22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ali Kiba ang’ara tuzo za muziki Tanzania 2015

AlikibaNa Festo Polea
MSANII Ali Kiba anayetamba na wimbo wa ‘Mwana’ na ‘Chekecha’, ameng’ara usiku wa juzi kwa kunyakua tuzo sita za muziki Tanzania zilizotolewa katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Tuzo alizonyakua ni wimbo bora wa Afro Pop, mtunzi bora wa mwaka Bongo Fleva, mtumbuizaji bora wa muziki wa mwaka wa kiume, mwimbaji bora wa kiume Bongo Fleva, wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa kushirikishwa na Mwana FA.
Katika tuzo hizo zilizoongozwa na mtangazaji wa kituo cha redio, East Africa, Zembwela na Dj Fety kutoka redio Clouds, waliomfuata Ali Kiba kwa tuzo ni mwimbaji wa taarabu, Mzee Yusufu aliyenyakua tuzo tatu ikiwemo mtunzi bora wa mwaka, mwimbaji bora wa kiume na kikundi bora cha mwaka Taarabu.
Wakati Ali Kiba akiwa kinara, aliyekuwa kinara wa tuzo saba mwaka jana, Nassib Abdul ‘Diamond Platinum’, mwaka huu amenyakua tuzo mbili ikiwemo video bora ya mwaka na wimbo bora wa Zouk/Rhumba.
Wengine walioibuka na tuzo mbili ni Vanessa Mdee aliyenyakua tuzo ya mtumbuizaji bora wa mwaka wa kike na mwimbaji bora wa kike Bongo Fleva, wakati tuzo ya mtunzi bora wa mwaka na msanii bora wa Hip Hop ikienda kwa Joh Makini huku Issa Mashauzi akinyakua tuzo ya mwimbaji bora wa kike na wimbo bora wa Taarabu.
Wengine walioibuka na tuzo usiku huo ni Yamoto Band iliyoibuka kikundi bora-Bongo Fleva, FM Academia iliibuka bendi bora ya mwaka huku Baraka Da Prince akinyakua tuzo ya msanii bora chipukizi. Wimbo bora wenye vionjo vya Asili ya Kitanzania ni ‘Waite’ umeimbwa na Mrisho Mpoto kwa ushirikiano na Felly Kano.

Mtayarishaji bora wa mwaka wa bendi ni Enrico na mtayarishaji bora wa wimbo wa mwaka Bongo Fleva ni Nahreel, huku mtunzi bora wa mwaka upande wa bendi akiibuka Jose Mara.

Nyingine ni wimbo bora wa Kiswahili wa bendi ni ‘Walewale’ wa Vijana wa Ngwasuma huku tuzo ya wimbo bora wa R&B ukiwa ni ‘Sisikii’ wa mchumba wa Vanessa Mdee, Juma Jux aliyekuwa nchini China kwa masomo.

Wengine ni rapa bora wa Hip Hop ambaye ni Profesa J, huku wimbo bora wa Afrika Mashariki ukiibuka ‘Sura Yako’ wa Sauti Sol. Marehemu Kapteni. John Komba ametunukiwa tuzo maalumu inayotolewa kwa watu maalumu kutokana na kufanikisha maendeleo ya muziki nchini ‘Hall of Fame’.

Maoni ya wasomaji
Maoni mengi kuhusu tuzo hizo yameonyesha mshangao kwa mwanamuziki wa muziki wa dansi, Christian Bella na wimbo wake wa ‘Nani kama Mama’ uliojizolea sifa kila kona kukosa tuzo hata moja katika tuzo hizo huku mwenyewe akiamini kwamba alistahili kupata tuzo nyingi.
Awali kabla ya utolewaji wa tuzo hizo, Bella aliweka wazi kwamba anaamini amekwenda kupata tuzo lakini akikosa haitakuwa mbaya kwake kwa kuwa mashabiki wake watapata burudani aliyoitoa katika usiku huo, hata hivyo baada ya utoaji tuzo hizo kukamilika wengi akiwemo na yeye hawakuamini huku wakibaki na maswali amekosaje tuzo hata moja kwa wimbo wa ‘Nani kama Mama’.
Wengine waliotoa maoni katika utoaji tuzo hizo ni wale waliotaka kuwe na uhusiano wa wimbo bora unaotamba na kuzoa tuzo nyingi katika tuzo hizo ndiyo utoe prodyuza bora.
Madai hayo yamekumbusha mwaka ambao msanii wa muziki wa Bongo Fleva, 20 Percent alizoa tuzo tano za muziki wa Tanzania lakini prodyuza wa wimbo uliomwezesha kushinda hakushinda hata tuzo moja kama ilivyokuwa kwa wimbo bora na prodyuza aliyetengeneza wimbo uliotamba mwaka huu na kuwa bora ndiye aliyetamba kipindi 20 Percent aliposhinda tuzo tano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles