwa kusimamia tasnia ya habari kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari 2016, unaongeza mashaka kuhusu lengo la kutungwa kwa sheria hiyo.

Katika sheria hiyo Sehemu ya III na vifungu vyake 11, 12, 13, 14, 15, 16,17,18, 19, 20,21,22 na 23, pia Sehemu ya IV na vifungu vyake vyake 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33 &34 ambavyo vinazungumzia uundwaji wa Bodi ya Ithibato na Baraza Huru la Habari.

Sehemu hizi za Sheria zina vifungu ambavyo vinatoa mamlaka kwa vyombo viwili ambavyo majukumu yake yangeweza kutekelezwa na chombo kimoja. Kuwa na chombo kimoja kwa kiwango kikubwa, kunaweza kupunguza gharama za uendeshaji.

Uundwaji wa chombo kimoja cha Bodi ya Ithibati kinachotokana na wanahabari wenyewe, kinaweza kutekeleza majukumu ya yaliyomo katika vifungu vya sehemu ya tatu na ya nne ya sheria iliyopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles