25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Algeria bila ya Abdelazizi Bouteflika

Othman Miraji

NI wiki chache zilizopita niliandika katika ukurasa huu juu ya nchi ya Kaskazini ya Afrika- Algeria- ambayo baada ya wiki sita zijazo itakuwa na uchaguzi wa urais.

Nimeona ni bora mara hii niizungumzie tena nchi hiyo ambayo rais wake aliye mgonjwa kwa muda mrefu, Abdelazizi Bouteflika (82), atagombea tena wadhifa huo.

Wiki iliyopita maelfu kwa maelfu ya watu waliandamana katika Mji mkuu wa Algiers- idadi kubwa kabisa ya watu ambayo haijwahi kushuhudiwa- wakipinga uwezekano wa Bouteflika kukamata madaraka kwa awamu nyingine ya tano ya miaka mitano.


Baada ya wiki mbili za matibabu huko Geneva, Uswisi, Rais huyo amerejea nyumbani kutokana na hali ya kisiasa kuzidi kuwa mbaya nchini mwake. Jumapili iliyopita kulikuwapo mgomo mkubwa wa nchi nzima, maduka mengi yalifungwa. Pia wafanyakazi wa kampuni waligoma kwenda kazini wakipinga Bouteflika kuwa mtetezi wa uchaguzi.


Hasa katika mkoa wanakoishi Waberber, Mashariki ya Algiers, mwito wa kuungwa mkono mgomo mkuu uliitikiwa kwa nguvu. Katika mji mkuu usafiri wa umma ulikosekana kwa sehemu kubwa, huku maandamano yakifanywa katika miji mingine ya nchi hiyo.
Hapo jumamosi iliyopita, wanafunzi wa vyuo vikuu waliamrishwa waende makwao kwa likizo, ikiwa wiki mbili kabla ya wakati, serikali ikitarajia kwamba hatua hiyo itapunguza maandamano.

Kwa kawaida, wanafunzi wengi hushiriki kwenye maandamano. Hapo kabla ni vijana na wanafunzi waliokusanyika katika miji kumpinga Bouteflika na utawala wake unaoonesha unakata roho. Zaidi ya vyama vya kisiasa 15 na vya wafanyakazi viko nyuma ya maandamano na migomo hiyo.


Hapo kabla, kwa mara ya kwanza kulitokea mapambano makali baina ya polisi na vijana waandamanaji ambapo kwa mujibu wa polisi watu 200 walikamatwa- wakiwamo wale waliopora mali na polisi 112 walijeruhiwa. Katika sehemu nyingine za nchi maandamano yalibakia kuwa ya amani.


Siku ya Jumapili chama tawala cha Ukombozi wa Taifa (National Liberation Front) kilimaliza ukimya na kutangaza kwamba kiko tayari kuutanzua mzozo huo kwa kushirikiana na vyama vingine. Kilisifu vuguvugu la malalamiko hayo kuwa ni chemchemi kwa taifa kujivunia.

Pia vyama zaidi vya siasa vimetaka uchaguzi wa rais uahirishwe kufanywa na kiwepo kipindi cha mpito. Kesho (alhamisi) Baraza la Katiba lazima liamue watu gani wataruhusiwa kugombea uchaguzi huo.

Kuna uwezekano kwamba baraza hilo litakataa Bouteflika agombee uchaguzi huo. Hiyo itakuwa ni njia kwa watawala kuiepuka aibu, pia ni kuihifadhi nchi hiyo isitumbukie zaidi katika dimbwi la matatizo. Pindi wagombea wengine nao wataacha kuwania, basi njia itakuwa wazi kwa mwanzo mpya.

Na pindi awamu ya sasa ya utawala wa Bouteflika itakapomalizika rasmi hapo Aprili, basi Rais wa Baraza la Senate la Bunge, Abdelkader Bensalah, ataapishwa kuwa rais wa mpito. Itambidi yeye aitishe uchaguzi mpya. Suluhisho hilo huenda likalizuia jeshi kuwaza kujiingiza moja kwa moja kutaka kuitawala nchi hiyo.


Bouteflika anaitawala Algeria tangu 1999, lakini kutokana na ugonjwa wa kiharusi alioupata miaka sita iliyopita, haonekani hadharani. Licha ya hayo, mwanasiasa huyo ametangaza kutaka kugombea uchaguzi wa April 18, ikiwa ni mara ya tano.

Waalgeria wengi wanashuku kwamba kikundi cha washauri wake wa karibu walio na madaraka pamoja na majenerali wa jeshi wako nyuma ya wazo hilo la kutaka kuendelea kung’ang’ania madaraka.


Kwa hakika, Algeria imo katika mzozo. Watu tayari wanazungumzia kwamba nchi hiyo inaelekea katika Mapinduzi. Neno Mapinduzi limo vinywani mwa watu, na pia neno machipuko linatajwa.

Lakini haya yanayoonekana si machipuko mapya ya Kiarabu, kwani maandamano ya sasa yamesheheni zaidi katika maeneo wanakoishi Waberber. Tangu miaka mingi Mkoa wa Waberber ulioko Kaskazini ya nchi hiyo ndio umekuwa kiini cha uasi dhidi ya Serikali kuu ya Algiers.


Uasi wa Mwaka 2011 katika nchi kadhaa za Kiarabu uliwakumbusha Waalgeria kipindi cha giza katika nchi yao. Wakati Waarabu katika miji ya Damascus (Syria) na Tunis (Tunisia) wakijaribu kuivunja mifumo mikongwe ya tawala za kidikteta katika nchi zao, wananchi wa Algeria walivikumbuka vita vyao vya kienyeji vilivyochukua hapo kabla maelfu ya roho za watu.


Mkuu wa Jeshi katika Algeria, Ahmed Galid Salah, wiki iliyopita alikumbusha kipindi hicho cha giza na maumivu. Alisema jeshi litahakikisha usalama unaimarishwa na halitaiacha nchi itumbukie tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Maneno hayo ya mkuu huyo wa jeshi yalikuwa ni onyo. Vita vya kienyeji vya miaka ya tisini vilichukua roho za watu 60,000 -150,000 na vilitanguliwa na machipuko ya kisiasa mwisho wa miaka ya themanini kwa kufanywa uchaguzi wa kidemokrasi.

Waislamu wenye siasa kali walishinda katika uchaguzi huo, lakini jeshi likajiingiza, likatumia nguvu na kukataa kabisa Waislamu wenye siasa kali kuitawala nchi hiyo.


Ndipo mwaka 1999 alichomoza usoni kabisa Abdelaziz Bouteflika. Punde baada ya Algeria kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa, Bouteflika, akiwa kijana kabisa, aliitumikia nchi yake kwa miaka mingi kama Waziri wa Mambo ya Kigeni.

Alichangia kuutuliza ugomvi baina ya jeshi na Waislamu wenye siasa kali kwa kutoa msamaha wa jumla na kuwarejesha wapiganaji wa Kiislamu katika maisha ya kiraia. Utulivu na amani vikarejea katika Algeria.


Leo, miaka 20 baadaye, Waalgeria wanautaja utawala wa Bouteflika kuwa ni mamlaka, neno linalofaa kuelezewa mchanganyiko wa wanasiasa, wanajeshi wa vyeo vya juu na wafanyabiashara wakubwa pamoja na maafisa wa usalama.

Watu hao wamegawana baina yao utajiri wa nchi. Wao wanaamini kwamba ilivyokuwa mtu wa kawaida anaitegemea dola, basi mtu huyo hatofanya jambo lolote dhidi ya uongozi wa dola hiyo.


Lakini wakati umebadilika. Bouteflika baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi amebaki anaketi tu kwenye kiti cha kusukumwa, mwili wake ukiinama upande wa kushoto, mdomo uwazi kila wakati, huku macho yakitumbua tu. Hotuba yake ya mwisho hadharani aliitoa Mwaka 2012.

Hivi sasa anashuhudia maandamano yanayofanywa nchi nzima dhidi yake ilhali akiwa kitandani. Kilichobakia kwa Bouteflika ni mwili wake tu, ulio tu kama sanamu.

Bouteflika amekwisha, kimwili na kiakili pia.
Waalgeria wengi hawamjui rais mwingine isipokuwa Bouteflika, lakini pia Waalgeria wengi hawajavishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe na ikiwa walivishuhudia basi walipokuwa watoto.

Zaidi ya hayo, utajiri wa mafuta na gesi ya ardhini katika nchi hiyo umepungua. Utajiri huo ndio uliowatuliza raia wengi kwa kununuliwa. Kwa hivyo, kiharusi alichopata Bouteflika pamoja na kwenda chini bei ya mafuta na gesi yamewafanya watu wajiulize juu ya uhalali wa Bouteflika kubakia madarakani.


Sasa watu wanailinganisha Algeria na Syria pale ulipoanza uasi. Waandamanaji waliwagawia polisi na wanajeshi maua na mawaridi. Algeria sasa ina rais aliye mgonjwa, utawala usiokuwa na kichwa na wananchi wanaotaka kusikilizwa.

Nini cha kufanya?
Kile ambacho watu wamejifunza kutokana na Machipuko ya Kiarabu ni kwamba maendeleo ya kimapinduzi si jambo lenye kutabirika. Hamna mtu anayeweza kujua vipi mambo yatakavyochukua sura ipi baadaye huko Algeria. Kila kitu kinaweza kikatokea.

Upinzani umegawika, hakuna msimamo wa pamoja baina ya Waliberali wa mrengo wa kushoto, wazalendo na Waislamu wenye siasa za wastani. Lakini, kama ilivyotokea Misri Mwaka 2013, pia jeshi linaweza likaingilia kati kutaka nalo ligawiwe madaraka .

Pia, Waalgeria, kutokana na uzoefu walioupata katika vita vya kienyeji, wanatambua kwamba itawabidi walipie gharama kubwa ya kisiasa pindi wanajeshi watachukua mamlaka.

Mkuu wa Jeshi, Ahmed Gaid Salah, mshirika wa Rais Bouteflika, huenda ataweza kujitenga na rais, lakini yeye haonekani kwamba ni mbadala mwenye kuaminika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles